JICHO LA MWEWE: Samatta, haya ya Farid na sisi tunasikia juu juu

NILIKUWA napitia ukurasa wa Instagram wa Mbwana Samatta wikiendi hii. Aliandika waraka maalumu kwenda kwa winga mahiri wa Azam na timu ya taifa, Farid Mussa. Ilitia huzuni lakini ilikuwa inachekesha pia.

Samatta aliandika hivi “Niliposikia Farid anaenda Hispania kwa majaribio nilipata furaha sana, niliamini kwa kipaji alichonacho asingeshindwa majaribio kwa klabu aliyokwenda. Furaha yangu iliongezeka maradufu kusikia Azam imemruhusu kwenda kuanza maisha mapya ya soka Ulaya. Kwa nini nisiwe na furaha kwa sababu naamini maendeleo ya timu yetu ya taifa yatapiga hatua kwa haraka tukiwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania. Lakini kadri siku zinavyosonga mbele nimekuwa simsikii Farid akiwa katika klabu yake mpya na habari nilizonazo ni kuwa bado yupo Tanzania.

Je, kwa nini bado yupo Tanzania wakati kila kitu kilishakwisha? Nani ana jibu la swali hili? Tafadhali kuna nini nyuma ya pazia?”

Sikushangazwa sana na kilio cha Samatta. Machi mwaka huu nilipokwenda kwake pale Genk alikuwa anammwagia sifa Farid kama vile amepagawa. Mwishowe kabisa alikuwa anamfananisha Farid na winga mahiri wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Brazil, Douglas Costa.

Pamoja na kilio cha Samatta, bado nilimshangaa kidogo staa huyu wa Genk. Mpaka leo hajui kwa nini yeye anabakia kuwa mchezaji pekee anayecheza Ulaya kwa sasa? Kabla hajaondoka nyumbani alikuwa hajui kwa nini wachezaji wa Tanzania hawachezi Ulaya?

Nadhani atakuwa ameanza kupata mwanga. Ukweli ni kwamba hakuna dhamira ya dhati sana kwa klabu zetu kufanya biashara ya kuuzwa kwa wachezaji. Suala la Farid ni danadana tu ambazo zimewahi kutokea katika soka letu kwa miaka nenda rudi.

Nasikia tu inasemwa kwamba Farid alikuwa hajapata viza. Viza gani wakati alishajenga uaminifu wa kwenda Hispania na kurudi wakati akienda majaribio? Wengine walisema Farid hakuwa na kibali cha kazi Hispania. Ukweli ni kwamba klabu ya Hispania kama kweli inamhitaji suala la kumtafutia kibali cha kazi ni ndani ya wiki tatu tu na si miezi yote hii.

Imewahi kutokea huko nyuma kwa wachezaji waliokwenda nje ya nchi kwa majaribio. Zamani walikuwa wanakwenda Ulaya kufanya majaribio, siku hizi wanakwenda Afrika Kusini. Wakirudi tunasikia kimya. Baadaye tunaambiwa watarudi tena, halafu ghafla inakuwa kimya tena na tunamwona mchezaji anaendelea kukipiga Uwanja wa Taifa kama kawaida.

Mwishowe nchi hii haina wachezaji wengi Ulaya kama Samatta anavyotaka kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni utayari wa wachezaji wenyewe kwenda Ulaya au nje ya nchi. Wengi hawapo tayari kama wanavyodanganya waandishi wa habari.

Wamezaliwa na kukulia katika sera za Ujamaa ambayo imepoozesha akili zao kwa sababu wana uwezo wa kupata visenti vya nje ya soka.

Sababu nyingine ni klabu zenyewe kutokuwa na utayari na kufanya mizengwe kwa wachezaji. Wakati mwingine mizengwe hii inafanywa waziwazi mbele ya mchezaji, wakati mwingine mchezaji anazungukwa na asijue kama anafanyiwa mizengwe na klabu yake.

Kabla hata haijafika katika zengwe kwa mchezaji binafsi, lakini tayari klabu hazina sera za kuwauza wachezaji nje kwa ajili ya biashara. Ndiyo maana inapofika suala la mchezaji kutakiwa nje inakuwa kazi rahisi kwao kumkatalia au kuweka zengwe.

Klabu zetu kubwa zinahofia kuuza wachezaji wake au kuwaruhusu wachezaji wake kuondoka zikiamini kwamba zinazorotesha tena. Viongozi pia wanaamini kuwa hawatakuwa na majibu ya kuwapa wanachama kama timu itafanya vibaya. Kumbuka viongozi wetu huwa wanafanya maamuzi kwa kuwafurahisha wanachama.

Inakujia akilini kama Simba wanaweza kumruhusu Shiza Kichuya kuondoka kwa sasa? Inakujia akilini kwamba Yanga wanaweza kumruhusu Haji Mwinyi kuondoka kwa sasa? Itakuwa ngumu. Mpaka pale watakapopungua uwezo ndiyo wataruhusiwa kuondoka.

Samatta amesema kweli kwamba timu yetu ya taifa haiwezi kuendelea kama itaendelea kutegemea wachezaji wanaocheza ligi ya ndani. Wachezaji wanaocheza nje ya mipaka yetu ndio ambao wanapaswa kutubeba katika timu ya taifa kwa sababu wanakuwa na mbinu nyingi uwanjani kama Samatta na Thomas Ulimwengu walivyoonyesha siku za karibuni.

Kama tungeweza kumpeleka mchezaji kama Farid nje, kisha wakaenda vijana wengine kina Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Juma Mahadhi, Simon Msuva, Hassan Kabunda, Simon Msuva na wengineo, baada ya miaka michache tungeanza kuvuna matunda.

Vinginevyo tutaendelea kila siku kumshabikia Samatta peke yake pale Ulaya huku tukitegemea kuiona Taifa Stars ikifanya maajabu kupitia kwa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom ambao wanacheza soka katika mazingira ya rushwa na udhaifu mwingi wa ndani na nje ya uwanja.

Mfano mkubwa tunauona wakati klabu zetu zinaposhiriki michuano ya Caf. Hakuna wanachopata kwa sababu wachezaji wameandaliwa kushindana katika soka la ndani zaidi.