BENCHI LA UFUNDI: Ushindani ndani ya VPL ndio utamu wenyewe

Muktasari:

  • Na hapa unaweza kuona ni kiasi gani timu zinapata tabu kushinda mechi mfululizo, hivyo kukosa muendelezo na kuzifanya kuokoteza pointi moja moja zinazotokana na sare na ushindi usiotabirika.

SIO jambo la kushangaza kabisa kwa hali ilivyo katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu baada ya mzunguko wa kwanza, ikionyesha jinsi timu zilivyokabana koo huku baadhi hususan Majimaji ya Songea iliyoianza ligi vibaya ikiburuza mkia kwa muda mrefu.

Lakini, tayari Kocha, Kally Ongala amerejea tena kwa ajili ya kuinusuru timu hiyo. Hadi hapo msimamo unaonyesha Majimaji baada ya kukamilisha michezo yake 15 imepanda kutoka mkiani na kushika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 16 na kuzitimulia vumbi timu za JKT Ruvu na Mwadui zenye pointi 13 kila moja zikizidiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Toto African inayoburuza mkia kwa sasa ikiwa na pointi 12, kuthibitisha kwamba Majimaji ndiyo timu iliyoonyesha mabadiliko makubwa katika mzunguko wa kwanza.

Hapa ndipo unapoweza kugundua ugumu wa ligi msimu huu, kwani hata tofauti ya pointi kati ya timu zinazoongoza msimamo wa ligi, Simba na Yanga, si kubwa na inaendelea kuzitia hofu timu hizi na kufanya mzunguko wa pili wa ligi kuwa mkali zaidi na usiotabirika.

Wakati timu hizi zilipokuwa zimebakiza michezo miwili pekee ili kukamilisha mzunguko wa kwanza, Yanga iliachwa mbali na Simba, hali iliyowatia hofu Wana Jangwani hao huku hamasa na matumaini yakijengeka zaidi kwa Wana Msimbazi na sasa mambo yamebadilika baada ya Simba kupoteza mechi mbili na kufanya tofauti kati yao kuwa pointi mbili hivyo, wote kuwa na nafasi sawa katika mbio za kuelekea ubingwa.

Siku zote uhondo wa ligi ni pale timu zinapoingia uwanjani zikiwa na nafasi sawa ya kushinda hivyo, kufanya mechi zisitabirike kama ilivyotokea katika mechi ya African Lyon dhidi ya Simba wakati wengi hawakutegemea timu hii inayodhaniwa kuwa ndogo ingeweza kufanya kile ilichokifanya na kuifunga Simba bao 1-0 na kuvurugia rekodi yake ya miaka ya nyuma ilipofanikiwa kubeba ubingwa bila kupoteza mechi.

Kama vile haitoshi Simba ilipoteza tena dhidi ya Prisons ya Mbeya kwa mabao 2-1 kudhihirisha ugumu wa ligi msimu huu.

Ni vema viongozi wa soka nchini wakajifunza kutokana na yale tuliyoyashuhudia katika ligi mbalimbali ulimwenguni kuwa kinachojalisha siku zote ni pointi unazozikusanya pia mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kumaliza ratiba, na hilo ndilo linaloamua nafasi ya timu mwishoni mwa ligi, hivyo timu inaweza kuwa katika fomu nzuri kabisa na kushinda mechi, lakini kadiri michezo inavyoendelea wachezaji hutokea wakapata majeraha au kuchoka na ndipo matokeo yasiyotarajiwa huanza kujitokeza.

Kama ilivyojionyesha kwa mechi za kwanza za Yanga,  na si ajabu ikatokea kwa timu kubwa na yenye mashabiki wengi na iliyowekeza kwa kiwango kikubwa ikapoteza mchezo dhidi ya timu ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa kufungwa tena kwa mabao mengi na hilo huwa haliwashangazi mashabiki wa huko Ulaya na kwingineko kama ilivyo hapa nyumbani ambapo, tayari kiongozi mmoja wa timu kubwa anayeheshimika amesikika akianza kulalama na kuonyesha wasiwasi akishutumu kuwa baadhi ya wachezaji wa timu yake kucheza chini ya kiwango kwa makusudi, jambo ambalo linaweza kuwavunja moyo wachezaji na kusababisha timu kufanya vibaya zaidi.

Matamshi kama haya yanaweza kuleta madhara makubwa hata kuweza kusababisha mpasuko ndani ya klabu kisha kuirudisha timu nyuma kule ilikotoka. Kwani miongoni mwa sifa za kiongozi wa michezo ni uungwana, uvumilivu, subira na kuwaheshima wadau wote wakiwemo wachezaji.

Kazi ya benchi la ufundi ni kuiandaa timu kwa kufundisha mbinu mbalimbali zinazoweza kuisaidia timu kupata ushindi, pia kurekebisha makosa ya wachezaji mazoezini pindi yanapojitokeza na ni jukumu lao kupandisha na kuboresha viwango vya wachezaji, na si kuwatupia lawama tu kwani wachezaji sio vipuri vya kubandika na kubandua.

Timu inapofanya vibaya na kusababisha matokeo yasiyotegemewa hilo ni jukumu la mwalimu kurekebisha hali hiyo na si kuanza kutafuta wachawi nje ya mfumo wa mchezo wenyewe. Hali hii inatia wasiwasi na inaweza tu ikathibitisha kuwa soka letu bado linaendeshwa kishabiki kwani, tatizo la ufundi hutafutwa kwa kutumia vigezo vya ufundi, pia hutatuliwa kwa ufundi.

Ligi ya msimu huu imekuwa na mvuto mkubwa hadi hapa ilipofikia na moja ya vivutio ni pale unapouangalia msimamo wa ligi na kuzipata timu takriban nne zikiwa na pointi 19 kila moja huku zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa peke yake na zikifuatana zote kuanzia nafasi ya saba inayoshikwa na Prisons hadi ya 10 inayomaliziwa na Ndanda.  Na hapa unaweza kuona ni kiasi gani timu zinapata tabu kushinda mechi mfululizo, hivyo kukosa muendelezo na kuzifanya kuokoteza pointi moja moja zinazotokana na sare na ushindi usiotabirika.

Lakini, pamoja na yote hapa ndipo ulipo utamu wa ligi, na unapoziangalia timu zilizopo mkiani mwa ligi, nazo zimo katika vita kali kuhakikisha hazishuki daraja kwani, msimamo wa ligi unaonyesha JKT Ruvu na Mwadui zikiwa katika nafasi ya 14 na 15 huku zote zikiwa na pointi 13 na kutofautiana mabao ya kufunga na kufungwa hali inayozilazimisha timu hizi kufanya juhudi za makusudi kujinasua katika nafasi hizo katika mzunguko wa pili wa ligi.

Ni vema timu zote zikalitumia vizuri dirisha dogo la usajili ili kurudisha makali pia kuendeleza ari ya mapambano ili kujiweka mahali salama.