JICHO LA MWEWE: Mpelekeeni Bocco mikanda ya Costa

Muktasari:

>>Lakini ni nani, ambaye hataki kuwa na mshambuliaji mpiganaji kama Suarez?

NAMPENDA John Bocco wa Azam kwa sababu nyingi, lakini moja kubwa ni jinsi ambavyo timu za Simba na Yanga hazimsumbui. Amezifunga mara nyingi. Kuna wakati nilihesabu mabao aliyowafunga hawa washkaji wa Kariakoo mpaka nikapoteza hesabu.

Ghafla tulihitaji timu ambayo itazisumbua Simba na Yanga. Familia ya Bakhresa ikatuletea Azam FC. Tukahitaji mshambuliaji wa aina ya Bocco, ambaye angekuwa anazifunga Simba na Yanga mara nyingi kwa ajili ya kukomesha utawala wao ambao wakati mwingine unachosha.

Ni kweli, Bocco amezifunga mara nyingi Simba na Yanga. Na zaidi ya yote haonekani kama anakaribia kuhamia timu hizo. Zimemtamani muda mrefu lakini hazina uwezo wa kipesa wa kumng’oa kama ambavyo zinawang’oa mastaa wa Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na kwingineko

Nje ya uwanja, Bocco ni mtulivu. Ndani ya uwanja Bocco ni mtulivu vilevile. Hili la utulivu wa ndani ya uwanja sio tatizo. Kuna tatizo moja tu, Bocco ni mnyonge sana. Kuna kitu hakiwezi kuwa mfano mzuri kwa mastraika vijana wanaomtazama Bocco.

Soka la kileo linahitaji ujeuri fulani hivi. Tanzania ya leo mabeki wengi ni wababe kuliko washambuliaji. Tanzania ya zamani niliyoifahamu washambuliaji na mabeki wote walikuwa wababe. Muda mwingi ulikuwa wa mapambano baina ya pande mbili. Ilifurahisha hata kuwaangalia.

Nimetazama mechi nyingi za Azam pindi Bocco anapokabiliana na Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Salim Mbonde na wengineo. Mara nyingi Bocco anakuwa katika upande wa kuonewa na kulalamikia waamuzi kwa rafu za makusudi anazochezewa. Kwa nini Bocco anachezewa rafu mara nyingi? Kwa sababu ni mrefu na anawapa shida mabeki wetu wavivu katika kucheza mipira ya juu. Wale mabeki wa timu kubwa hawaoni uvivu kumpiga kwa makusudi kwa sababu wanafahamu kuwa hawawezi kupewa kadi nyekundu.

Nimewatazama washambuliaji wengi wa zamani kwa makini. Wengi wao waliwafanya mabeki wasiwe na raha. Mmoja wapo alikuwa Marehemu Said Mwamba ‘Kizota’. Wakati ule akicheza kama mshambuliaji, Kizota alikuwa tatizo kwa mabeki. Kitu alichoweza zaidi ya mpira ni kucheza rafu ambazo mwamuzi alikuwa haoni. Ni mabeki ndio ambao walikuwa wanakwenda kwa mwamuzi kumlalamikia Kizota.

Kama Kizota angeenda hewani ilikuwa rahisi kwake kuruka na kiwiko na kukuacha na alama usoni. Ilikuwa ni kitu cha kawaida kwake. Kwanza alikuwa anawatia hofu mabeki waliokuwa wanamkaba, lakini pia alikuwa anajilinda dhidi ya mabeki wakorofi.

Nikiwa kijana mdogo nilipenda kumtazama Idephonce Amlima wa Bandari ya Mtwara. Alikuwa rafiki yangu pia. Licha ya kipaji chake kikubwa, lakini nilikuwa nashangazwa na upande mwingine wa soka lake. Ukorofi mwingi. Baadaye aliniambia jinsi ambavyo ilikuwa vigumu kupata mabao kwa ulaini laini. Yalihitajika mapambano ya jasho na damu na sio kwenda kumlalamikia mwamuzi kila mara.

Kufunga mabao ni mapambano ya kufa na kupona. Mfano wa kileo ni Diego Costa. Ni mshambuliaji kama beki. Mbabe. Anawatia hofu mabeki. Kazi ya kumkaba yeye ni kazi ya kufa na kupona. Ni mkorofi na mabeki wanajiandaa kweli kweli kumkaba akiwa na mpira au hana.

Mwingine ni kama Wayne Rooney. Siku zake za kucheza soka katika kiwango cha juu zinaelekea ukingoni, lakini Rooney katika ubora wake ni zaidi ya mshambuliaji. Anakaba kuanzia mbele na anapambana kuanzia hukohuko. Iwe kwa ngumi, mateke na kila kitu kwake utakipata.

Mtazame Luis Suarez. Anafikia hatua hadi ya kung’ata. Mashabiki wengi walikuwa wanamchukia Suarez kwa sababu walikuwa sio mashabiki wa Liverpool au kwa sasa sio mashabiki wa Barcelona. Lakini ni nani, ambaye hataki kuwa na mshambuliaji mpiganaji kama Suarez?

Bocco lazima ajifunze kwa wachezaji kama hawa hasa ukizingatia kuwa yeye ni mshambuliaji asilia wa kati. Kuna washambuliaji wengi wa kati ambao hawahitaji ukorofi huu kwa sababu kwa aina yao ya soka wao huwa wanatokea pembeni.

Mbwana Samatta ni mshambuliaji wa kati lakini muda mwingi anatokea zake pembeni kuja kushambulia katikati. Ni kama ilivyokuwa kwa Thierry Henry. Lakini kuna washambuliaji wa kati ambao huwa wanasimama pale katikati kusubiri mipira. Hawa ndio haswa huwa wanapambana na mabeki wa kati. Bila ya kuwa mkorofi kwa mabeki hawa hauwezi kutamba zaidi.

Wakati mwingine unatazama baadhi ya picha za Amiss Tambwe unagundua kuwa na yeye ni mkorofi. Ipo picha anaonekana amezishika korodani za beki wa Simba, Juuko Murshid. Ni mapambano ya ndani ya uwanja kwa sababu soka sio kazi rahisi.

Bocco angeweza kuwa mzuri zaidi kama angekuwa mkorofi zaidi. Mambo haya wakati mwingine yanakwenda sambamba. Soka ni mchezo wa mapambano. Katika maisha yake ya soka alikuwa anahitaji kadi kadhaa nyekundu. Unaweza kudhani ni ujinga kusema hivi, lakini ukweli ni kwamba inawezekana Bocco hadi wakati anastaafu soka akawa amecheza asilimia 50 tu ya uwezo wake.