Ismail Khalfan alifunga kama Sanchez, akatibiwa kama mzaha

Muktasari:

Bao lake linafungwa na wachezaji wakubwa wenye akili nyingi. Msimu uliopita lilifungwa na staa wa Chile wa Arsenal, Alexis Sanchez katika pambano la kwanza la Arsenal dhidi ya Manchester United pale Emirates.

MUNGU amrehemu Ismail Khalfan. Alianguka juzi na kufariki katika pambano la timu yake ya vijana ya Mbao dhidi ya Mwadui ya vijana. Kazi ya Mungu haina makosa. Dakika chache kabla ya hapo alifunga bao maridadi sana.

Bao lake linafungwa na wachezaji wakubwa wenye akili nyingi. Msimu uliopita lilifungwa na staa wa Chile wa Arsenal, Alexis Sanchez katika pambano la kwanza la Arsenal dhidi ya Manchester United pale Emirates.

Kwa mujibu wa picha za video zilizosambaa mitandaoni, baadaye kidogo Ismail alikwatuliwa katika rafu ya kawaida kabisa katika soka. Alikwatuliwa miguuni, lakini akakaa, akashika kifua na kuanguka. Inaonekana kilichomsibu hakikutokana na faulo aliyochezewa.

Kwa jinsi alivyoshangilia kwa kifua kwa kasi kubwa hauwezi kubisha kama akitokea daktari akasema Ismail aliutibua moyo wake wakati akisugua kifua chake katika nyasi za uwanja wa Kaitaba. Hakuguswa kichwa wala kifua na mchezaji mwenzake aliyemchezea rafu.

Katika hali ya kawaida, kifo hupangwa na Mungu, lakini unaweza kutabiri ambacho madaktari walibeba kwa ajili ya kumpa huduma ya kwanza kwenda kumtibu Ismail. Katika soka letu, katika mechi kama hizo madaktari hubeba pamba, barafu, maji ya kunywa, dawa za kidonda, basi.

Kama mechi za Ligi Kuu zinaambatana na vifaa kama hivi, vipi katika mechi za vijana ambazo haziingizi pesa? Vipi katika mechi za daraja la kwanza? Hiki ndicho kinachotokea. Wachezaji na mashabiki wanaokwenda uwanjani wanaweka rehani roho zao.

Katika hali ya kawaida ya kuokoa uhai wa mchezaji kama Ismail, uwanjani lazima kuwe na mashine za Oksijeni, lazima kuwa na mashine za kuamsha mapigo ya moyo (Resuscitation machine).

Vitu kama hivi ndivyo ambavyo viliokoa maisha ya kiungo wa zamani wa Bolton, Fabrice Muamba alipoanguka Machi 2012 wakati akicheza dhidi ya Tottenham dimba la White Hart Lane.

Wapo ambao wanafariki hata baada ya haya yote kufanyika. Mfano halisi ni Marc-Vivien Foe, ambaye alifariki wakati akiwa amewekewa mashine za kumsaidia kupumua. Lakini walau juhudi zionekane kabla ya jambo baya au zuri kutokea.

Vitu kama hivi havipo uwanjani wala katika gari la wagonjwa ambalo huwa linakuwepo uwanja wa Taifa wakati mechi za soka zinachezwa katika mikoa yote ya Tanzania kwa wakati mmoja.

Haya ni maisha ya kubahatisha ambayo yanatokana na kuufanya mchezo wa soka kutokuwa maisha ya watu wala ajira za watu.

Jaribu kujiuliza, mchezaji aliyevunjika kama Eduardo wa Arsenal au Demba Ba aliyevunjika akiwa nchini China, dawa ya kidonda itamsaidia nini? Inachukua zaidi dakika 15 kwa madaktari wenye vifaa vya kisasa kumuondoa uwanjani mchezaji ili mguu wake usipate madhara zaidi wakati wa operesheni.

Atafanya nini daktari mwenye pamba na dawa na kidonda bila ya gari la kubebea wagonjwa nje ya uwanja? Kupuuziwa kwa mambo katika soka la mikoani au la madaraja ya chini ni jambo la kawaida tu.

Kwa mfano, katika pambano la daraja la kwanza la Coastal Union dhidi ya KMC ya Dar es Salaam pale Tanga, alikuwepo askari mmoja tu uwanjani wakati mashabiki wa Coastal walipoamua kumpiga mwamuzi.

Huu ni mzaha kama ulivyo mzaha wa matibabu. Na bahati mbaya zaidi ni kwamba tunaishi kwa matukio. Tunasubiri janga litokee halafu tuwe wanafiki wa kujibu mapigo. Ni maisha ya kawaida ya Mtanzania wa kawaida. Tunaishi kwa mazoea.

Jaribu kujiuliza pia, ni kweli wachezaji wetu wa soka wanapimwa afya zao kwa ukamilifu? Kama jibu ni hapana, basi hapa tuna matatizo makubwa mawili ambayo tunapaswa kuyashughulia wakati tukiendelea kuhuzunika na msiba wa Ismail.

Kwanza kabisa ni vipimo vya afya kwa wachezaji wetu. Pili ni matibabu yanayoeleweka kwa wachezaji wetu. Bahati nzuri ambayo inatuokoa mpaka sasa ni kwamba walau soka letu sio la ushindani sana ndani ya uwanja.

Hii inapunguza majeraha ya hatari. Kama tungekuwa katika matumizi makubwa ya mabavu kama kwa wenzetu, halafu kwa vifaa hivi vya matibabu vya ujanja ujanja, hali ingekuwa mbaya zaidi.