Bila kuuheshimu mpira hauwezi kuwaheshimu

Muktasari:

  • Lakini cha kushangaza tathmini inaonyesha kwamba Ligi Tanzania ndiyo ambayo inapoteza wachezaji kwa muda mfupi zaidi.

LIGI ya Tanzania ndiyo inayosifika zaidi kwa sasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki. Ni Ligi ambayo imetokea kuwa na fedha nyingi ambazo zinatolewa na wadau, mashabiki na wadhamini kwenye klabu mbalimbali.

Mishahara mikubwa ya wachezaji hususani kwenye klabu za Simba, Yanga na Azam imevutia wachezaji wazawa na wageni. Ni mishahara ambayo ni ngumu kuipata kwenye klabu nyingine, ingawa hata katika klabu zingine za chini uwepo wa Azam Tv na mdhamini mkuu vodacom kumechangia kuimarisha uchumi wao.

Lakini cha kushangaza tathmini inaonyesha kwamba Ligi Tanzania ndiyo ambayo inapoteza wachezaji kwa muda mfupi zaidi. Mastaa wengi hususani wazawa wamekuwa wakicheza muda mfupi sana kabla ya kujilazimisha au kulazimishwa kustaafu kutokana na uhalisia wa mazingira.

Wachezaji hao huanza kwa kasi lakini ndani ya muda mfupi wamekuwa wakitoweka kwenye ramani ya soka. Wapo wachezaji wengi waliokumbwa na hali hiyo ndani ya miaka ya hivikaribuni ambao ni wengi kuliko kwenye nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda hata Burundi. Hali hiyo imekuwa ikiathiri hata ufanisi wa timu za Taifa kwavile wachezaji wengi wamekuwa wakipotea mapema kutokana na kuchuja viwango. Matunzo binafsi pamoja na nidhamu ya mazoezi na vyakula ni baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa vikichangia hayo kwani wachezaji wengi hawajakuzwa kwenye misingi mizuri tangu enzi za utoto kama ilivyo katika nchi za wenzetu. Si kitu cha ajabu sana kukuta mchezaji aliyetoka kwenye mechi ngumu akila chakula hafifu na wakati mwingine kujiingiza kwenye vitendo vya ulevi uliokithiri jambo ambalo ni athari kubwa kwa miili ya wachezaji.

Ukifanya tathmini ya haraka utagundua kwamba Wachezaji waliocheza Ligi ya Bara kwa kipindi kirefu hawafiki hata kumi. Yupo Shabaan Nditi wa Mtibwa, Lulanga Mapunda na Fred Mbuna wa Majimaji na Juma Kaseja wa Mbeya City.

Lakini Nditi ndiye aliyecheza kwa miaka zaidi ya kumi mfululizo kwani hao wengi wamekuwa wakiacha na kurudi wanavyojisikia. Ukiangalia katika nchi jirani hata DR Congo hususani kwenye klabu kama TP Mazembe, AS Vital na nyinginezo ambazo zinafanya vizuri utagundua wachezaji wengi wanacheza misimu mingi na hawachuji kuanzia kwenye klabu mpaka timu za Taifa. Wanajitunza binafsi kwenye mambo mengi lakini hata klabu husika imekuwa na wataalam mbalimbali ambao wamekuwa wakisaidia kwenye ushauri na kuhakikisha kila mchezaji anakuwa katika hali inayotakiwa.

Kuna masharti ya vyakula ambayo ni lazima mchezaji ayafuate ili akue katika afya bora na aweze kumudu aina fulani ya mazoezi yanayotolewa na kocha kutokana na staili zake za uchezaji na utamaduni wa klabu husika.  Uchunguzi mdogo kwenye Ligi yetu unaonyesha kwamba wachezaji wengi hawana nidhamu ya ndani na nje ya uwanja jambo ambalo linawafanya wapotee muda mfupi wanapopata utajiri wa ghafla na sifa za mashabiki. Wachezaji wengi wanakosa viongozi na mameneja wa kuwaongoza kwenye katika mstari unaostahili matokeo yake ndiyo hayo kwamba wamekuwa wakiishia kucheza soka katika muda mfupi tofauti na mategemeo ya wengi ambao huzingatia umri  wa wachezaji hao. 

Bila kuuheshimu mpira ni ngumu kufanikiwa kwavile soka lina miiko yake, wachezaji wanapaswa kujituma na kujilinda kiafya na kiakili. Si jambo zuri kwa wachezaji wengi hususani wenye umri mdogo kupotea kwenye medani ya soka la Tanzania. Ni kitu ambacho wachezaji wenye kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kujiangalia kwa jicho la pili na kuona nini cha kufanya ili kukabiliana na hali hiyo ambayo imekuwa ni aibu katika miaka ya hivikaribuni. Hali hiyo pia ndiyo imekuwa ikisababisha Taifa linakosa wachezaji wa kulipwa wanaocheza nje.

Maoni yetu ni kwamba wachezaji haswa chipukizi wanapaswa kujitathmini na kuangalia mwenendo wao kwenye maisha ya soka kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe na soka la Taifa kwa ujumla.

Hata klabu pia ziwasaidie wachezaji kwa ushauri na akili ili ziwatumie muda mrefu na wanufaike nao pia. Kufa kwa viwango vya wachezaji ndani muda mfupi kunaingiza klabu kwenye gharama za kufanya usajili mpya jambo ambalo linaweza kuepukika kama wakiweka miundombinu mizuri hata ya kuangalia afya zao mara kwa mara.