Huu ni wakati wa Wenger kumuamini Giroud

Muktasari:

Ni muda mrefu sana tangu Arsenal iifunge Man United. Ni jambo la kushangaza kwani hata Man United ikiwa kwenye wakati mgumu ni vigumu kupoteza mechi dhidi ya Arsenal.

OLIVIER Giroud mshambuliaji wa klabu ya Arsenal ya Engalnd Jumamosi iliyopita alinikumbusha mbali mno, enzi nikisakata soka. Alifunga bao safi sana ingawa klabu yake ya Arsenal ilipoteza mechi dhidi ya mtani wake Manchester United ‘Mashetani Wekundu’.

Ni muda mrefu sana tangu Arsenal iifunge Man United. Ni jambo la kushangaza kwani hata Man United ikiwa kwenye wakati mgumu ni vigumu kupoteza mechi dhidi ya Arsenal.

Mashabiki wengi wa Arsenal wamehuzunishwa sana na kipigo hicho kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Emirates.

Mabao ya Man United yalifungwa na Kieran Gibbs aliyejifunga na Wayne Rooney aliyefunga akipokea pasi ya Angel Di Maria.

Kwa hakika hii ni mechi ambayo Arsenal watajilaumu wenyewe. Dakika za kwanza ndani ya dakika ishirini hivi walipata nafasi nzuri mno za kutumia lakini walizipoteza zote. Kumbuka Jack Wilshere alibaki pekee yake ndani ya eneo la hatari na kupoteza nafasi.

Hata hivyo sifa zimwendee David de Gea kipa wa Man United. Kwa kweli alifanya kazi ya ziada kwani mipira ambayo aliweza kuiokoa kipindi cha kwanza kama ingepita basi Man United ingekuwa hoi. Kumbuka kitu ambacho Wilshere alishindwa kufanya ndicho Rooney alikifanya alipofunga bao la pili.

Mechi ikiwa mapumzikoni ilikuwa sare ya bila kufungana, nikitazama mechi hiyo na rafiki zangu nikiwa shabiki mkubwa wa Man United niliwaambia wenzangu kuwa Man United ikitangulia kuifunga Arsenal basi watashinda hiyo mechi.

Ama kwa kweli walipata bao kupitia kwa Gibbs aliyejifunga baada ya Antonio Valencia kupiga shuti ambalo Gibbs alilisindikiza wavuni akiwa katika harakati za kuokoa na kuiweka nyuma timu yake kwa bao 1-0. Ilikuwa raha mustarehe. Mechi hiyo niliitazama jijini Eldoret nikiwa huko kwa shughuli zangu.

Arsenal ilisonga mbele ili kusawazisha bao hilo lakini ikiwa ni makosa makubwa kwao kwani shambulizi la kushtukiza ‘counter attack’ walilofanyiwa na Man United kwa mpira ulioanzia kwa Marouane Fellaini ulimfikia Angel Di Maria ulimaliza mchezo huo.

Kwani Di Maria alimuandalia Rooney pasi safi sana, naye Rooney alimalizia kwa kufunga bao zuri. Hata hivyo, Arsenal wamshukuru Mungu kwani Angel Di Maria angekuwa katika hali yake nzuri ya umaliziaji basi mambo yangekuwa 3-0 na ingekuwa ngumu sana kwa wao hata kupata bao moja.

Fellaini kwa ukweli na De Gea hivi karibuni wamekuwa wakionyesha mchezo wa hali ya juu mno. Kwangu Fellaini sasa kwa mara ya kwanza mechi zilizopita kama tatu hivi amerejesha kiwango chake ambacho alikuwa nacho Everton kabla ya kujiunga na Man United chini ya David Moyes.

Naweza kusema kuwa alikuwa chini mno nyakati za Moyes kwani yeye ndiye aliyekuwa kocha wake Everton kwa hivyo alikuwa kama ngao ya kumtetea kwa uwezo wake hafifu. Lakini kwa sasa yupo fiti mno na wengi wenu mtakubaliana na hilo.

Arsenal ilipoteza mechi hiyo kwa sababu hawakuzitumia vilivyo nafasi walizozipata. Hata hivyo sifahamu kwa sababu gani kwa muda mrefu Wenger amekuwa hamchezeshi straika Giroud.

