BENCHI LA UFUNDI : Matokeo yataendelea kutesa mashabiki nchini

Muktasari:

Mashabiki wa soka hufurahi na wengine huwa na huzuni kutokana na matokeo na wakati mwingine hata kupoteza maisha kutokana na matokeo ya kwenye viwanja vya soka.

NI kwanini leo nisizungumzie matokeo katika soka wakati ndiyo yanayokuwa sababu ya kuacha historia ya aina yake katika soka?

Mashabiki wa soka hufurahi na wengine huwa na huzuni kutokana na matokeo na wakati mwingine hata kupoteza maisha kutokana na matokeo ya kwenye viwanja vya soka.

Viongozi nao huwa na wakati mgumu wengine hutimuliwa kutokana na matokeo mabaya viwanjani, majumbani chakula hakiliki kutokana na matokeo.

Watu hutaniana na kurekebishana kutokana na matokeo ya viwanjani huku wengine wakifikia hatua ya kuwaita wenzao wa mchangani na kuwafanya wanune na kujiapiza iko siku watalipiza kisasa.

Yote hayo ni kutokana na matokeo ya viwanjani ambayo siku zote huamua yupi kashinda na nani kashindwa, uwanjani wapo wanaotuhumiwa na viongozi huku wengine wakihusishwa na kuuza mechi na kusababisha timu zao kupata matokeo tofauti na yaliyotarajiwa .

Viongozi hutaka kusajili timu bora ili tu kupata matokeo mazuri, timu hupelekwa Ulaya na kwingineko kujiandaa ili kuimarika ili tu waweze kupata matokeo mazuri na zile timu ambazo zipo zipo tu hakuna jingine isipokuwa kupata matokeo, hata wapenzi wa soka siku zote hutegemea makocha kuwapatia matokeo yanayowaridhisha. Hivi ndiyo ilivyo na siku zote watu wataendelea kudai matokeo.

Makala yangu ya leo inalenga kuonyesha kwamba mafanikio ya timu ya soka yanapimwa na matokeo mazuri, viongozi wasiojituma na kukosa ubunifu wanazisababishia timu zao kupata matokeo mabaya na kuwafanya wapenzi na wanachama kupata maumivu makali ambayo kama nilivyogusia hapo juu wakati mwingine husababisha vifo .

Hivi bila matokeo yasiyoridhisha kwa baadhi ya timu maarufu na vigogo vya soka nchini ambao, misimu kadhaa ya hivi karibuni wameonyesha kupotea njia, utani ule ulio na ukakasi dhidi yao ungepata wapi nafasi na hata wale makocha kwa nini wafukuzwe? Na hata wachezaji wangetuhumiwa kwa lipi, hiyo ndiyo kusema kwamba matokeo yanaponza kweli.

Hapo zamani kumbukumbu zinaniambia kwamba pale Dodoma makao ya nchi wengine wakipaita Dodomya, ipo timu inayofahamika rasmi kwa jina la CDA a.k.a Watoto wa Nyumbani, timu hii iliwahi kuwa fahari ya mji mkuu wa Dodoma, vijana walikuwa balaa enzi hizo miaka ya 1980 kuelekea 90 na kufanikiwa kuitwa Kiboko ya Vigogo yaani Yanga na Simba.

CDA nakumbuka waliwahi kuifunga timu moja wapo kati ya vigogo ambayo jina lake linafanana na mnyama na matokeo gazeti moja wapo hapa nchini likatoa katuni ya mnyama mkali akionyesha analia akiugulia uchungu huku mkuki ukiwa umekita mgongoni na mkia ukininginia katika hali ya kusikitisha.

Pembeni yake akionekana kijana shujaa wa kabila la wagogo katika vazi la kimila akishangilia- Agwe agwe basi.

Utani na vicheko vilipamba moto kwa timu hiyo kutaniwa Agwe Agwe kukoleza ujumbe wa katuni ile, yote hiyo ilisababishwa na matokeo, leo hii baada ya miaka kadhaa kupita, machungu kama yale ya vicheko na utani uliwanyima raha kambi ile ile sasa vimerejea kwa staili nyingine.

Staili hiyo inayobeba taswira ya kejeli zaidi ya utani wa Wamatopeni na Mchangani, nani alaumiwe hapa.

Yote hiyo inatokana na matokeo mabovu, nani angethubutu kuyasema haya kama timu hiyo ingekuwa na matokeo mazuri.

Kwa sasa timu yetu ya taifa bado haijakaa vizuri, tunasema hivyo kwa sababu moja kubwa ni matokeo yasiyoridhisha.

Ni nini hasa Tanzania inachohitaji toka kwa wachezaji wa timu hii? Hakuna zaidi ya matokeo ya kuridhisha.

Ni wazi sasa baada ya yote hayo kuhusu matokeo, ndipo naweka wazi kuwa matokeo mazuri hayapatikani iwapo hatutaona umuhimu wa kuandaa mazingira bora yanayowezesha kupatikana matokeo bora.

Soka la Tanzania bado litaendelea kusuasua na kuwasababishia Watanzania hususan mashabiki na wapenzi wa mchezo huu maumivu na vifo kutokana na msongo wa mawazo sababu tu mchezo wa soka unalenga kuleta furaha kwa wapenzi na mashabiki wake na hilo haliwezi kutokea bila ya kupata matokeo mazuri.

Ni vema watu wakafahamu kuwa ili matokeo mazuri yapatikane ni lazima wapatikane viongozi bora walio na weledi, ubunifu, wanaosukumwa na dhamira na mapenzi ya dhati kwa mchezo huu.

Viongozi wa namna hii wanapaswa kuwa na muono wa mbali ili kuweza kubuni mipango bora ya maendeleo kwa mchezo ikiwa ni pamoja na kuzalisha makocha bora na wachezaji bora waliojengwa kwa utaratibu sahihi ili mwisho wake nchi hii iweze kupata matokeo ya kuridhisha.Si bora matokeo tu, vinginevyo matokeo yatabaki kuwa matokeo kama ilivyo siku zote .

Ushindi wa Serengeti Boys ni matokeo bora na yameleta faraja kwa taifa na haya ndiyo matokeo tunayoyakusudia katika taifa hili kubwa Afrika Mashariki tofauti na hivyo, mashabiki hawatachoka kulilia matokeo mazuri.