HISIA ZANGU: Kabla ya Tanzania ya viwanda tupigane vita ya umasikini

Muktasari:

  • Hili la Serengeti Boys linaweza kuwa labda  lilipangwa kwa sababu vijana hawa ni wadogo na ndio kwanza wamekusanywa. Chini ya Kim Poulsen sina hofu sana.

JIONI ambayo Serengeti Boys walikuwa Chamazi maeneo ya Mbagala wakiichapa timu ya vijana ya Afrika Kusini, ndiyo jioni ambayo mtoto wa Mbagala, Mbwana Samatta alikuwa amefunga mabao mawili ugenini katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Lokeren Ligi Kuu ya Ubelgiji huku akiibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi hiyo kwa sasa.

Na jioni hiyo hiyo kilomita 9,486 kutoka Tanzania, Mwanariadha wa Tanzania Alphonce Simbu alikuwa akimaliza mbio za heshima za Marathoni jijini Rio de Janeiro, Brazili akishika nafasi ya tano. Wakati mwingine yanakwenda kasi ndani ya saa chache tu kabla au baada ya kuzama kwa jua.

Ilikuwa jioni ya mafanikio kwa Tanzania. Juzi usiku ungeweza kuchagua habari ya kukupa tabasamu katika hizi tatu. Huwa inatokea mara chache sana katika maisha ya Mtanzania.

Unadhani mafanikio haya yalipangwa? Hapana. Hili la Serengeti Boys linaweza kuwa labda  lilipangwa kwa sababu vijana hawa ni wadogo na ndio kwanza wamekusanywa. Chini ya Kim Poulsen sina hofu sana. Jamaa ni kocha maridadi na anaufahamu mpira. Nilishangaa Rais Jamal Malinzi alipomfukuza baada ya kuingia madarakani. Alichanganya soka na siasa. Shukrani alijirudi. Katika hili alifanya uungwana.

Hili la Mbwana Samatta hatukulipanga. Mtoto mmoja wa Kitanzania kutoka Mbagala alizaliwa na akili ya kipekee na amejifikisha alipofika. Watu wachache sana walimsaidia, lakini zaidi alijisaidia mwenyewe. Kama kila mtu huwa anasaidiwa, mbona Samatta yupo peke yake Ulaya?.

Timu yake ya mtaani aliyokulia haikuwa na uwanja wowote wa kisasa wala vifaa vya maana. Alijisaidia zaidi. Labda shukrani kubwa unayoweza kuitoa ni kwa viongozi wa Simba kukubali dau la kumuuza kwenda TP Mazembe wakati alipohitajika. Wengine huwa wanakataa.

Vinginevyo, kama tungeweka mfumo madhubuti kwa vijana wetu, Samatta angeweza kwenda Ulaya mapema tangu akiwa na miaka 18. Hata hivyo nani alikwambia timu zetu zinajiendesha kibiashara na zinaangalia biashara hii kwa mapana zaidi? Hakuna.

Kama unabisha la Samatta, basi jifunze kwa hawa hawa Serengeti Boys. Ingekuwa Ulaya klabu kubwa zingekuwa zimevamia kambi ya Serengeti Boys zikigombania kuwanunua na kuwalea vijana hao. Hapa Tanzania, nani anajali? Labda Jamal Bayser ndio ana tabia ya kuwanunua wachezaji wa aina hii na baadaye anawauzia Simba na Yanga.

Kama ilivyo kwa Samatta ndivyo ilivyo kwa Simbu. Ameshika nafasi ya tano Olimpiki kila mtu anajifanya kumjua kwa sasa. Nani anajua alikuwa anafanyia mazoezi wapi? Kuna miaka ya 1970 au 1980 wakati akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa na Suleiman Nyambui wakishindana na Wakenya na Waethiopia. Unadhani vipaji vile vimeisha? Vipo vingi.

Kama Sumbu angeandaliwa mapema miaka 10 nyuma, leo angeshinda Olimpiki. Leo wakiletwa wapinzani wake wa mbio za juzi waangalie sehemu anazofanyia mazoezi watashangaa kwanini alishika nafasi ya tano.

Wenzake wanafanya mazoezi katika bonde la Ufa kule Kenya. Wanakimbia katika milima ya Eldoret. Yeye alikuwa anakimbia wapi? Vipi kama tungekuwa na kundi kubwa la watu wa aina yake ambalo limeandaliwa Kisayansi miaka 10 iliyopita?

Sio yeye tu. Kuna mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Aurora anaitwa Hilal. Katika kundi lake la kuogelea aliongoza, ingawa alitumia sekunde nyingi zaidi na hakuweza kwenda mbele zaidi. Jiulize, Tanzania kuna mabwawa mangapi ya kuogelea yenye hadhi ya Olimpiki ambayo yalimuandaa kushinda walau katika kundi lake?

Jioni ya juzi ilikuwa inaendelea kutufungua macho kuwa bado Tanzania kuna vipaji vingi. Tatizo hatuna maandalizi. Kwanini hatuna maandalizi? Kwa sababu hatujafanya michezo kuwa maisha. Sehemu za wazi mafisadi waligawana. Sehemu nyingine zimefanywa kuwa gereji. Watoto watacheza wapi?

Sehemu ambayo aliwahi kuzaliwa Sunday Manara, Filbert Bayi, Nyambui, Rashid Matumla haiwezekani isizalishe tena watu wa aina hiyo. Sio rahisi kupoteza vizalia kama watu wanavyodhani. Watu wapo isipokuwa hatujali michezo.

Tukipanga mikakati tunaweza kurudi tena kama zamani. Jiulize, wenzetu washaanza kujiandaa na Olimpiki ijayo, sisi tutaanza kujiandaa lini? Kuna sehemu tumekosea na lazima tutengeneze mkakati wa kitaifa kurudi kama zamani. Inawezekana.