Ni mshambuliaji hodari mno ambaye namuogopa sana akiwa ndani ama hatua chache nje ya miguu 18. Ukiangalia bao alilofunga, hata kama mimi ni shabiki wa Man Utd hilo bao lilikuwa safi mno. Ni vizuri Wenger akamuamini Giroud na kumpa wakati mrefu wa kucheza kwani kwangu ni mshambuliaji mzuri na wakati wowote anaweza kufanya mambo.

Alexis Sanchez, Wilshere, Danny Welbeck kwa ukweli walipoteza nafasi za wazi, nafasi ambazo kwa mechi kama hiyo haifai kupoteza.

Mashuti ambayo walipiga langoni mwa Man United yalikuwa mengi mno. Hata hivyo, mechi dhidi ya Arsenal na Man Utd inakuwa ya kukamiana sana ukianzia kwa wachezaji wenyewe hadi mashabiki. Nakumbuka mashabiki wa Man United mjini Eldoret walikuja dukani kwangu kwa fujo wakiwa wamebeba mabango ya Man United wakitafuta jezi ya timu yao, wakiwakemea mashabiki wa Arsenal.

Jioni wakajikusanya ndani ya klabu ya 411, kwa kweli ungedhani wapo ndani ya Uwanja wa Emirates wakati Man Utd ilitangulia kupiga bao lao la kwanza. Man United inaongoza kwa idadi ya mashabiki dunia nzima ikifuatiwa kwa karibu mno na Arsenal.

Kumbuka Chelsea na Man City walikuwa wakicheza siku hiyo hiyo kwenye viwanja tofauti lakini hakuna aliyefuatilia hizo mechi kwa karibu. Hata hivyo uhasama bado upo. Nakumbuka shabiki mmoja aliikejeli Arsenal kwamba tangu Cristiano Ronaldo aondoke England, Arsenal haijawai kuifunga Man United.

Wakati nazungumzia yaliyotokea Emirates itakumbukwa Chelsea wako kileleni mwa ligi hiyo, hawajapoteza mechi yoyote tangu Ligi Kuu England ianze msimu huu. Jumamosi waliifunga West Brom Albion 2-0 Uwanjani Stamford Bridge, Diego Costa na Eden Hazard wakifunga. Vijana wa Jose Mourinho wakati huu wameamua kutwaa ubingwa mapema. Wameweka tofauti ya pointi saba wakifuatiwa na timu ya Victor Wanyama, Southampton ambayo jana Jumatatu usiku ilicheza na Aston Villa.

Chelsea wameonyesha kila dalili ya kunyakua taji hilo msimu huu. Wameanza ligi vizuri sana. Hata hivyo Ligi Kuu huwa ni Mbio za Nyika. Kwani mwenye pumzi hadi mwisho huwa mshindi. Kutangulia kwenda klabuni si kulewa, au siyo?

Katika Uwanja wa Etihad, Winfred Bonny aliwanyamazisha mashabiki wa Man City ndani ya dakika sita za kwanza alipopiga bao safi sana. Raia huyo wa Ivory Coast amepiga mabao matano ndani ya mechi sita alizozicheza zikimpa nafasi nzuri mno ya kuitwa katika kikosi cha Ivory Coast kitakachoenda kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.

Hata hivyo bao lake halikuisaidia Swansea kushinda kwani Man City walisawazisha dakika ya 19 kupitia kwa kiungo Stevan Jovetic kabla kiungo wa Ivory Coast, Yaya Toure kupiga bao la ushindi dakika ya 62. Man City usiku wa leo Jumanne wanakutana na Bayern Munich katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Man City kwa sasa ipo katika nafasi ya tatu ikifuatiwa kwa karibu na Man United walio katika nafasi ya nne.

Nikiingia mitamboni Liverpool ilikuwa inacheza na Crystal Palace na ikaangukia pua kwa kufungwa mabao 3-1. Klabu ambayo msimu uliopita iliinyima Liverpool taji katika mechi ambayo Liverpool waliongoza kwa mabao 3-0 lakini ndani ya dakika kumi za mwisho mechi iliishia kuwa 3-3. Matokeo ambayo yanaiumiza Liverpool hadi leo.

Kwa sasa Chelsea ipo kileleni, ikifuatiwa na Southampton nafasi ya pili. Tatu wakiwa Man City, nafasi ya nne ikichukuliwa na Man Utd. Arsenal iko nafasi ya nane. Mechi zilizochezwa ni 12 kwa kila klabu.

Tukutane wiki ijayo.