STRAIKA WA MWANASPOTI : Afcon ibadilishiwe muda ili kuongeza mvuto

Muktasari:

Mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo ilipigwa kati ya wenyeji Gabon dhidi ya Guinea- Bissau na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika 90.

MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), 2017 yalianza rasmi nchini Gabon mwishoni mwa wiki iliyopita na mpaka sasa mechi kama sita zimepigwa ndani ya viwanja tofauti.

Mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo ilipigwa kati ya wenyeji Gabon dhidi ya Guinea- Bissau na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika 90.

Burkinafaso ilifuatia kwa kuvaana na Cameroon na kutoshana nguvu kwa kufunga pia bao 1-1 katika mechi za Kundi A.

Siku ya pili ya fainali hizo Algeria ikiongozwa na nyota wao, Riyad Mahrez ilipiga soka kali, lakini ikaishia kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Zimbabwe kabla Senegal kuwashangaza wengi baada ya kuinyuka Tunisia 2-0.

Matokeo ya ushindi wa Senegal dhidi ya Tunisia yameshangaza wengi na wakati tukiingia mitamboni kulikuwa na mechi mbili za kukata na shoka za Kundi C zilikuwa zikitarajiwa kuchezwa usiku wa jana.

Watetezi wa Kombe hilo, Ivory Coast ilikuwa ikivaana na Togo na Mabingwa wa CHAN, DR Congo walikuwa wamalizane na Morocco.

Hata hivyo ukweli ni kwamba michuani ya mwaka huu kabla ya kuanza huwa hayakosi dosari mbalimbali. Timu ya Zambia kulikuwa na mshike mshike kati ya wachezaji na viongozi, kisa ikiwa ni suala la posho zao. Kulikuwa na kutoelewana hasa kwa upande wa marupurupu yao kabla ya wao kusafiri kuelekea Gabon. Vile vile katika kambi ya Cameroon kumekuwa na kutoelewana kwa hayo hayo na kuweza kufanya wachezaji kadhaa kutojiunga na timu yao ya taifa kwa ajili ya michuano hiyo.

Wachezaji ambao huwa kikosi cha kwanza cha Cameroon wengi walisusia Afcon na kulazimisha kocha kubadilisha kikosi chake bila kutarajia. Ndani ya wiki moja kabla kusafiri kuelekea Gabon wachezaji mahiri karibia nane walijiondoa katika mashindano hayo wengi wakizingatia kuendelea kuzitumikia klabu zao.

Wakali kama Eric Maxime wa Schalke 04, Joel Matip wa Liverpool, Andre Onana wa Ajax FC, Allan Nyom wa West Brom, Maxime Poundje FC wa Bordeaux, Andre Frank Zambo (Olimpique Mersaille) na Ibrahim Amadou (Lille) walisusa.

Wamekifanya kikosi cha Cameroon kudhoofika, pia kufanya michuano hiyo kupungua ladha yake iliyotarajiwa. Kukosekana kwa nchi kama Nigeria kwenye fainali hizo nako kumepunguza uhondo wake. Kuna baadhi ya wachezaji walitarajiwa kuonekana na mashabiki kwenye fainali hizo za Gabon, lakini wamekosekana. Ni jambo gani hasa hufanya wachezaji kuamua kutosafari au kukubali kuwakilisha nchi zao kwenye mashindano makubwa kama hayo?

Jambo la kwanza kabisa ni mchezaji akiwa na majeraha na anajua ya kwamba akizidi kucheza jeraha hilo litazidi kuongezeka, inakuwa ni vigumu kwake kuweza kujiunga na timu ya Taifa. Hilo kwangu ni jambo ambalo niliweka kama ni utovu wa nidhamu. Lakini kuna baadhi ya wachezaji ambao wemeweka hela mbele kwanza kuliko nchi. Kuitumikia nchi yako wakati wa dhiki na faraja huwa jambo zuri sana. Wachezaji wengi wao huweka hela mbele kwanza.

Ukumbuke ya kwamba wakati wanapoamua kusafiri mishahara na marupurupu ya klabu zao husimamishwa. Shida inakuja wakati nchi au taifa linawapa hela kidogo wakilinganisha na hela ambazo wanalipwa na klabu zao, hivyo wengine huamua kususia.

Hilo kwangu ndilo jambo la utovu wa nidhamu na kukosa uzalendo kama ambavyo limefanyika kwa wachezaji wa Cameroon. Lakini wanachosahau ni kwamba hiyo hiyo nchi ndiyo iliwapa ngazi ambayo wameitumia kufika waliko. Wachezaji wengi hupata mialiko ya kucheza soka katika klabu kubwa duniani kwa sababu ya kuonekana wakizichezea nchi zao. Ikiwa nchi ilikupa ngazi na ukaonekana duniani na klabu kote duniani na ukapata ulaji kupitia kwa mechi za kimataifa, sasa inakuwaje wakishafanikiwa wanadhulumu nchi zao tena? Mambo kama haya yamekuwa yakijitokeza hasa hapa Afrika kwa sababu ya kukosa mipangilio kabambe. Kwangu ningependa kuwasihi viongozi wetu hasa Afrika, angalau waweze kuweka mikakati ya kulipa wachezaji wakati wowote ule wanapoitwa kuziwakilisha nchi zao.

Ijulikane tu kuanzia mwanzo hadi mwisho ni marupurupu gani na kiasi kipi watakacholipwa mradi wameitwa katika timu za Taifa. Nashangaa nchi kama Cameroon kila kukicha ni malumbano tu. Siku za nyuma ilibidi Samuel Et’oo kujitolea kulipa marupurupu ya wachezaji wote wa timu ya Taifa. Haya yataendelea hadi lini? Kwa upande wa CAF ningependa pia kuwasihi wabadilishe kalenda yetu angalau iwezeshe wachezaji wetu kushiriki katika mashindano hayo kikamilifu. Inakuwa pia vigumu kwa makocha kuachilia wachezaji wake kusafiri. Ukiangalia klabu kama ya Leiceste City kupoteza wachezaji wake mahiri Mahrez na Slimani kwa Algeria kuliwaathiri sana katika mechi yao dhidi ya Chelsea. Mechi ambayo Leicester watetezi wa EPL walipokea kichapo nyumbani kwao. Pia kwa upande wa wachezaji inakuwa ni ngumu kusafiri kwa kuhofia kupoteza nafasi zao katika klabu zao punde waendapo Afcon. Naamini kama michuano hiyo itabadilisha kalenda kutoka Januari hadi Juni ili iambatane na kalenda ya FIFA wengi watashiriki.