Hizi dalili zilizojitokeza Yanga siyo nzuri

Muktasari:

Aidha wakati tukienda mitamboni kulikuwa na taarifa kwamba mabeki Vincent Bossou na Oscar Joshua nao wametemwa dakika za mwishoni kwa sababu kama hizo za kuendesha mgomo wa chini chini kushinikizwa kulipwa fedha zao.

MSAFARA wa timu ya Yanga,  umeondoka jioni ya jana kwenda mjini Algiers, Algeria kwa ajili ya pambano lao la marudiano la michuano la Kombe la Shirikisho Afrika inayosimamiwa na kuendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Yanga imewafuata wapinzani na wenyeji wao, MC Alger katika mechi ya kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, huku wakiwa na hazina ya ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi yao ya mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania wanahitaji sare ya aina yoyote ama ushindi katika mchezo huo utakaopigwa usiku kwenye Uwanja wa July 5, 1962 mjini Algiers, ili isonge mbele na kucheza makundi kwa mara ya pili mfululizo baada ya awali kufanya hivyo katika michuano ya msimu uliopita.

Watanzania wana matumaini makubwa na Yanga katika mechi hiyo ya marudiano ikizingatiwa kuwa rekodi zao za hivi karibuni kwa mechi za ugenini hasa katika mechi za Kiarabu hujituma na hupata matokeo ya kufungwa idadi ndogo.

Kwa maana hata kipigo cha mabao 2-1 ama 3-2 kinaweza kuivusha Yanga kucheza hatua hiyo ya makundi, itakayoshirikisha timu 16 Bora kwa nia ya kusaka timu nane za kucheza robo fainali na kutoa fursa ya kuongelea mamilioni ya fedha za Caf.

Hata hivyo, kuna dalili ambazo zimeashiria mwisho mbaya wa Yanga katika mechi hiyo, kama viongozi na wachezaji hawatalimaliza kabla ya kesho usiku kushuka uwanjani kupepetana na wapinzani wao hao.

Yanga imeondoka ikiwa imewaacha baadhi ya nyota wake, akiwamo Obrey Chirwa ambaye imeelezwa kuwa alikuwa kinara wa kugomea safari hiyo, kisa kutaka kulipwa mishahara anayoidai klabu.

Aidha wakati tukienda mitamboni kulikuwa na taarifa kwamba mabeki Vincent Bossou na Oscar Joshua nao wametemwa dakika za mwishoni kwa sababu kama hizo za kuendesha mgomo wa chini chini kushinikizwa kulipwa fedha zao.

Kwa hakika hizo siyo dalili nzuri kwa timu inayoendelea kukabiliana na pambano gumu kama hilo dhidi ya Waalgeria ambao rekodi zinaonyesha kwa zaidi ya miaka 40 ya ushiriki wao kuiwakilisha Tanzania haijawahi kuitoa klabu yoyote ya Kiarabu.

Mwanaspoti haina tatizo la msimamo wa wachezaji, kwa sababu ni haki yao, ila jambo hilo limekuja wakati usio mwafaka kwani, Yanga kwa sasa inahitaji utulivu wa akili na mwili kabla ya kuvaana na MC Alger kesho mjini Algiers. Kilichoanza kuonekana mapema jijini Dar es Salaam kabla ya safari ya Algeria, ina maana kuwa Yanga inajiweka katika nafasi kubwa ya kuvurunda pambano hilo kwa sababu kwanza kikosi kimezidi kudhoofika kwa kuwakosa kina Chirwa.

Hakuna asiyejua kuwa, Yanga ya sasa inapata wakati mgumu katika mechi zao kwa kukosekana nyota wao walio majeruhi, lakini wakati ikienda kwenye pambano kali zaidi, inawapoteza wengine katika mazingira yasiyo sahihi.

Hata hivyo, kwa namna timu ilivyoondoka, huku wachezaji wakionekana kuwa na kinyongo na kuachwa kwa wenzao kadhaa ni dalili isiyotoa matumaini kwa Yanga kufanya vyema katika pambano hilo, ingawa Mwanaspoti linaiombea heri.

Kwa mechi kubwa na muhimu kama hii Yanga ilikuwa inahitaji utulivu wa hali ya juu hasa kwa wachezaji wao, ili washuke uwanja wa ugenini akilini mwao wakiwaza kitu kimoja tu; kuivusha timu hatua ya makundi na siyo kuwaza fedha.

Ila kwa namna wawakilishi hao walivyoondoka, lolote litakalotokea Algeria hasa kwa Yanga kutolewa kwenye michuano hiyo, hakutakuwa na sababu ya kusakwa mchawi kwa sababu tatizo limezalishwa na wahusika wenyewe hata kabla ya kwenda ugenini.

Kitu muhimu ni kuwaombea Yanga na wachezaji kwa jumla kusahau yote waliyoyaacha nyumbani na kuelekeza nguvu na akili zao katika pambano hilo ili kuendelea kuipeperusha Bendera ya Tanzania katika michuano hiyo ya kimataifa.