Hivi ndivyo mechi Ligi Kuu zinavyopaswa ziwe

Monday February 27 2017

 

By MWANASPOTI

HATIMAYE zile tambo na kejeli za mashabiki wa soka wa klabu za Simba na Yanga zimemalizwa kwa amani na utulivu juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Watani wa jadi hao walipambana kwenye mchezo wa marudiano katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kushuhudiwa Yanga ikilala mbele ya Simba kwa mabao 2-1.

Bao la mapema la penalti la Simon Msuva wa Yanga na mengine ya kipindi cha pili ya Laudit Mavugo na Shiza Kichuya wa Simba yalimaliza ubishi uliokuwapo mtaani na vijiweni kabla ya pambano lao hilo la 98 tangu ligi ilipoanzishwa mwaka 1965.

Kwa waliolishuhudia pambano hilo uwanjani na hata waliolifuatilia kupitia luninga na hata kwenye akaunti ya Facebook ya Mwanaspoti, walipata burudani ya aina yake. Watani waliamua kucheza soka na ndivyo mechi za Ligi Kuu zinavyotakiwa kuchezwa.

Namna wachezaji walivyojituma uwanjani na kuwajibika katika kila dakika ya mchezo huo, ilionyesha kuwa kama klabu zetu zikiamua na kucheza soka, basi ligi yetu inaweza kufika mbali na mahali ilipo kwa sasa.

Mwanaspoti linayasema haya kutokana na ukweli kuwa kwa siku za karibuni, mechi za Ligi Kuu Bara mbali na pambano la watani, timu hucheza kwa mtindo wa bora liende na huwezi kutofautisha na mechi nyingine za ligi za madaraja ya chini na hata mchangani.

Lakini katika mechi ya juzi pale Taifa, kuanzia kwa mashabiki waliofurika uwanjani, wachezaji na hata waamuzi waliopangwa kulichezesha pambano hilo la watani, kwa asilimia zote walitekeleza majukumu yao.

Hata kama Yanga imepoteza mchezo huo kwa watani zao, bado ilionyesha uhai tangu dakika ya kwanza mpaka kipyenga cha mwisho, hata kama Simba ilianza kwa kushtukizwa kwa penalti ya Msuva na kisha kumpoteza mchezaji mmoja, lakini ilionekana kujituma na ilistahili ushindi ilioupata.

Katika hili tunapenda kuwapongeza wachezaji wa pande zote kwa kile walichokifanya. Soka lao la hali ya juu lilionekana na ndicho mashabiki wanachokitaka siku zote.

Waamuzi Mathew Akrama na wasaidizi wake; Mohammed Mkono na Hassan Zani na yule wa akiba, Elly Sasii wanastahili heko kwa kazi kubwa waliyofanya uwanjani. Kama waamuzi wote wa Ligi Kuu wangekuwa wakitenda walivyotenda kina Akrama hata zile kelele dhidi yao zingepungua.

Nani angekuwa na muda wa kuwatupia lawama wakati wanachezesha kwa kuzingatia Sheria 17 na busara ili kuona mechi za Ligi Kuu zinachezwa na kumalizwa kwa amani na salama uwanjani?

Hatuna maana hakuna waamuzi waliowahi kuchezesha mechi kwa kiwango kizuri kama kilichofanywa na waamuzi wa juzi, lakini ukweli ni kwamba waamuzi wengi wamekuwa wakibebeshwa lawama kwa kuvuruga mechi uwanjani.

Mwanaspoti linaamini mechi zote zingekuwa zikichezeshwa hivi na kuchezwa kama walivyocheza Simba na Yanga juzi, heshima ya Ligi Kuu Bara ingekuwa maradufu, ila tunaamini kuwa kila kitu kinawezekana iwapo wadau wataamua.

Lakini tunaomba hayo yasiishie kwenye mchezo huo tu.