Hii ndio bahati tuliyonayo Watanzania, kujiongeza kidogo tu

Muktasari:

Kufanya kazi kwa mazoea kunaweza kumfanya mtu mmoja aonekane mchapakazi kwa sababu amejiongeza kidogo tu.

BAHATI ambayo tunayo Watanzania ni kwamba kwa kujiongeza kidogo tu, unaweza kuonekana upo tofauti na wengine kwa ubora.

Kufanya kazi kwa mazoea kunaweza kumfanya mtu mmoja aonekane mchapakazi kwa sababu amejiongeza kidogo tu.

Maeneo ya kazi, watu wengi wanafanya kazi kwa mazoea, lakini iwapo itatokea mtu mmoja akajiongeza kidogo tu, utashangaa anaonekana shujaa mbele ya wengine.

Kama ni mkulima unatakiwa kujiongeza kidogo tu ili uwe mkulima bora na upate mavuno mengi kuliko wengine. Tunapaswa kuwa hivyo.

Kama anafanya kazi jitahidi kujiongeza kidogo tu, utajikuta ukipata tuzo ya mfanyakazi bora wa kampuni au shirika unalofanyia kazi.

Ili biashara yako ipate wateja wengi jitahidi kujiongeza kidogo kwa kuwapa huduma bora watu ili wapende kuja mara kwa mara na hilo litafanya biashara yako iwe nzuri na iwe na faida zaidi.

Tofauti na maeneo mengine ya dunia ambayo watu wamejiongeza sana, Watanzania tuna bahati kubwa kwani bado kuna nafasi ya kujiongeza.

Kutokana na mfumo wa ujamaa ambao umetulea kwa miaka yote, wengi wameshindwa kuamka na bado wanadhani wanaishi katika mfumo huo wakati dunia yenyewe imebadilika.

Lakini walioishi katika mfumo wa kibepari, wanajua maana ya kujiongeza kiasi kwamba wamechangamkia kila fursa inayopita mbele yao, huku wakijua jinsi ya kukabiliana na maisha.

Iwapo tutajiongeza kidogo tu, Tanzania tutakuwa na ligi bora kuliko nyingine yoyote Afrika Mashariki na Kati.

Iwapo tutajiongeza kidogo tu, tutakuwa na timu ya taifa bora na imara kuliko timu yoyote katika Bara la Afrika.

Tanzania kuna vipaji vingi vya wachezaji, inawezekana tukawa na vipaji vingi kuliko sehemu nyingine yoyote Afrika, lakini wachezaji wetu wameshindwa kujiongeza.

Tanzania licha ya kuwa hakuna akademi za soka, bado kuna wachezaji wametokea mchangani wanatamba katika Ligi Kuu Bara, hili si jambo dogo hata kidogo.

Ukiona Ligi Kuu inaundwa na wachezaji ambao hawajapita katika mfumo sahihi wa makuzi ya soka, ujue kuwa nchi ina wachezaji wengi wenye vipaji binafsi.

Baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Congo Brazaville, Vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys’ wanahitaji kujiongeza kidogo tu ili kupata angalau sare ugenini.

Wakitoka sare maana yake watakuwa wamefuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 ambazo zitafanyika Madagascar, mwakani.

Na nimekuwa ninaamini kuwa kikosi hiki cha Serengeti Boys, nakiona kikiunda timu bora ya Taifa Stars miaka miwili ijayo na haitakuwa ajabu Tanzania ikifuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019.

Hata kama vijana wa Serengeti watatolewa na Congo, wasikatishwe tamaa ila wapewe matunzo mazuri ikiwa ni pamoja na kupelekwa katika klabu mbalimbali zinazoweza kuwalea vizuri ili waje kuunda timu nzuri ya taifa.

Kwa kikosi hiki cha Serengeti, tunaweza kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika ndani ya miaka mitano ijayo. Hutakiwi kushangaa ni mipango tu.

Hayo yote hayawezi kuja kwa kufirika tu au kwa kubweteka, bali yatakuja kwa kujiongeza na kuzingatia tunachopaswa kukifanya kwa nguvu zetu ili tuupate ubora unaokusudiwa.

Sio kingine ni kujiongeza kidogo na kuchana kuishi au kufanya mambo yetu kwa mazoea.