JICHO LA MWEWE: Hata mimi natamani Okwi arudi Simba

Muktasari:

  • Kwa mchezaji wa kipaji cha Okwi inashangaza sana. Lakini akiwa hapa nchini tuliambiwa na watu wa Simba kwamba Okwi alikuwa hapendi mazoezi.

NILISOMA mahala katika tovuti hii wiki iliyopita. Namna ambavyo Simba ina mkakati wa nguvu kumrudisha Emmanuel Okwi. Nilitabasamu sana na mwishowe nikacheka. Natamani hili jambo litokee.

Kwa nini natamani litokee? Kwa sababu kuna baadhi ya vitu duniani lazima vitokee ndipo kelele zipungue. Natamani hili litokee kwa sababu likitokea ndio utakuwa mwisho wa kelele za kutamaniana kati ya Simba na Okwi.

Kwa sasa imeanza kuchosha kusikia namna ambavyo Simba wanavyomtamani Okwi kila siku. Imeanza kuchosha kusikia kuwa hata Okwi mwenyewe anatamani kurudi Simba. Sasa kwa nini isitokee tu ili jambo hili liishe jumla. Kuna wakati Okwi alikuwa anaonekana mkubwa kuliko klabu. Mara nyingi klabu huwa hazipendi kusikia kuna mchezaji mkubwa kuliko timu. Lakini kuna wakati ilionekana kama Okwi alikuwa mkubwa kuliko timu hii iliyoanzishwa mwaka 1935.

Sasa imeanza kujidhihirisha tena hivyo. Hivi Simba wanaamini kwamba matatizo yao makubwa yapo kwa Okwi? Ni kweli wameshindwa kupata mbadala sahihi wa kuwasahaulisha Okwi? Ni kitu kinachoshangaza sana.

Simba walipita kina Willy Mwaijibe, Nico Njohole, Zamoyoni Mogella, Hamis Gaga na wachezaji wengi wenye vipawa vya kushangaza, lakini Simba ya leo imepiga magoti kwa Mganda mmoja tu aliyekulia hapa hapa.

Ndani ya miaka hii 10 iliyopita, mfalme wa Simba alikuwa Mussa Hassan Mgosi. Baadaye ghafla akatokea Mbwana Samatta akawa mfalme na kumweka Mgosi pembeni. Mbwana hakudumu sana akauzwa kwenda TP Mazembe ya DR Congo.

Baada ya hapo ufalme ukawa wa Okwi. Baada ya Okwi kuuzwa kwenda Afrika Kaskazini, Simba haikuona kama inaweza kuishi bila ya Okwi. Akarudi tena. Ameuzwa kwenda Ulaya, Simba bado imeona haiwezi kuishi bila ya yeye. Inashangaza na kuchekesha sana.

Kwa upande wa Okwi naye, huyu rafiki yangu huwa ananichekesha sana. Ana bahati mbaya sana. Ana kipaji maridadi mno kuliko wachezaji wengi wa ukanda huu ambao wamewahi kutoka bara hili. Lakini ana bahati mbaya kwamba, nchi iliyomlea kisoka ilimlea vibaya.

Ustaa wa Okwi na ule wa wachezaji wengi wazawa unamfanya mchezaji kujisahau sana na kujikuta na wakati mgumu akienda kucheza soka la kulipwa Ulaya. Nasikia Okwi hafanyi vizuri Ulaya na ni majuzi tu ameingia katika kikosi cha kwanza.

Kwa mchezaji wa kipaji cha Okwi inashangaza sana, lakini akiwa hapa nchini tuliambiwa na watu wa Simba kwamba Okwi alikuwa hapendi mazoezi. Baadaye tukaambiwa na watu wa Simba ujinga ambao daima ulikataa kuniingia akilini. Kwamba Okwi akifanya mazoezi sana hachezi vizuri uwanjani.

Sasa kwa kulelewa hivi ilikuwa lazima Ulaya imshinde Okwi. Malezi haya ndiyo ambayo yamesababisha Tanzania isitoe wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya. Pia ndani ya uwanja Okwi akifunga bao maridadi basi nje ya uwanja atapewa pesa nyingi za wadau wake wa Simba.

Pesa hizi ni nje ya mshahara wake, nje ya posho zake, nje ya haki zake za msingi. Kuna lile bao ambalo Okwi aliunyanyua mpira kwa umaridadi mkubwa juu ya kichwa cha kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’. Nasikia alipata zaidi ya Shilingi 10 milioni nje ya uwanja.

Kwa Ulaya hauwezi kupata pesa hizi. Kwa Ulaya mfumo wa soka ni tofauti sana. Kwa Ulaya wachezaji hawalelewi katika misingi ya soka la ujamaa kama ilivyo nchini. Tanzania staa mkubwa huwa anapewa pesa na mashabiki, Ulaya staa mkubwa huwa anaombwa pesa na mashabiki.

Sishangai kusikia Okwi anatamani kurudi zake Simba na yupo tayari kufanya hivyo muda wowote ule Simba ikiafikiana na timu yake. Nani wa kumpa pesa za nje ya mfumo Ulaya? Nani wa kuafiki wazo la kijinga kwamba, akifanya mazoezi sana hachezi vizuri? Hata Lionel Messi hawezi kueleweka akiitaja sababu hiyo.

Kisaikolojia, Simba na Okwi hawawezi kusonga mbele kama wanafikiriana namna hii. Ni sawa na mtu na mpenzi wake walioachana baada ya penzi tamu. Kama wakiendelea kufikiriana sana basi ni wazi kwamba, hawawezi kuwa na mahusiano imara kwa wenza wao wa wakati huo.

Siyo mbaya kwa Okwi kwa sababu ni mtu mmoja tu. Lakini ni mbaya kwa Simba kwa sababu wanajaribu kujishusha angali wao ni taasisi imara na kongwe tangu mwaka 1935. Siamini kama Okwi ni suluhisho lao la matatizo ya ndani ya uwanja.

Hata hivyo, wapendanao kamwe usiwaingilie. Kitu cha msingi ni kuwasapoti kwa kile wanachokiwaza.

Kama kikifanikiwa, basi kelele zinapungua. Na ndio maana natamani sana Okwi arudi Simba ili kelele zipungue baina yao.