TFF inapaswa kuepuka aibu zisizo za lazima

Muktasari:

  • Ratiba inaonyesha baada ya timu hizo kupambana zilikuwa zikikabiliwa na michezo mingine dhidi ya Majimaji na Ndanda katika tarehe ambayo TFF ilipendekeza, lakini busara za viongozi wa Simba na Azam zimesababisha mchezo kutoahirishwa tena.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kwa mara nyingine lilikaribia kuingia kwenye aibu nyingine ya mtindo wake wa panga pangua ya ratiba ya Ligi Kuu Bara.

Ilikuwa tayari kupangua ratiba ya mchezo wa Azam na Simba kwa kisingizio cha kupisha pambano la kimataifa la timu ya taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys itakayochuana na Congo katika kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.

Mchezo wa Simba na Azam ulipangwa kuchezwa Jumamosi hii, lakini TFF ikataka usogezwe mbele mpaka Septemba 24, ambapo kwa yakini ungetibua pia ratiba ya mechi za wikiendi hiyo kwa timu hizo na nyingine kwa jumla.

Ratiba inaonyesha baada ya timu hizo kupambana zilikuwa zikikabiliwa na michezo mingine dhidi ya Majimaji na Ndanda katika tarehe ambayo TFF ilipendekeza, lakini busara za viongozi wa Simba na Azam zimesababisha mchezo kutoahirishwa tena.

Simba na Azam zitacheza kama kawaida ila sio tena kwenye Uwanja wa Taifa, ila Uwanja wa Uhuru ambao tayari mechi kadhaa zimeshachezwa mpaka sasa na hata siku za nyuma kabla ya kujengwa kwa Uwanja wa Taifa mechi kama hiyo ilichezwa hapo.

Mwanaspoti inadhani kilichotaka kufanywa na TFF ni ugonjwa uleule ambao licha ya kupigiwa kelele na wadau wa soka wakiwamo wanahabari, bado haujapatiwa tiba na ni kama viongozi wa shirikisho hilo bado wanaishi enzi za ujima na sio dunia ya sasa yenye kwenda kwa kasi ya mabadiliko ya kisasa.

Kilikuwa ni kitu cha kushangaza kwa TFF kutaka kutibua ratiba kwa kisingizio cha mechi ya Serengeti Boys, ilihali jijini Dar es Salaam kuna viwanja vinne vya kisasa ambavyo vingeweza kutumiwa kwa mchezo huo wa kimataifa.

Mechi ya Serengeti inachezwa Jumapili, mchezo wa Ligi Kuu wa Simba na Azam umepangwa Jumamosi, kulikuwa na sababu gani ya kutaka kuzingua ratiba wakati hata kama wageni walikuwa wakitaka kuutumia Uwanja wa Taifa, Uwanja wa Uhuru si upo?

Ingawa Rais wa TFF, Jamal Malinzi alishakaririwa kuwa, upanguaji wa ratiba ya Ligi Kuu hautaisha na haukwepeki, lakini sababu nyingine za kupangua ratiba hiyo ni aibu kwao na wanapaswa kuepuka kama hakuna ulazima wowote kwa kufanya hivyo.

Hii ni mara ya pili kwa TFF kufanya jaribio la kuwatibua mashabiki, lakini mara zote imekuwa ikiaibishwa na viongozi wa klabu. Awali walitaka kutibua ligi kwa mechi za Azam jijini Mbeya kwa kisingizio cha pambano la kukamilisha ratiba la Taifa Stars dhidi ya Nigeria, lakini viongozi wa Azam wakawagomea na ratiba kubaki ilivyo.

Wakati hata mashabiki hawajaanza kusahau wanaibuka tena na kutaka kuleta madudu mengine, hii ni aibu kubwa kwa shirikisho linaloongozwa na viongozi weledi na wenye uelewa mpana wa kupambanua mambo.

Mwanaspoti tunaamini kabla ya upangwaji wa ratiba ya Ligi Kuu ni wazi TFF huangalia kalenda za michezo yote ya kimataifa na hata ile ya ndani kwa lengo la kuepuka muingiliano usio wa lazima ambao utakuwa unatibua ratiba kila mara.

Je, ni kwamba TFF hilo hawaliangalii? Kama hawaliangalii basi ni kosa ambalo litaendelea kuliaibisha shirikisho hilo kila msimu na kuwaachia maswali mengi mashabiki wa soka chombo hicho kinaongozwaji kama bado kipo enzi za FAT.

Tunaamini jambo kama lililotaka kutokea kwa mchezo wa Jumamosi hii, litakuwa mwanzo na mwisho kwa viongozi wa TFF kulazimisha aibu pasi na sababu na badala yake ielekeze nguvu zake katika kuona Ligi Kuu ikichezwa kwa ufanisi na mafanikio.