Ghafla tu, Wanasiasa wamevamia Serengeti Boys kutafuta sifa

Muktasari:

Timu inakaribia kufuzu kwenda Madagascar katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika U17. Litakuwa tukio la kusisimua kama tukifanikiwa. Magazeti yatapamba kurasa za mbele.

WANASIASA huwa wanaangalia wapi pa kutokea. Wana akili fupi kuliko unavyodhani. Wanaangalia jinsi upepo unavyokwenda. Na sasa wamevamia katika kambi ya timu ya taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.

Timu inakaribia kufuzu kwenda Madagascar katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika U17. Litakuwa tukio la kusisimua kama tukifanikiwa. Magazeti yatapamba kurasa za mbele. Vyombo vya Habari vitakuwa karibu zaidi. Wanasiasa wetu huwa hawataki kuipoteza nafasi kama hii.

Wanasiasa walikuwa kimya wakati Serengeti wakiitoa Shelisheli. Mechi zote mbili zilichezwa kwa utulivu mkubwa. Moja ilichezwa katika Uwanja wa Chamazi nyingine ikafanyika Shelisheli. Hakuna mwanasiasa aliyejitokeza kutoa ahadi. Hakuna Mwanasiasa aliyetembelea kambini.

Hawa hawa ndugu zetu wetu wanasiasa walikuwa kimya wakati Serengeti wakiitoa Afrika Kusini katika mechi ngumu mbili. Moja ilichezwa hapa, nyingine ikachezwa katika ardhi ya Mzee Mandela pale Bondeni. Hakuna Mwanasiasa aliyetembelea kambi wala kutoa ahadi ya pesa.

Mtu aliyeniaga kwamba anaenda kushangilia mechi hiyo dhidi ya Afrika Kusini ugenini ni staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mtemi Ramadhani. Huyu huwa ana tabia ya kusafiri kwenda kuangalia mechi za kimataifa kwa mapenzi yake binafsi na soka.

Lakini sasa tulikuwa tumekabiliwa na mechi dhidi ya Congo Brazzaville ili tuweze kufuzu. Wanasiasa walipoona kama masihara Serengeti wanakaribia kufuzu michuano hiyo na kuweka historia huku wakiwa wameibakiza timu moja tu mbele yao basi wamedandia treni kwa mbele.

Kabla ya mechi wamechangishana pesa na kuweka ahadi nyingi ambazo zimewaweka watoto wetu katika presha. Wenyewe huwa wanasema kutoa motisha kwa vijana ili washinde. Usiaamini sana wanachosema. Kitu pekee ambacho mwanasiasa anasema kweli ni salamu tu na pengine jina lake. Mengine uongo mtupu!

Lengo hasa ni kutafuta kujisifu kwamba walichangia kwa kiasi kikubwa kwa Serengeti kufuzu katika fainali hizo za mwakani zitakazochezwa nchini Madagascar.

Hawajui kwamba kwa kiasi kikubwa wameanza kutibua vichwa vya vijana wetu ambao waliwatoa Shelisheli na Afrika Kusini bila ya ahadi zozote za pesa.

Kocha wa timu hiyo Bakari Shime ameshalalamikia hali hiyo. Kijana mdogo unapomuahidi akifunga bao utampa shilingi milioni moja basi unamtoa mchezoni. Mkononi hajawahi kushika kiasi hicho cha pesa, kwanini unamshtua ghafla na usimpe baada ya matokeo?

Kama hilo halitoshi, Kocha Kim Poulsen alikuwa na ratiba zake nzuri tu za kambi yake, lakini wanasiasa wanapojitokeza siku chache kabla ya mechi basi tegemea kwamba watoto wataamshwa usiku kwa ajili ya kwenda kusikiliza risala ndefu katika ukumbi wa hoteli. Risala hizo zinawachosha zaidi kwa sababu mechi mbili za Shelisheli na Afrika Kusini walicheza soka kwa utulivu tu.

Wanasiasa kamwe hautawaona katika michakato ya mwanzo ya ushindi. Ushindi haupatikani kwa kwenda mechi ya mwisho zinazokaribia kutufikisha mahala. Ushindi unapatikana kwa kutengeneza sera nzuri na kubuni mikakati ya kupata vipaji vilivyojificha.

Kwa mfano, nilimsikia kiongozi wa Simba, Zakaria Hans Poppe akiwaponda wanasiasa hao kwa jinsi walivyovamia kambi ya Serengeti na michango yao feki badala ya walau kuwasaidia viongozi wa Simba ambao nyasi zao bandia zimekwama katika Bandari ya Dar es Salaam. Hawa ndio wanasiasa.

Hata kwa sasa kwa wale walio wabunge au wenye nia ya kugombea ubunge wapo kimya na ile michuano yao ya wakati wa kuelekea katika uchaguzi. Michuano ya kina ‘Kumwembe Cup’. Michuano hii inajitokeza miezi 24 kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuwadanganya wapiga kura. Hawa ndio wanasiasa. Najua kwa sasa, baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Congo Brazzaville wanasiasa wanasubiri kwa hamu sana Serengeti ifuzu kule ugenini, ili wawahi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwapokea vijana. Kuna wengine watasafiri na timu kabisa wakiwa na majaketi yao ya bendera za taifa. Wakiwa huko kazi yao ni kusumbua watoto watu. Tuwakane Wanasiasa wa aina hii katika soka. Hawalisaidii soka letu. Ni bora waendelee na siasa zao popote walipo kuliko kuja katika mechi za mwisho mwisho kusaka sifa.