JICHO LA MWEWE: Kuna Kim Poulsen mmoja tu

Muktasari:

>> Wachezaji wetu wengi wana maumbo madogo ambayo ni vigumu sana kwao kung’ang’ania mpira na wachezaji wa timu nyingi za nje hasa wale wa mataifa ya Afrika Magharibi na kwingineko duniani.

NILIKWENDA kumpa mkono Kim Poulsen wakati wa mapumziko ya pambano kati ya Taifa Stars na Ivory Coast pale uwanja wa Félix Houphouet-Boigny Juni 2012. Sikuwa na deni naye baada ya kile ambacho wachezaji wa Stars walikionyesha hadi wakati wa mapumziko.

Ndiyo, tulikuwa tumefungwa 1-0 mpaka wakati huo kwa bao la Solomon Kalou baada ya Juma Kaseja kumuanzishia mpira Kevin Yondani katika eneo baya na akaporwa mpira. Kuanzia hapo Stars walinionyesha nilichokitaka.

Kim aliua winga zote katikati akawapanga watu wanne, Frank Domayo, Amri Kiemba, Salum Abuubakar na Mwinyi Kazimoto aliyekuwa katika ubora wake. Ivory Coast walikuwa wanawaza likizo wakiamini ingekuwa mechi rahisi, lakini Kim hakuwapa urahisi huo. Waliutafuta mpira kwa tochi.

Mwinyi, Domayo, Sure Boy na Kiemba walikuwa wakipiga pasi fupi fupi za haraka ambazo ziliwalazimisha Ivory Coast kukimbiza mpira bila ya kupenda. Mwisho wa mechi walitufunga 2-0, bao la pili likifungwa na Didier Drogba baada ya Agrey Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Walichokifanya Stars siku ile ndicho hiki ninachokiona kwa Serengeti Boys kwa sasa. Aina ya mpira ni ule ule tu, ni mpira wa Kim. Pasi za haraka haraka na fupi fupi. Kama Kim angeendelea kuwepo kwa muda mrefu mwaka huu tungeweza kucheza Afcon pale Gabon. Jamal Malinzi alikosea sana kumfukuza Kim baada ya uchaguzi uliopita. Tungekuwa mbali.

Hata hivyo, bado hatujachelewa sana kuwa na Kim. Anaweza kuufumua mpira wetu kwa sababu mbili. Kwanza kabisa anatuonyesha staili ya soka ambayo Watanzania tunapaswa kuitumia. Mpaka leo Tanzania hatuna staili yetu ya soka. Ukienda viwanja mbalimbali kuanzia vile vya Ligi Kuu hadi mchangani hauwezi kujua staili ya soka ya Tanzania ni ipi hasa.

Timu moja inabutua, nyingine inapiga pasi za haraka haraka nzuri, nyingine inakimbiza tu kupitia kwa mawinga. Hauwezi kujua kwa urahisi mpira wetu ni upi sana. Hata hivyo, Kim anatuonyesha staili ambayo inatufaa sana kutokana na maumbile ya wachezaji wetu wa kileo.

Wachezaji wetu wengi wana maumbo madogo ambayo ni vigumu kwao kung’ang’ania mpira na wachezaji wa timu nyingi za nje hasa Afrika Magharibi na kwingineko. Kwa staili hii ina maana mpira utakuwa unatembea zaidi kuliko wachezaji.

Barcelona walikuwa wanatumia staili hii na timu ya taifa ya Hispania nayo ikatumia staili hii. Hii ilitokana na maumbo yao. Wakati Hispania wakitwaa kombe la dunia mwaka 2010 pale Afrika Kusini, timu yao iliweka rekodi ya kuwa timu yenye wachezaji wafupi zaidi kutwaa kombe la dunia.

Lakini, kama Kim tunaweza kumtunza basi anaweza kutuibulia vipaji zaidi kwa sababu ana uwezo wa kutengeneza timu nyingi za vijana za Taifa. Anaweza kututengenezea ile ya chini ya umri wa miaka 10, kisha 15, akaendelea na hii hapa inayotamba kule Gabon.

Hapana shaka, mastaa hawa hawa ndio ambao watajenga kikosi cha timu ya taifa ya chini ya umri wa miaka 21. Na kadri ninavyowaona basi hawana muda mrefu wanaweza kutuwakilisha katika michuano ya Olimpiki.

Kitu kinachotia wasiwasi ni klabu gani zitalea vipaji ambavyo Kim amevitengeneza. Wakiangukia katika klabu zetu nadhani watakuwa wameangukia katika mikono ambayo sio salama sana. Nadhani kuna maskauti wengi pamoja na mawakala waliojaa Gabon ambao, watawabeba kuwapeleka timu za nje.

Hivi ndivyo mpira unavyoundwa. Kwa sasa simuoni mtu mwingine ambaye anaweza kututengenezea muundo (Structure) zaidi ya Kim. Tatizo jingine linaweza kuja katika namna pia ya kuihudumia timu ya taifa ya wakubwa. Kim alipaswa kutushauri namna ya kumpata kocha wa timu ya wakubwa ya taifa, ambaye fasalafa zao za soka zitaendana.

Kocha wa aina hii ndiye ambaye ataweza kuwapa vijana uwezo wa kujiamini huku akichota wengi kutoka katika timu ya vijana ya chini ya miaka 21 na wakati mwingine chini ya miaka 17 kama ambavyo, nimeanza kuona kuna vijana wa sasa wa Kim wanaoweza kufanya mazoezi na timu ya wakubwa.

Kuna Kim Poulsen mmoja tu. Huyu hapa ambaye aina yake ya soka analotaka ndilo linalowafaa Watanzania. Lakini pia ni tuna Kim huyu huyu, ambaye anajua jinsi ya kukusanya vijana wadogo na wakacheza mpira unaovutia.

Tusipomtumia Kim vizuri basi tunaweza kubakiwa na majuto kama ambayo kwa nyakati tofauti tuliwahi kuachiwa na Professa Victor Stanculescu na baadaye kocha wa Zaire, Tambwe Leya. Nyakati ni hizi ambazo tunaweza kumpa Kim pesa na muda atupangie programu ya miaka 10 hivi ambayo tukijiwekea malengo ya kucheza kombe la dunia 2026 basi tuwe tunazungumza kitu ambacho tuna uhakika nacho kuliko ujanja ujanja tunaoufanya sasa.