Bado tunaishi na wasiwasi kwa mwamuzi zama za televisheni?

Muktasari:

Unajua sababu? Wataficha sana, lakini sababu ni kwamba walikuwa wanahofia Simba na Yanga watakimbizana kwenda kumhonga. TFF ina hofu na waamuzi wake. Nchi ina hofu na waamuzi wake. Halafu cha kushangaza mechi ipo live katika televisheni.

WAKATI Azam Tv wakianza kazi nilidhani ulikuwa mwisho wa kuhofia ujinga wa waamuzi. Nilikosea sana. Mwamuzi wa pambano la Simba na Yanga lililochezwa Jumamosi jioni alifichwa sana. Alijulikana saa 24 kabla ya kuchezwa kwa mechi.

Unajua sababu? Wataficha sana, lakini sababu ni kwamba walikuwa wanahofia Simba na Yanga watakimbizana kwenda kumhonga. TFF ina hofu na waamuzi wake. Nchi ina hofu na waamuzi wake. Halafu cha kushangaza mechi ipo live katika televisheni.

Zaidi ya Watanzania milioni 20 wapo mbele ya kamera zao, lakini TFF pamoja na klabu za Simba na Yanga zina hofu na mwamuzi. Watu wanahofia kwamba mwamuzi atajulikana mapema halafu atahongwa na kupendelea timu fulani. Inachekesha sana.

Kwanza kabisa hauwezi kumpata mwamuzi ambaye haipendi Simba au Yanga katika nchi hii. Ni vigumu sana. Lakini hata awe shabiki wa Simba au Yanga mpira hauchezwi chumbani, unachezwa hadharani. Mbaya zaidi siku hizi soka linachezwa mbele ya kamera za Azam TV.

Inahitaji mwamuzi mwenye roho ya ajabu kupindisha sheria na kuharibu kazi yake. Mwamuzi anaweza kukosea mara moja au mara mbili, lakini kudhamiria kupendelea katika mechi kama ya Simba na Yanga juzi inatia ukakasi. Kwa mfano, jazba ilitawala katika pambano la kwanza ambalo liliisha kwa sare ya 1-1. Amissi Tambwe aliunawa mpira kwa mkono kabla ya kufunga. Kama Martin Saanya alidhamiria kufanya madudu jaribu kuona jinsi ambavyo TV zilivyomuumbua. Hata hivyo, bado naamini kwamba Saanya alipitwa na baadhi ya matukio kutokana na udhaifu wa kibinadamu tu.

Nilifahamu kuwa Mwamuzi Mathew Akrama au mwamuzi yeyote yule ambaye angepewa filimbi kuchezesha mechi ya juzi angefanya vizuri tu. Kwa sasa waamuzi wanakwenda kutibua mechi ya Mtibwa Sugar na Toto Africans ambayo haionyeshwi katika televisheni. Ni vigumu kwao kufanya makusudi kupendelea.

TFF iachane na upuuzi wa kuendekeza kuficha majina ya waamuzi wa mechi ya Simba na Yanga. Hii ni mechi kama zilivyo nyingine. Ni jukumu la watu tunaotazama soka kwenye televisheni kuwaumbua waamuzi. Haiwezekani tukaendelea kuishi kwa wasiwasi katika zama za televisheni.

Kama mwamuzi anaweza kupendelea timu mbele ya kamera za televisheni, basi soka letu limefika pabaya. Kama hali ni hiyo basi hatutakuwa tena na dawa dhidi ya waamuzi. Kama mwamuzi hana haya mbele ya kamera za TV na macho ya Watanzania milioni 45, basi hatuna haja ya kuendelea kucheza mpira nchi hii. Lakini pia turudi nyuma na kujiuliza. Wakati mpira haupo katika televisheni mbona zamani klabu zilikuwa hazina hofu kubwa ya waamuzi? Zamani watu walikuwa na hofu ya ushirikana zaidi. Kuna makomandoo walikuwa wanalinda mipira itakayochezewa pale ofisi za TFF kuanzia asubuhi mpaka wakati wa mechi.

Zaidi ya yote hayo, upinzani wa zamani wa Simba na Yanga ulikuwa mkubwa kuliko huu wa leo. Kwa nini kulikuwa hakuna hofu na mambo ya waamuzi na badala yake yalikuwepo zaidi kwa ushirikina?

Kwa nini hofu hiyo imeondoka imehamia kwa wachezaji na waamuzi? Sababu ni moja tu. Siku hizi soka limevamiwa na watu ambao si wa soka. Wenyewe wanajuana na ndio maana wanahofiana. Wanajua ujinga wanaoufanya. Watu hawa wanataka matokeo ya haraka haraka bila ya kuwekeza.

Ni mabingwa wa kumiliki namba za simu za waamuzi na wachezaji wa timu pinzani. Bahati nzuri wanajulikana.

Wengine wamewahi hata kurekodiwa. Lakini nani anajali? Hakuna na wala hawajawahi kuchukuliwa hatua.

Watu hawa wamepata nafasi katika ofisi fulani kubwa mijini na rafiki zao wamewaleta katika mpira. Kwa sababu wana pesa, basi inakuwa rahisi kwao kupewa madaraka katika soka. Wengi hawafahamu lolote kuhusu soka.

Wengine ni wale ambao wameingia katika mpira kwa ajili ya kutafuta umaarufu wa kisiasa na kwenda kugombea ubunge. Hawa nao wapo wengi.

Wameletwa na rafiki zao, lakini ufahamu wao na soka bado upo chini.

Hawa ndio wamejaa kwa sasa. Wamejaa katika klabu zetu na wamejaa katika TFF kuu na zile za mikoani. Na ndio maana umaarufu wa kununua mechi umekuwa mkubwa siku.

Ndio maana leo mwamuzi anakuwa siri wakati zamani mwamuzi alikuwa anajulikana wiki mbili kabla ya mechi tena bila ya uwepo wa televisheni na watu walikuwa hawahofii sana.

Tutaendelea kuwaficha waamuzi hadi lini? Mjue wenzetu walioendelea wakisikia watatucheka. Tusipowandoa watu hawa katika soka letu, basi maisha yetu yataendelea kuwa haya haya tu kila siku. Usitegemee kama tutabadilika.