JICHO LA MWEWE: Nimeiona Yanga isiyo na Yusuf Manji

Monday March 13 2017

 

By EDO KUMWEMBE kumwembe@yahoo.co.uk

NIMEIONA Yanga isiyo na Yusuf Manji ndani ya hizi wiki nne. Mwenyewe yupo katika kitanda fulani pale Hospitali ya Aga Khan akiwa anajiuguza ugonjwa wa moyo. Mtu na pesa zake. Amewekwa chini ya ulinzi. Sidhani kama ana hofu kubwa.

Hofu kubwa wanayo Yanga na timu yao. Nimeiona Yanga iliyorudi enzi zake kabla ya Yusuf Manji hajaenda Kituo cha Polisi cha Central kisha kitanda cha Hospitali ya Aga Khan. Yanga wapo hoi na wamerudi katika maisha yao halisi. Ni vile tu hawawezi kusema. Wanajikaza.

Yanga isiyo na msaada kutoka kwa Manji huwa inatapatapa kuliko Simba. Huwa haijiwezi kipesa. Kama wangeweza kutumia ukubwa wao kwa muda mrefu sasa si ajabu wangekuwa moja kati ya klabu tajiri Afrika. Inachosha kukumbusha hili mara kwa mara.

Ilianzia kwa Yanga kwenda kuweka kambi Kigamboni kwa ajili ya kucheza na Simba. Katika miaka ya karibuni Yanga huwa inakwenda Pemba. Huwa inapata ushindi zaidi wakiwa kule. Ni suala la kiimani kwao. Huwa siamini katika hilo.

Tangu lini Yanga wakaridhika kwenda Kigamboni kujiandaa na Simba katika zama hizi? Walijaribu kupigapiga chenga lakini ukweli ni kwamba Yanga hawakuwa na fedha. Wangekuwa nazo wangekwenda zao Pemba.

Baadaye wachezaji wa Yanga wakaanza kulumbana na mashabiki wao pamoja na viongozi wao mitandaoni. Donald Ngoma alituhumiwa kuwatoroka viongozi wa Yanga na kukacha pambano la Simba huku akiwa na ripoti kwamba alikuwa mgonjwa. Daktari wa Yanga alikuwa ana kauli tofauti huku akidai kwamba Ngoma alikuwa fiti kucheza.

Yote haya yalitokea kwa sababu Ngoma hakutaka kuwasikiliza viongozi wa Yanga ambao walikuwa wanaonekana kama vile maskini mbele ya macho yake. Angepigiwa simu moja tu na Manji angekimbilia kambini. Ndivyo maisha ya mtu mweusi yalivyo.

Halafu majuzi tu beki, Vincent Bossou alikuwa akilumbana na mashabiki wa Yanga mitandaoni. Mwishoni akapasua jipu kwamba alikuwa hajalipwa mshahara wake kwa muda mrefu. Mashabiki hapo hapo wakawa kimya kabisa. Hii ndio Yanga isiyo na Manji.

Pambano la juzi la Yanga na Zanaco limeonyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Azam TV. Hiki ni kituo ambacho kilikuwa na bifu la muda mrefu na Yanga, hasa mwenyekiti wao bwana Yusuf Manji. Kabla ya Manji kwenda kitandani Aga Khan pambano hili lisingeonyeshwa na Azam TV.

Hata hivyo, viongozi waliobaki wa Yanga wamelazimika kuchukua pesa kutoka Azam TV na kuwapa haki za kuonyesha mechi hii.

Zamani kisingizio kilikuwa kwamba mashabiki walikuwa hawaendi uwanjani kwa sababu wanabaki nyumbani kutazama mechi katika televisheni.

Haya yote yalitokana na maisha bila ya Manji. Wangepata wapi pesa za uhakika za kuipeleka timu Zambia katika mechi ya marudiano? Viongozi waliobaki kwa sasa akili zao inabidi zifanye kazi kwa haraka na wasahau bifu la Azam TV. Kwa sasa wanawahitaji Azam TV kuliko Azam TV inavyowahitaji Yanga.

Bwana Manji akipona na matatizo yake na serikali yakiisha jeuri itarudi tena. Hata hawa viongozi wa sasa ambao wanashirikiana na Azam TV pamoja na wadau wengine wataanza tabia ileile ya zamani ya kujifanya na wao jeuri. Kumbe jeuri yenyewe inategemea mfuko wa mtu mmoja tu. Inashangaza sana.

Hali ikiendelea hivi hivi nadhani muda si mrefu Yanga wataenda kuchukua pesa zao za Azam TV pale TFF. Wamezisusa kwa muda mrefu sasa tangu Azam TV ichukue haki za kurusha mechi hizi. Sijamwona kiongozi yeyote wa Yanga nje ya Manji ambaye ana ubavu wa kweli wa kuzikataa pesa hizi.

Hata hivyo, viongozi hawa na mashabiki wao kwa muda mrefu wamekuwa wakijifanya jeuri kwa kutegemea mfuko wa Manji huku nao wakijifanya hawazitaki hizo pesa. Kama kweli wana jeuri hiyo wasizifuate sasa. Kama kweli wana jeuri hiyo wasingewapa Azam TV haki ya mechi ya juzi.

Mwishowe, nimeiona Yanga isiyo na Manji kwa kipindi cha wiki tatu hizi. Maisha haya yataendelea kwa timu za Tanzania kwa muda mrefu. Kama hazitajua ukubwa wao na umuhimu wake kwa jamii basi kila siku zitaendelea kuishi kwa kutegemea mifuko ya watu.

Yanga haikuwa timu ya kuyumba kwa matatizo ya mwezi mmoja tu ya Manji. Kama ingekuwa baada ya miezi mitatu ningeweza kukubali.

Hata hivyo, ni kitu ambacho nilitarajia kwa sababu siioni Yanga inayoweza kuishi maisha ya Kimanji kama mwenyewe akikaa kando kwa wiki moja tu. hakuna kitakachokwenda.

Hili ni funzo kwao. Lakini hapo hapo naamini kwamba hata Bwana Manji mwenyewe anaifurahia hali hii.

Anafurahi jinsi ambavyo timu inavyomtegemea na ambavyo haiwezi kumudu kusonga mbele bila ya yeye. Hasa katika nyakati hizi ambazo soka ni pesa.