Hili la Banda tunahitaji Gwajima aanze kuwasema watu katika soka

Muktasari:

Banda kwao ni muhimu na Simba ipo katika mapambano ya kurejesha heshima yao iliyopotea tangu mwaka 2012 ilipochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya mwisho. Unahitaji kikosi kamili kwa muda wote. Mechi dhidi ya Kagera ilikuwa ngumu kwa Simba ingawa uwanjani walikuwa na wachezaji 11. Vipi kama mwamuzi angemuona Banda?

ABDI Banda, beki wa kati wa Simba anaonekana katika picha za marudio akimpiga kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla, katika eneo ambalo hakukuwa na mpira. Hata mashabiki na viongozi wa Simba wamekerwa na tukio lenyewe.

Banda kwao ni muhimu na Simba ipo katika mapambano ya kurejesha heshima yao iliyopotea tangu mwaka 2012 ilipochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya mwisho. Unahitaji kikosi kamili kwa muda wote. Mechi dhidi ya Kagera ilikuwa ngumu kwa Simba ingawa uwanjani walikuwa na wachezaji 11. Vipi kama mwamuzi angemuona Banda?

Mtu pekee ambaye mara chache anaweza kusimama hadharani na kuponda ujinga wa Banda ni Zacharia Hans Poppe. Huyu ndiye mwanaume anayeweza kusimama hadharani na kusema anachojisikia hata kama wakati mwingine anakosea.

Unaachana na ujinga huo. Baada ya Banda kusalimika, ilipaswa kamati inayohusika kutoa maamuzi mapema kabla ya Simba kucheza mechi inayofuata. Juzi wametangaza kumsimamisha Banda na jana Simba ilikuwa inacheza pale Mwanza.

Inashangaza kidogo. Ingawa wengi tuliona kwamba Banda alikuwa amefanya kosa, wao bado hawajajiridhisha kwamba Banda amefanya kosa. Vipi wakigundua kwa mitazamo yao kwamba Banda alikuwa hajafanya kosa? Hawaoni kama watakuwa hawajaitendea haki Simba na mchezaji mwenyewe?

Wataifidia vipi Simba kwa kumkosa mchezaji wao muhimu siku ya jana? Au hii ina maana kwamba tayari wameshamhukumu Banda? Inashangaza kidogo kuona watu walioushikilia mpira hawajui taratibu.

Ukiuliza sababu za wao kutokutana haraka na kutoa uamuzi utaambiwa kwamba watu wanaounda kamati hiyo walikuwa na udhuru. Kama wako bize kiasi hicho, kwa nini wasitafute kazi nyingine za kufanya na kutuachia mpira wetu?

Katika nchi zilizoendelea maamuzi haya yanachukuliwa haraka kabla ya mechi inayofuata. Tuachane na ujinga wa kucheleweshwa kwa ripoti ya mwamuzi. Hii inaweza kumnyima haki Banda, au timu yake, au walalamikaji.

Kwa gharama hizi hizi za ujinga wao, Banda alistahili kucheza mechi ya jana, halafu akaanza kutumikia adhabu yake mara baada ya kufungiwa rasmi. Hata kama angefungiwa mechi nyingi basi anaweza kutumikia msimu ujao au siku yoyote atakayogusa soka la nchi hii ngazi ya ligi.

Hii ndio hasara ya mechi kuonyeshwa moja kwa moja katika televisheni. Wakubwa wanaumbuka halafu wanashikwa na kigugumizi. Tuliyataka haya halafu tunajaribu kujificha mithili ya mbuni anayezamisha kichwa chake mchangani.

Kichekesho kingine katika suala hili kinakuja nje ya tukio lenyewe. Juzi nimesoma mahala Banda atatimkia Afrika Kusini kujaribu kucheza soka la kulipwa. Anachezaje soka la kulipwa kwa tabia zake hizi? Hii si mara ya kwanza kwa Banda kufanya alichofanya.

Mara nyingi amekuwa akitembeza ubabe usio na maana. Banda ni kijana wangu. Nikiwa msemaji wa Coastal Union yeye alikuwa mchezaji wa timu ya vijana. Nazielewa tabia zake. Mara nyingi tabia zake zinafichwa na kiwango chake. Katika ubora wake, Banda ni mmoja kati ya wachezaji watakaokukosha uwanjani.

Anapoteza sifa ya kuwa mchezaji wa kulipwa. Wachezaji wa kulipwa wanaojielewa huwa wanafanya ubabe wakiwa na mpira. Unapofanya ujinga wakati hauna mpira klabu inakupiga faini na inaweza kukufungia. Huu ndio ukweli halisi.

Wachezaji wa kulipwa wanazuia hasira zao. Wanaishia kushikanashikana tu. kadi nyekundu moja ya kipuuzi huwa inaigharimu klabu mamilioni ya pesa. Klabu inapopotea katika mbio za ubingwa basi inapoteza pesa nyingi. Inapoteza pesa za ubingwa. Inapoteza pesa za mikataba kwa kushindwa kufanya vema, inapoteza pesa za kushiriki katika michuano mikubwa.

Simba na Yanga zinawavumilia wachezaji wa aina hii. Haziwakanyi. Haziwatozi faini, haziwapigi benchi. Zinawatetea hadharani bila ya aibu na matokeo yake wachezaji wanaendelea kukifanya wanachokifanya bila ya hofu kubwa. Waamuzi ni wao, na hata mabosi wa TFF nao ni mashabiki wa timu hizi.

Ni katika tabia kama hizi ndani ya mpira wetu, wachezaji wetu huwa wanaona maisha ni magumu ugenini pindi wanapokwenda kujaribu soka la kulipwa. Unakuwa sio staa tena, tofauti na inavyokuwa katika Uwanja wa Taifa na hauruhusiwi kufanya unachojisikia.

Kwa sasa soka letu linamhitaji Mchungaji Gwajima aanze kuwasema watu. Inabidi tuanze kumpeleka kesi zetu za soka ili aziseme hadharani. Mara nyingi kesi zetu za soka ni kichefuchefu zaidi kuliko mambo ambayo yanamkera kwa sasa.