INAWEZEKANA : Sevilla ina kila dalili ya kufika mbali msimu huu

Muktasari:

Timu nyingine ya Hispania ambayo imekuwa kileleni barani Ulaya katika miaka ya karibuni ni Sevilla. Ingawa timu hiyo haijakuwa na uwezo wa kuingia katika mbio za kushinda La Liga, lakini imekuwa na mafanikio makubwa sana katika Ligi Ndogo ya Ulaya, maarufu kama Europa League.

KLABU za Barcelona na Real Madrid zimetawala Ligi Kuu ya Hispania, La Liga kwa miaka mingi. Lakini katika misimu ya hivi karibuni La Liga imekuwa na ladha nzuri zaidi kutokana na Atletico Madrid kuzipa ushindani mkubwa klabu hizo za Barcelona na Real Madrid kiasi cha kushinda taji la ligi hiyo mwaka 2014.

Timu nyingine ya Hispania ambayo imekuwa kileleni barani Ulaya katika miaka ya karibuni ni Sevilla. Ingawa timu hiyo haijakuwa na uwezo wa kuingia katika mbio za kushinda La Liga, lakini imekuwa na mafanikio makubwa sana katika Ligi Ndogo ya Ulaya, maarufu kama Europa League.

Sevilla imeshinda taji la ligi hiyo ya Ulaya mara tatu mfululizo na kuonyesha kwamba, ina timu nzuri yenye uwezo wa kupambana na klabu nzuri kutoka sehemu nyingi barani humo. Hivyo mashabiki wengi wa soka wa Hispania wamesubiri kwa hamu kuiona timu hiyo ikifanya makubwa katika La Liga.

Hatimaye msimu huu kuna dalili fulani kuwa, Sevilla ni klabu ambayo itakuwa kileleni katika La Liga kama itakaza midogo tu ilipo kwa sasa.

Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya pili katika La Liga, nyuma ya Real Madrid ikitofautiana nao kwa pointi moja tu, huku wakiwazidi Barcelona kwa pointi moja.

Kitu ambacho kinawashangaza wengi ni kwamba Sevilla wamekuwa na msimu mzuri sana huku wakiwa na kocha mpya, Jorge Sampaoli. Chini ya kocha wao wa zamani Unai Emery, Sevilla walishinda Europa League mara tatu mfululizo. Lakini, baada ya msimu uliopita kumalizika kocha huyu aliamua kuvunja mkataba wake na kuhamia Paris Saint Germain nchini Ufaransa.

Hivyo, wengi wameamini kwamba Sevilla wangepata shida msimu huu kutokana na Unai Emery kuondoka. Pia wachezaji tegemeo wa Sevilla waliuzwa katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana. Wachezaji kama Gregorz Krychowiak na Ever Banega waliondoka kikosini.

Lakini, chini ya uongozi wa Sampaoli timu hiyo imepiga hatua na kuwapa presha kubwa Barcelona, Real Madrid na Atletico Madrid katika Ligi Kuu. Juzi Jumapili iliweza kuvunja mwiko wa Real Madrid wa kushinda mfululizo kwa kuwachapa mabao 2-1 katika ligi hiyo maarufu ya Hispania.Hakika, moja ya sababu kubwa ya mafanikio ya Sevilla msimu huu ni mwenyekiti wao wa usajili, Ramon Verdejo mwenye jina la utani la Monchi.

Monchi amekuwa na jicho zuri la kutambua na kusajili wachezaji wenye vipaji. Kwa miaka mingi amesajili wachezaji kwa bei nafuu na kuwauza kwa bei kubwa. Ni wachezaji kama Dani Alves, Ivan Rakitic, na Seydou Keita.

Hata kama Sevilla waliuza wachezaji tegemeo katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana, Monchi aliweza kuziba pengo la nyota hao kwa kusajili wachezaji wazuri wenye bei ndogo. Wachezaji kama Wissam Ben Yedder, Franco Vasquez, Gabriel Mercado na Samir Nasri ambaye amekuja Sevilla kwa mkopo.

Sababu nyingine ya Sevilla kufanya vizuri msimu huu ni kwamba kocha wao, Sampaoli, ambaye ni kocha wa zamani wa Chile ni mwanaharakati na chini ya uongozi wake Sevilla wanaendelea kupata matokeo.

Kipigo cha 2-1 ilichowapa Mabingwa wa Ulaya na Dunia, Real Madrid katika mechi ya La Liga ni ishara kwamba, Sevilla msimu huu wamejipanga sio tu kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa bali wanataka kupiga hatua katika La Liga na kwa hakika inawezekana.