JICHO LA MWEWE: Kaseja ni mchezaji wa kulipwa zaidi ya wengi

Monday May 15 2017

 MCL

By EDO kumwembe

NILIMUONA Juma Kaseja Jumanne iliyopita pambano lao dhidi ya Yanga akiwa katika jezi yake ya Kagera Sugar. Alionekana kuwa mwepesi. Anaurudisha umri nyuma kama ilivyo kawaida yake. Bao la kwanza alizidiwa ujanja na Simon Msuva. Bao la pili la Obrey Chirwa alistahili kufungwa.

Juma anarudisha umri wake kila siku. Sijui ni kitu gani kilichomgombanisha na kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo. Mpaka leo bado sijafahamu vizuri. Vinginevyo achilia hilo, Kaseja ameendelea kuwa mchezaji bora wa kulipwa ninayemfahamu.

Kabla ya mechi ya Yanga alicheza vizuri mechi ya Simba. Kabla ya hapo alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu ya Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu. Nina sababu nne ambazo zinanifanya niamini Kaseja ni mchezaji bora wa kulipwa.

Kwanza kabisa Kaseja anapenda mazoezi na anapenda kucheza mchezo wenyewe. Waulize watu walio karibu yake.  Kaseja anapenda sana mazoezi. Wachunguze wachezaji wetu wengine kama wana tabia ya kupenda sana mazoezi kama Kaseja. Kama wote wangekuwa kama yeye basi si ajabu tungekuwa tunashuhudia ligi tamu zaidi.

Pia, Kaseja amekuwa mchezaji wa kulipwa kwa sababu ya maamuzi yake aliyowahi kuchukua katika soka. Ni maamuzi ya kutocheza nje tu ambayo yanatia shaka. Labda alihofia maneno kuhusu kimo chake au aliridhika zaidi na pato lake la Uwanja wa Taifa.

Vinginevyo Kaseja ameonyesha wazi kwamba ni mwanasoka sahihi wa kulipwa kwa kuwahi kucheza klabu zote mbili kubwa nchini, Simba na Yanga, tena kwa uadilifu, ingawa watu wote wa Yanga walifahamu kwamba Kaseja ni shabiki wa Simba.

Naipenda tabia hii kwa sababu inawaamsha viongozi wetu na mashabiki wetu na wachezaji makinda waelewe kwamba soka ni kazi tu. Wachezaji hawapaswi kuwa mashabiki. Hii ndio tabia ya wanasoka wa kulipwa inavyokuwa.

Lionel Messi anasumbuana na Barcelona mpaka sasa, lakini hii ndiyo timu ambayo akiwa na miaka 13 ilimpeleka Hispania ikamlipia sindano ya ugonjwa ambao ulikuwa unamfanya awe anadumaa. Leo anafanya mazungumzo kama mfanyakazi na sio shabiki. Mpaka sasa amegoma kusaini mkataba mpya mpaka kieleweke.

Kitu kingine ambacho unaweza kumsifu Kaseja ni ukweli kwamba amegoma kuzeeka na amegoma kuondolewa katika soka na mashabiki. Baada ya kuondoka Simba na Yanga akaenda Mbeya City. Wakati watu tukiamini kwamba ameisha, akaibukia Kagera Sugar ambako amekuwa aking’ara.

Hii ndiyo sifa ya mchezaji wa kulipwa. Huwa unajiambia mwenyewe kwamba umechoka na hauwezi kuendelea. Hauwezi kupangiwa na mashabiki. Achana na Kaseja ambaye sio tajiri jiulize kuhusu kina John Terry na utajiri wao wote waliokusanya katika soka, lakini bado wanataka kuendelea kukipiga katika kiwango cha juu wakiwa na umri wa miaka 36.

Kuna wachezaji wengi tumewaondoa katika soka kwa sababu ya kuvumisha tu kuwa walikuwa ni wazee. Wenyewe walikubali na wakajiondoa. Ndio tatizo la soka letu. Mashabiki wanapiga soga ambalo linawaingia wachezaji na baadaye wachezaji wanakubali.

Francesco Totti ni mkubwa kuliko Nsajigwa Shadrack, lakini tulimwondoa Nsajigwa katika soka mapema zaidi.

Leo nafanya naye mazoezi pale Taswa Uwanja wa Chuo cha Ustawi wa Jamii na akijifua zaidi anaweza kucheza Ligi Kuu yetu bila ya wasiwasi.

Kaseja ameukataa uzee feki na hii ndio tabia ya wanasoka wengi wa kulipwa. Ukiwa mwanasoka wa kulipwa unajaribu kushindana na muda kila siku. Sisi wachezaji wetu hawashindani na muda. Wakiambiwa wazee wanakimbia.

Kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla anaonekana kuwa na umri mkubwa, lakini kila nikitazama mechi ambazo Kavilla anacheza dhidi ya timu mbalimbali za Ligi Kuu huwa sioni tofauti kubwa dhidi ya viungo wenzake. Bahati yake Kavilla.

Kama angekuwa anacheza Simba na Yanga ingekuwa tumemsahau katika soka kwa muda mrefu sasa.

Pia, kitu kingine ambacho kinanifanya nimpongeze Kaseja ni jinsi alivyofanikiwa kufanya kazi tena na Marcio Maximo wakati aliporudi nchini wakakutana katika klabu ya Yanga.

Inabidi uwe mchezaji wa kulipwa kucheza katika mazingira yoyote yale.

Hapa alikutana na kocha ambaye siku za nyuma ilionekana kuna mgogoro mkubwa kati yao, lakini bado alifanikiwa kufanya kazi yake kama kawaida. Inatokea kwa wachezaji wanaojielewa barani Ulaya. Wanaendelea kufanya kazi zao kama kawaida.

Ni kama ilivyotokea kwa Juan Mata wa Manchester United. Aliwekwa benchi na Jose Mourinho pale Chelsea. Baadaye akauzwa kwenda United. Hata hivyo, wamekutana tena na Mourinho na maisha yanaendelea kama kawaida.

Hivi ndivyo mchezaji wa kulipwa anavyopaswa kuwa na sio kukimbilia katika magazeti kwenda kuonyesha kutoridhishwa na ujio wa kocha mpya.

Inatokea sana kwa wachezaji wetu ambao hawajielewi katika maisha yao. Wengi hawa tabia za uanasoka wa kulipwa.