ROHO NYEUPE: Bado kidogo tutaanza kuzika soka la Mbaraka Yusuf

MBARAKA Yusuf. Ni miongoni mwa chipukizi wachache wanaofanya vizuri katika soka la Tanzania kwa sasa. Hivi majuzi aliifungia, Taifa Stars, bao la ushindi dhidi ya Burundi, tena akitokea benchi. Inapendeza sana.

Mbaraka ni chipukizi wa kweli. Huu ni msimu wake wa pili tu Ligi Kuu Bara. Msimu uliopita alianza kucheza hapo hapo Kagera Sugar akitokea Simba kwa mkopo. Kabla ya hapo alikuwepo katika timu ya vijana ya Simba.

Kwa haraka unaona kabisa kuna hatua ambayo straika huyo amepiga. Msimu uliopita alifunga mabao saba Ligi Kuu lakini msimu huu zikiwa zimebaki mechi sita, tayari amefunga mabao 10, inavutia sana. Kama ni mtoto unaweza kusema anakua.

Uzuri ni kwamba alifunga katika mechi yake ya kwanza tu ndani ya Stars. Huwa inatokea mara chache sana mambo kama haya. Yawezekana hata Mbwana Samatta mwenyewe hakufunga katika mechi ya kwanza aliyoitwa Stars. Ni wachache wenye bahati hiyo.

Kwa msimu huu, Mbaraka ni miongoni mwa chipukizi wanne wanaofanya vizuri katika ligi. Wa kwanza ni Shiza Kichuya wa Simba. Kichuya licha ya kucheza winga,  tayari ana mabao 11. Inatia moyo.

Chipukizi mwingine ni Hassan Kabunda wa Mwadui. Msimu huu tayari amefunga mabao matano. Mwezi uliopita wa Februari alitangazwa Mchezaji Bora. Ni mafanikio makubwa sana kwa mchezaji ambaye hana misimu mitatu Ligi Kuu.

Mwingine ni Raphael Daud wa Mbeya City. Licha ya kucheza nafasi ya kiungo,  tayari amefunga mabao manane. Msimu uliopita alifunga mabao tisa katika mashindano yote. Anaonyesha kukua kwa kiwango kikubwa.

Hao ndio chipukizi ambao wanacheza kwa kiwango cha juu kwa wakati wote msimu huu. Kasi waliyoanza nayo mwezi Agosti mwaka jana wanayo mpaka sasa. Siyo watu wanaobahatisha sana.

Wapo chipukizi wengine kama Omary Mponda, Riffat Khamis, Gadiel Michael, Shaban Iddi na wengineo ambao wanaonyesha vipaji, lakini bado hawajaweza kuwa na kasi ya kuvutia kama wenzao hao niliowataja awali. Kuna wakati wanapanda na kuna wakati wanashuka.

Tuachane na hayo kwanza, turejee kwa Mbaraka. Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba tunaweza kumharibu staa huyo ndani ya siku chache tu zijazo. Historia inaonyesha kwamba wachezaji wengi tumewaharibu sisi wenyewe.

Mosi, straika huyo anamaliza mkataba wake na Simba msimu huu. Ikumbukwe kwamba anacheza Kagera Sugar kwa mkopo japo kuna magumashi yanadaiwa kufanyika. Kama unavyojua Kagera inatoka mkoa wa ‘Baba’ hivyo kuna mambo fulani yalilazimishwa tu.

Mwishoni mwa msimu tutaona timu kadhaa zikianza kuzunguka naye. Yanga watapeleka ofa. Simba watapeleka ofa. Pengine na Azam nao watapeleka ofa. Hapa ndipo tunapoanza kummaliza straika huyu.

Siyo kwamba timu hizi zinaona ana nafasi ya kucheza kwao, hapana. Timu hizi zinataka tu kumsajili kwa kuwa anafanya vizuri. Hivi ndivyo Yanga ilivyowaua Matteo Anthony, Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi.

Walionekana kuwa ni wachezaji wenye vipaji vikubwa, lakini sasa wamefeli na kuwa wachezaji wa kawaida sana.

 Siku hizi Mwashiuya hatishi tena. Siku hizi Mahadhi havutii tena kumtazama. Matteo ndiyo hachezi tena. Inasikitisha sana. Yanga imeua wengi.

Wachezaji ambao tuliona wanaweza kupiga hatua na kusonga mbele wamekwisha ghafla. Nuru yao imepotea gizani. Mchezaji anasajiliwa kwa kuwa tu aliifunga timu fulani ama alicheza vizuri dhidi ya timu fulani. Hatutazami mbele zaidi.

Mfano wachezaji Emmanuel Martins na Pastory Athanas walisajiliwa Simba na Yanga kutokana na mihemko tu, mwisho wa siku hakuna kitu wanachofanya. Martins amekuwa ni mchezaji wa kawaida tu, hatishi wala havutii. Athanas ndiyo kwanza hayupo hata kwenye mipango ya kocha Joseph Omog. Hivi ndivyo tunavyowamaliza wachezaji hawa kirahisi tu. Martins alisajiliwa tu kwa kuwa aliifunga Yanga mabao mawili katika mechi ya kirafiki. Athanas alisajiliwa tu kutokana na kitendo chake cha kuifunga Yanga akiwa Stand United. Inasikitisha sana kuona namna tunavyofanya usajili wetu. Tunashindwa kuwasajili wachezaji kwa matakwa ya kiufundi na mwisho wa siku tunawamaliza wenyewe.

Wakati mwingine umakini unahitajika ili kuwasaidia wachezaji. Huyu Mbaraka wa leo akijiunga na Simba ama Yanga inaweza kuwa ndiyo mwisho wa maisha yake ya soka. Kuna wakati inabidi mchezaji aimarike zaidi na zaidi kwanza japokuwa fedha huwavuruga.

Leo hii Yanga inaendelea kubaki na Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Amissi Tambwe, ikimsajili Mbaraka atakwenda kucheza wapi? Kifo huwa kinaanzia hapo. Malimi Busungu na Matteo watafia hapa wengine wengi tu.