ROHO NYEUPE: Kila mchezaji mzuri ana upande wake wa pili

Muktasari:

  • Hata hivyo, pamoja na yote ni wazi kwamba kuna kitu hakiendi sawa kwa Ngoma. Ni dhahiri kuwa amejipambanua kuwa staa wa timu hiyo na uwezo wake ni wa juu kuliko mastraika wengine wote waliopo klabuni hapo.

NIMEFUATILIA kwa makini sekeseke linaloendelea baina ya Yanga na staa wao, Donald Ngoma kwa muda sasa. Ni mshike mshike kweli kweli.

Kuna taarifa zinazodai kwamba Ngoma haumwi na amekuwa akidanganya ili tu asicheze. Kuna taarifa nyingine zinadai Ngoma anaumwa na Yanga wanataka kumlazimisha acheze mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya watani zao, Simba. Kila mtu anaongea lake, ukweli anao Ngoma peke yake.

Hata hivyo, pamoja na yote ni wazi kwamba kuna kitu hakiendi sawa kwa Ngoma. Ni dhahiri kuwa amejipambanua kuwa staa wa timu hiyo na uwezo wake ni wa juu kuliko mastraika wengine wote waliopo klabuni hapo.

Licha ya kwamba, Amissi Tambwe ndiye aliyefunga mabao mengi kuliko Ngoma kwa muda ambao wamecheza pamoja, lakini bado hawafanani. Ngoma ana uwezo mkubwa wa kulazimisha mabao. Tambwe hana uwezo huo, ana uwezo wa kuvizia zaidi.

Ni wazi kwamba katika kikosi cha Yanga huwezi kumfananisha Ngoma na mchezaji mwingine yeyote. Uwezo wake uwanjani ni mkubwa na amewazidi vitu vingi mastraika wenzake pamoja na wachezaji wa nafasi nyingine pia. Huo ndio upande wa kwanza wa Ngoma ambaye juhudi zake msimu uliopita zilisaidia kuibeba Yanga hadi kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Unataka kubisha? Endelea kubishana na ukweli.

Hata hivyo, upande wa pili wa Ngoma ndio unaoonekana sasa. Usumbufu na utovu wa nidhamu. Ni jambo la kawaida kabisa kwa wachezaji wazuri, upande wao wa pili huwa mchungu kama ndimu changa.

Mabao aliyokuwa akifunga Ngoma. Nafasi alizokuwa akitengeneza Ngoma na kiwango chake cha jumla uwanjani hulipwa na upande huu wa pili. Ni lazima timu ikubali kumvumilia katika haya kama inapenda kuupata upande wake wa kwanza uwanjani.

Nasikia Kocha Hans Pluijm alipokuwa katika timu aliweza kumudu vizuri upande wa pili wa Ngoma. Pindi alipoona kuwa ana mechi ngumu na Ngoma haonyeshi dalili ya kutaka kucheza, alizungumza naye na kumuomba acheze. Hii ndiyo sababu Ngoma alikuwa imara nyakati za Pluijm.

Mbali na kwamba Pluijm ana misimamo yake na amekuwa mkali kwa wachezaji anafahamu wazi kuwa wachezaji wenye kitu cha ziada wana uchungu ndani yake. Yaani wako kama dhambi, tamu mwanzo ila mwisho chungu.

Wachezaji wazuri wako kama msichana mrembo pia. Anaweza kukupelekesha kwa kadiri anavyojisikia. Kama unataka kuwa naye ni lazima uvumilie upande wake wa pili. Akikujibu vibaya unamwambia ‘asante mpenzi’. Vizuri vina gharama zake.

Simba walikuwa na uvumilivu wao kwa Emmanuel Okwi. Alikuwa akiwasumbua anavyojisikia. Kuna wakati aliondoka Dar es Salaam kinyemela na kwenda kwao Uganda. Kuna wakati aliondoka kwa kuaga na kukawia kurudi. Hata hivyo, aliporudi walimpokea kishujaa na kumpa nafasi ya kucheza.

Uvumilivu wa Simba ndio uliwawezesha kuupata ubora wa Okwi vizuri. Uvumilivu wao uliwasaidia kupata milioni zaidi ya 800 kwa mauzo yake kwenda katika klabu mbili tofauti. Mvumilivu hula mbivu.

Kiongozi mmoja wa Azam alikuwa ananiambia kuwa nyuma ya staa wao wa zamani, Kipre Tchetche kulikuwa na mambo mengi. Uwanjani Tchetche angeweza kumpiga chenga Kelvin Yondani, kisha akamtoka Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kufunga bao tamu, lakini lenye maumivu ndani yake.

Kabla ya hapo utakuta Tchetche hakufanya mazoezi na wachezaji wenzake siku mbili ama tatu kwa wiki. Sheria zikiwekwa kambini Tchetche ndiyo alikuwa mtu wa kwanza kuzivunja. Wakiambiwa chakula cha mchana ni saa sita anaweza kwenda saa saba. Inahitaji uvumilivu.

Hata hivyo, Kocha Stewart Hall alikuwa anafahamu tabu hiyo ya wachezaji mastaa. Alimvumilia Tchetche na ubora wake ukaonekana uwanjani. Huu ndio upande wa pili wa mchezaji mzuri.

Wachezaji wengine kama Haruna Moshi ‘Boban’, Athuman Idd ‘Chuji’, Ulimboka Mwakingwe na wengineo nao walikuwa na upande wa pili ambao ni mchungu. Timu ziliwavumilia na kuweza kupata ubora wao.

Ni wachezaji wachache wazuri ambao hawana upande wa pili. Unaweza kuwahesabu kwa vidole. Kwa Yanga wapo Simon Msuva na Tambwe. Hawa huwezi kusikia wamekwaruzana na kocha ama kiongozi. Mbali na ubora wao uwanjani wana nidhamu ya hali ya juu.

Kwa Simba yupo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, huwezi kusikia amevunja sheria. Lakini wachezaji wengine kama Jonas Mkude na Ibrahim Ajib upande wao wa pili ni mchungu. Inahitaji uvumilivu kuwa nao.

Huko duniani wachezaji wengi wazuri nao wana matatizo hayo. Luis Suarez pamoja na uzuri wake alikuwa na tatizo la kung’ata wachezaji wenzake. Carlos Tevez alikuwa mchungu pale Manchester City. Diego Costa ni mchungu pale Chelsea lakini wote hawa wanavulimiwa. Unataka nimzungumzie Mario Balotelli? Hapana, huyu ni mchungu kila upande, sio upande wa pili tu. Hivyo Yanga inapaswa kuendelea kumvumilia Ngoma kama wanahitaji huduma yake.