NINACHOKIAMINI: Arsenal, Chelsea zinavyotoa elimu kwa Simba, Yanga

Muktasari:

Hivi unapoona Mahakama Kuu ya Kenya imetengua matokeo ya Uchaguzi wa Rais unadhani ni kitu kidogo. Tulishangaa siku ya kwanza tu, lakini sasa tunaona ni kawaida.

KUNA mambo fulani yakitokea katika nchi nyingine tunayaona ya kawaida, lakini yakitokea nchini kwetu tunashangaa au hata kuyakataa.

Hivi unapoona Mahakama Kuu ya Kenya imetengua matokeo ya Uchaguzi wa Rais unadhani ni kitu kidogo. Tulishangaa siku ya kwanza tu, lakini sasa tunaona ni kawaida.

Jambo kubwa ambalo tunalisahau ni kuwa, tunaishi katika dunia ambayo sasa imekuwa ni kijiji. Hutakiwi kwenda China kununua nguo, unaweza kununua ukiwa hapo ulipo kwa kutumia simu yako.

Licha ya kujua kuwa dunia ni kijiji, bado tumeshindwa kukubali kwamba kuna mambo yanayotokea katika nchi za watu wengine yanaweza pia kutokea Tanzania.

Unapoona mafuriko katika nchi za Asia yakiua maelfu kwa maelfu ya watu usidhani watu hao hawastahili kuishi, wala usidhani sisi hatuwezi kupata majanga kama hayo.

Tunachotakiwa kufanya ni pale tunapoona majanga au matatizo katika nchi za wenzetu tuwe tunajifunza na kujiandaa, ipo siku mambo kama hayo yatajitokeza na kwetu.

Tumekuwa tunayashuhudia mambo mengi yakitokea nchi za nje, lakini tumekosea jambo moja, hatupendi kujifunza wala kukiri kuwa yanaweza kutokea katika mazingira yetu pia.

Unapoona Crystal Palace inaifunga Chelsea si jambo la kawaida. Unapaswa kujiuliza maswali zaidi ya elfu moja halafu baadaye uje na jibu kuwa ‘ndio mpira’.

Timu ambayo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi ikiwa haina pointi yoyote baada ya kupoteza mechi zote saba ikaibuka na kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England.

Crystal Palace ilikuwa imepoteza mechi zote saba za mwanzo, lakini imeibuka Jumamosi na kuwafunga mabingwa watetezi Chelsea kwa mabao 2-1.

Tunapoona mambo kama haya, tunaona ni ya kawaida na yanakwisha hivyo hivyo, hatuamini kuwa yanaweza kutokea Tanzania.

Tunapoona Arsenal ikifungwa mabao 2-1 kutoka kwa Watford tunashangaa kidogo, halafu kuanzia siku ya pili tunagundua kuwa ni jambo la kawaida.

Tatizo langu ni kuwa tunaamini kuwa mambo hayo hayapaswi kutokea kwenye ardhi yetu ila yanapaswa kutokea huko huko kwa wazungu. Itakuwaje iwapo Ndanda ikiifunga Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Itakuwaje siku Njombe Mji ikiifunga Yanga katika mechi hizo. Mashabiki hawataelewa, viongozi hawawezi kuelewa, vyombo vya habari haviwezi kuelewa na hatimaye makocha wa Simba na Yanga wataonekana hawafai.

Nimewahi kuandika hapa kuwa mashabiki wa Simba wasije kushangaa kuona timu yao haichukui ubingwa msimu huu. Sijasema haitachukua, ila isipochukua wasije kumlaumu mtu yeyote wala kushangaa.

Uzuri wa dunia kuwa kijiji ni kwamba tunajifunza katika nchi zilizoendelea na mambo ambayo yanatokea katika dunia ya kwanza, tunapaswa kujifunza na kujiandaa kuwa ipo siku yatatokea na kwetu.

Nani alijua kuwa Chelsea ingepoteza mchezo, nani alijua kuwa Arsenal ingefungwa wikiendi hii? Mbaya zaidi timu ambazo zimewatuliza vigogo hao ni za kawaida kabisa.

Hii inataka kutwambia nini, tuwaache makocha Joseph Omog na George Lwandamina wafanye kazi zao bila kuwapiga presha ambazo badala ya kusaidia timu zao zinawafanya wawe na wakati mgumu wa kufanya uamuzi.

Simba imetoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar. Kuna watu wanaweza kumlaumu Omog, lakini wanapaswa kukumbuka kuwa Mtibwa ni timu kubwa na ipo juu katika msimamo wa ligi.

Wakumbuke kuwa Crystal Palace inashika nafasi ya mwisho Ligi Kuu England na imeifunga Chelsea. Tuwe tunajifunza.