Ijue filamu mpya ya Bongo Movie ya Uchaguzi wa TFF

Tuesday April 11 2017

 

By FRANK SANGA

KATIKA nchi za Afrika viongozi huwa wanang’ang’ania kukaa madarakani kwa muda mrefu, wakiamini kuwa hakuna mtu mwingine anayeweza kuchukua nafasi zao.

Huwa wanaogopa kuachia madaraka kwa sababu wanajua madhambi waliyoyafanya katika kipindi cha utawala wao, hivyo huogopa mkono wa sheria.

Lakini, wengi wao huwa wanang’ang’ania madaraka kwa sababu ya ulafi. Hujisahau na kudhani nchi au taasisi wanazoziongoza ni mali yao binafsi.

Madhara yake huwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe, kuporomoka kwa uchumi, migogoro ya mara kwa mara na mbaya zaidi kukosekana kwa demokrasia sehemu husika.

Tumeona hilo katika maeneo mbalimbali, ndio maana huwezi kushangaa ukisikia nchi mbalimbali zinabadilisha katiba zao ili kiongozi wao aongezewe muda wa kugombea tena.

Tumeona baadhi ya taasisi zikiweka sheria ngumu ambazo zinawazuia watu wengine wasigombee nafasi kubwa kwa sababu hawana uzoefu au kwa sababu nyingine yoyote.

Lakini, kuna maajabu yametokea katika taasisi mmoja iliyopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Unaposikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kufanya uchaguzi Agosti 12, ikiwa ni miezi minne kabla ya tarehe rasmi ya uchaguzi, lazima ushtuke na kujiuliza maswali mengi.

Utajiuliza maswali mengi kwa sababu usidhani wanafanya uchaguzi huo kwa nia njema. Hawa wanapatikana katika nchi za Afrika tena kusini mwa Jangwa la Sahara, hivyo hawawezi kuwa na nia njema.

Wanafanya uchaguzi huo kwa sababu tayari wamemaliza kampeni zao mikoani. Tumeshuhudia kuanzia mwaka jana mikoa mbalimbali ilifanya chaguzi zao.

Lakini, hakuna mkoa ambao ulifanya uchaguzi bila matatizo. Chaguzi ziliahirishwa na sehemu nyingine watu ambao wanampinga rais wa sasa wa TFF waliondolewa kwa madai ambayo hayakuwa ya msingi.

Watu waliochaguliwa ni wale tu ambao wanamuunga mkono na kumlamba miguu rais wa TFF aliyepo madarakani. Ndio maana kuna watu walijigeuza kuwa Vasco da Gama na kusafiri mikoa yote nchini kuhakikisha hilo linawezekana.

Kazi imekwisha, mikoa karibu yote imepata viongozi wake, wote wanamuunga mkono rais wa TFF, wote wapo tayari kumpigia magoti kila anachoongea, hakuna mtu wa kumbishia lolote, wapo tayari kufa kwa ajili yake, watampa kura.

Kwa sababu kazi hiyo imekamilika, TFF imeamua kutangaza uchaguzi mkuu ufanyike Agosti ili wasije kubadilisha mawazo baadaye.

Kwa kawaida uchaguzi wa TFF hufanyika Novemba na Desemba, japo uchaguzi uliopita ulifanyika Oktoba, lakini safari hii utafanyika miezi minne kabla ya muda wake kwa sababu kazi ya kampeni mikoani imekamilika.

Huu ni uchaguzi ambao hautakuwa na ushindani wowote, kwa sababu rais wa sasa amemaliza kazi na ili kuzuia wengine wasifanye kampeni ndio maana uchaguzi umepangwa kufanyika Agosti.

Unaweza kumsifu kwamba ameitisha uchaguzi ili demokrasia ichukue nafasi yake, lakini ukweli ni kuwa demokrasia imefinywa na uchaguzi huo ni kama filamu yoyote ya Bongo Movie.

Kwa kifupi uchaguzi huo ambao huchagua rais, makamu wake na kamati ya utendaji ni kama tayari umefanyika na ndio maana nasisitiza kuwa Agosti 12 tutakwenda kuona filamu tu.

Kuna mtu anataka kugombea nafasi ya urais, anapoteza muda wake na sifa yake. Kwa mtu makini hawezi kugombea nafasi hiyo labda naye awe tayari amepita mikoa yote. Vinginevyo tunaisubiri filamu hiyo.