INAWEZEKANA: Barca wana habati, Real Madrid wameanza vibaya

Muktasari:

Timu hiyo iliuza mmoja ya wachezaji bora kabisa duniani, Neymar, kwenda PSG

MSOMAJI, kati ya vilabu vikubwa zaidi barani Ulaya naamini kwamba, Barcelona ndio walikuwa na dirisha baya zaidi la uhamisho mwaka huu. Timu hiyo iliuza mmoja ya wachezaji bora kabisa duniani, Neymar, kwenda PSG. Pia walishindwa kusajili mchezaji mwenye uwezo wa kuboresha safu yao ya kati.

Hivyo, wengi wameshangaa kwamba Barcelona wameuanza msimu wao vizuri sana katika Ligi Kuu ya Hispania. Mpaka sasa timu hiyo haijafungwa na wikiendi hii walitoka sare kwa mara ya kwanza msimu huu wakicheza dhidi ya wapinzani wao wakubwa Atletico Madrid.

Real Madrid ni mabingwa wa Hispania na pia ni wabingwa wa Ulaya na bado wana kikosi bora barani Ulaya katika karatasi. Lakini, timu hiyo ilianza Ligi Kuu ya Hispania vibaya sana msimu huu. Katika mechi zao za awali walipoteza mechi na walitoka sare dhidi ya vilabu vidogo kama Real Betis na Levante. Na hivi sasa wameshika nafasi ya pili wakiwa pointi tano nyuma ya Barcelona.

Tofauti ya pointi tano ni tofauti kubwa katika Ligi Kuu ya Hispania kwa kuwa Barcelona na Real Madrid wanapoteza mechi chache sana katika msimu. Hata hivyo naamini kwamba Barcelona wapo katika hatari ya kupoteza nafasi yao kubwa ya kushinda Ligi Kuu.

Kwa mtazamo wangu Lionel Messi ameficha mapungufu ya Barcelona msimu huu kutokana na kuwa katika formu ya hatari sana. Mchezaji huyu ameshafunga magoli kumi na moja katika mechi nane. Lakini, nyuma ya mchezaji huyu hakuna wachezaji wengi wanaoibeba Barcelona. Luis Suarez mpaka sasa amefunga magoli matatu tu katika Ligi Kuu na pia wachezaji kama Iniesta na Raktic wameshindwa kutengeneza na kupiga pasi nyingi za kufunga magoli.

Kama kutakuwa na wakati ambao Messi hata kuwa katika hali nzuri kimpira msimu huu basi Barcelona kwa kweli watakuwa katika hali mbaya. Ni kweli kwamba Barcelona bado hawajafungwa lakini mpaka sasa Atletico Madrid ni mpinzani pekee wa maana ambaye Barcelona imekutana naye. Washabiki wengi wa Barcelona waliridhika kutoka sare na Atletico Madrid kutokana na Atletico kutawala mchezo kwa muda mrefu na kufunga bao la kwanza. Lakini, zamani Barcelona hawangeridhika kutoka sare na timu yoyote katika La Liga na washabiki wa timu hiyo wanajua kwamba timu yao ina mapungufu makubwa katika baadhi ya safu.

Mwanzoni mwa msimu huu Barcelona walifungwa katika mechi mbili mfululizo na Real Madrid katika kombe la ngao. Katika mechi hizi mbili Real Madrid walitawala mchezo na ilikuwa wazi kwamba wana kikosi bora kuliko Barcelona. Bila shaka Barcelona wana bahati kwamba Real Madrid wameuanza msimu vibaya lakini kama wachezaji wengine nyuma ya Messi wataendelea kutokuwa katika hali nzuri kimpira basi Real Madrid watakuwa na nafasi kubwa ya kuziba pengo lao na Barcelona kwa kufunga timu hiyo katika mechi mbili katika Ligi Kuu.

Hivyo, siamini kwamba Barcelona wana nafasi kubwa ya kumaliza msimu huu katika nafasi ya kwanza.