MTU WA PWANI: Hivi Ibrahim Ajib anatambua thamani ya jezi yake?

Friday March 17 2017Abel Charles_charlesabel24@gmail.com

Abel Charles_charlesabel24@gmail.com 

By Charles Abel

IBRAHIM Ajib anaujua mpira na anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wachache wasiowachosha watazamaji iwe uwanjani au kwenye runinga, yaani kila unapomwona anacheza, unatamani uendelee kumtazama, ni mtamu kwa soka lake.

Ndani ya kikosi cha Simba hivi sasa, Ajib ni staa kweli kweli na amewateka akili mashabiki wa klabu hiyo. Kwa Ajib, yaani huwaambii kitu.

Kwa Ajib, kila akili yake inapoamua kucheza mpira, huwa hashikiki uwanjani. Anafunga mabao matamu, anapiga chenga za maudhi na anaweza kupiga pasi ya bao baada kumpiga kanzu beki au kipa wa timu pinzani.

Ni mmoja kati ya matunda bora ambayo Simba imeyazalisha kupitia timu yake ya vijana akijumuishwa na wenzake kama Said Ndemla, Jonas Mkude, Hassan Isihaka, Abdallah Seseme, Waziri Junior, Marcel Boniventure, Edward Christopher, Hamad Tajiri, Miraji Adam, Frank Sekule, Hassan Hatib na Miraji Athuman ambao wanatamba kwenye Ligi Kuu Bara hivi sasa.

Miongoni mwa matukio yaliyonisisimua wiki hii kumhusu mshambuliaji huyo, ni lile la kusambaa kwa picha ya mtoto ambaye ni mkazi wa Dodoma, akiwa anafuatilia mechi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri huku akiwa amevaa fulana ambayo mgongoni ameiandika namba na jina la Ajib. Ameandika kwa peni.

Hii inadhihirisha ni namna gani Ajib amekuwa kipenzi cha wapenda soka nchini kiasi cha kuteka hisia hadi za watoto ambao wengi katika kizazi cha sasa hupenda kufananishwa au kuitwa majina ya wanasoka wa Ulaya hasa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.

Hata hivyo, huu unaweza kuwa msimu wa mwisho kwa mshambuliaji huyo kuitumikia Simba baada ya kuweka wazi nia yake ya kutosaini mkataba mpya klabuni hapo hivyo atakuwa huru kujiunga na timu yoyote ambayo ataafikiana nayo.

Anaweza kujiunga na upande wa pili, Yanga au Azam, Mtibwa Sugar ama kwenda nje ya nchi. Ameshaweka wazi kuwa hataitumikia Simba msimu ujao labda aamue kubadili mawazo.

Kama ataachana na Simba kama alivyodai, haiwezi kuwa habari nzuri kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo ambao wengi wana mahaba yaliyopitiliza kwa mshambuliaji huyo kama ilivyodhihirishwa na yule mtoto wa Dodoma.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya Ajib ataondoka Simba akiwa na kosa kubwa la kushindwa kutumia mahaba ya mashabiki wa timu hiyo kujinufaisha kiuchumi na kujitengenezea maisha bora baada ya kuachana na soka.

Ajib angeweza kuingia ubia na kampuni yoyote au watu wakamtengenezea bidhaa mbalimbali zenye jina lake kama kofia, jezi, khanga au skafu kisha zikauzwa na zikamwingizia fedha nyingi ambazo zingemfanya asitegemee mshahara tu au posho za timu.

Angetumia thamani ya jina lake kupata mikataba na makampuni mbalimbali kwa lengo la kutangaza bidhaa au huduma zao kupitia yeye, huku akipata mamilioni ya fedha.

Inawezekana huko anakokwenda, atalipwa mshahara na posho kubwa kuliko anayoipata Simba, lakini hilo halimfanyi akwepe lawama kwa kushindwa kuwatumia mashabiki wa Simba wanaoliimba jina lake kila wakati ili apige pesa.

Kwa mfano angetengeneza jezi 7,000 za wakubwa na watoto zenye jina au namba yake kisha akaziuza zote kwa bei rahisi tu ya Sh10,000, Ajibu angefanikiwa kupata Sh 70 milioni ambazo ni nadra kwa yeye kuzipata kwa kusajiliwa na timu ya hapa ndani.

Hapo sijazungumzia fedha ambazo angezipata kwa kuuza bidhaa nyingine zaidi ya hizo au zile ambazo angechuma kwa kuingia mikataba ya haki za matangazo na makampuni.

Wakati mwingine wanasoka wetu wanazichezea tu fursa kama hizo ambazo zipo usoni mwao kisha wakaziacha zipite hivi hivi pasipo kuwaletea manufaa yoyote kimaisha.

Tumezoea kuzilaumu timu zetu kwa kushindwa kutumia vyema faida ya rasilimali kwa maana ya mashabiki katika kujiendeleza kiuchumi,  lakini ni vyema sasa tukageukia na upande wa wachezaji ili nao waanze kutumia ya mashabiki katika kujitengenezea maisha bora.

Ajib anatakiwa atambue kuwa kuna kundi kubwa la mashabiki linalokoshwa na kile anachokifanya uwanjani ambao ni mtaji kwake iwapo ataamua kuwekeza kupitia hao.

Kama klabu zimeshindwa kuwatumia mashabiki ili kunufaika kiuchumi ni vyema sasa wachezaji wetu wakazitumia vyema fursa walizonazo ili kuchuma fedha.

Hata hivyo, bado wachezaji hawajafunguka akili ya kutumia thamani yao mbele ya jamii, na wanaendelea kuishi kwa kubahatisha wakitegemea kiasi kidogo wanachokipata kwenye mshahara na posho.

Hakuna maana yoyote kutembea kifua mbele kwa sababu tu wewe ni kipenzi cha mashabiki, huku ukishindwa kuwatumia kama mtaji wa kukunufaisha katika maisha yako.

Kuna fungu kubwa la fedha ambalo linawazunguka wanasoka wetu, lakini wanashindwa kujiongeza na kutengeneza njia rahisi zitakazowafanya wapate fedha hizo.

Kwa Ajibu kama ataondoka Simba, atakuwa ameshachelewa kuvuna fedha kutokana na thamani ya jina lake kwa mashabiki wa timu hiyo, lakini anaweza kutumika kama darasa kwa wengine katika siku za usoni.