JICHO LA MWEWE: Yanga walifungwa kabla hawajaugusa Uwanja wa Taifa

Muktasari:

  • Wakati Simba wakielekea Zanzibar kama kawaida, Yanga walijiathiri kwa kwenda Kigamboni. Kuanzia hapo mashabiki hawakuiamini tena timu.

YANGA walilala mapema. Ni katika pambano lao la juzi dhidi ya watani zao, Simba. Bahati nzuri sana wengi wao hawakubisha kwamba walistahili kufungwa na Simba. Sijui kwa nini lakini ilianzia kabla Mwamuzi, Mathew Akrama hajapuliza filimbi la kuanzisha pambano lenyewe.

Walifungwa mapema kabla ya mechi yenyewe haijaanza. Sijawahi kuwaona Yanga wakiwa wakimya kabla ya mechi dhidi ya Simba kama juzi. Na wala sijawahi kuwaona Yanga wakiwa wakimya baada ya matokeo mabovu dhidi ya Simba kama ilivyokuwa juzi.

Bao lao lilikuwa la penalti, shukrani kwa ujinga kwa beki wa kati wa Simba, Novatus Lufunga. Baadaye wakapewa faida ya kucheza wakiwa wengi uwanjani kuliko Simba baada ya Akrama kumuonyesha kadi nyekundu Janvier Bukungu. Bado hawakuweza kutumia faida yoyote ile. Simba walisawazisha na kuongeza bao la pili.

Yanga walifungwa mapema kabla ya mechi haijaanza kwa sababu walishatibuka kisaikolojia. Kuelekea katika mechi hii  Simba hawakuwa vizuri sana kimchezo kama ilivyo kwa Yanga yenyewe. Hawakuwa na timu ambayo waliiamini sana lakini walijipanga vema kisaikolojia.

Mashabiki wengi wa Simba walitamba mitandaoni na kwingineko si kwa sababu ya uwezo wa timu yao. Hapana. Hapa katikati Yanga walikuwa na matatizo mengi zaidi ambayo walihisi kwamba wangeweza kutumia fursa hiyo kushinda mechi.

Ilianzia kwa maandalizi ya Yanga kuelekea katika mechi hii. mwenyekiti na tajiri wa Yanga, Yusuf Manji alikuwa na matatizo na dola ya nchi hii. Huyu ni mtu ambaye katika miaka ya karibuni alikuwa chanzo cha uhodari wa Yanga ndani na nje ya mipaka.

Matatizo ya Manji na Yanga yalikuwa yanaashiria kwamba Yanga ilikuwa katika maandalizi mabovu. Kwa kumbukumbu za haraka nakumbuka mara ya mwisho Yanga iliweka kambi Kigamboni kujiandaa na Simba mwaka 1999 nikimaliza kidato cha sita pale Shule ya Sekondari Jitegemee. Yanga walishinda 3-1.

Safari hii Yanga walirudia kuweka kambi Kigamboni kwa sababu ambazo wanaweza kusema zilikuwa na mantiki lakini ukweli ni kwamba mwenyekiti wao hakuwa na timu na alikuwa na matatizo na dola. Kama angekuwa yupo huru basi Yanga ingeweza kuweka kambi kwingine zaidi.

Siamini zaidi katika kambi. Naamini katika ubora wa wachezaji wanaojitambua. Lakini kwa Tanzania kambi imekuwa mwongozo wa wachezaji wetu. Hata wachezaji wenyewe wanaamini katika kambi. Hata wale wa kigeni ambao hawajakulia katika utamaduni huo pindi wakifika nchini nao wanaingizwa katika mkumbo wa kuamini katika kambi.

Wakati Simba wakielekea Zanzibar kama kawaida, Yanga walijiathiri kwa kwenda Kigamboni. Kuanzia hapo mashabiki hawakuiamini tena timu. Na wale wa Simba walijengeka na imani zaidi.

Mara zote wanazofungwa na Yanga basi watani zao wanakuwa wanatokea Zanzibar. Ni suala la kiimani tu.

Nje ya mambo ya kambi, wakati Yanga wakielekea kucheza mechi hii siku saba kabla walikuwa wametoka sare na timu dhaifu inayoitwa Ngaya Uwanja wa Taifa. Haijalishi kutokuwepo kwa kina Haruna Niyonzima au Amissi Tambwe. Yanga inaweza kuifunga timu bingwa ya Comoro kwa kutumia wachezaji wa akiba tu.

Kuanzia hapo mashabiki wao walianza kuguna. Wale wa Simba walikuwa wanajipa moyo zaidi kwa sababu walikuwa wametoka kuichapa African Lyon katika pambano gumu la FA. Kisaikolojia walikuwa vema zaidi.

Wakati mwenyekiti wao akifunguliwa kesi mpya na serikali kuhusu masuala ya vibali vya wafanyakazi wake, mshambuliaji Donald Ngoma alikuwa akiongea moja kwa moja mitandaoni na mashabiki wake akijinadi kwa kujiamini kwamba hatacheza mechi dhidi ya Simba.

Kuna madai kwamba aliwatoroka viongozi wa Yanga na kuwazimia simu kuelekea katika pambano hilo. Hii inakuonyesha jinsi gani mambo yalivyokuwa ovyo kwa upande wa Yanga huku kwa upande wa Simba wakijengeka kisaikolojia zaidi.

Wakati hayo yakiendelea, Haji Manara, msemaji wa Simba alikuwa akitamba kuwa ushindi ulikuwa lazima kama kifo. Yanga walikuwa wakiendelea kusinyaa.

Na ndani ya uwanja, hata Yanga walipofunga bao la penalti, halafu Bukungu akatolewa kwa kadi nyekundu, bado wachezaji wa Simba walionekana kutulia na kutafuta kitu zaidi uwanjani. Hapa walijengeka kisaikolojia kutokana na matokeo ya mechi yao iliyopita.

Wao Simba walikuwa wamepungua hivi hivi lakini bado wakarudisha bao kupitia kwa Shiza Kichuya. Na waliona wazi kwamba wangeweza kufanya kitu katika mechi hii hata kama walikuwa pungufu.

Imani yao ndio ambayo iliwapa nguvu na kufanya walichofanya. Mambo mengine hayahitaji uchawi hata kama najua kuwa waganga watakuwa wamechukua pesa nyingi kwa ushindi wa Simba.

Baada ya mechi ilidhihirika wazi kwamba Yanga walikuwa wamejiandaa kufungwa. Mashabiki wao walipanda daladala na kurudi makwao bila ya shida. Baadaye wakaingia mitandaoni na kuanza kutoa pongezi kwa wachezaji wa Simba. Huwa inatokea nadra sana kwa Yanga kufanya hivyo. Hata hivyo, safari hii walifanya kwa sababu walishajiandaa kufungwa mapema zaidi.