‘Passolig’ inavunja utamaduni wa soka nchini Uturuki-1

Muktasari:

Ni Kasimpasa, Besiktas, Fenerbache, na Galatasaray. Inafahamika kwamba Ligi ya Uturuki ni ligi ambayo washabiki wake wanajaa uwanjani na wanashabikia timu zao kwa nguvu kubwa.

MSOMAJI, naandika nikiwa Istanbul, Uturuki. Istanbul ni mji wenye utamaduni mkubwa wa soka au mpira wa miguu. Katika mji huu kuna klabu nne ambazo zinacheza katika Ligi Kuu Uturuki.

Ni Kasimpasa, Besiktas, Fenerbache, na Galatasaray. Inafahamika kwamba Ligi ya Uturuki ni ligi ambayo washabiki wake wanajaa uwanjani na wanashabikia timu zao kwa nguvu kubwa.

Mwaka 2013 mashabiki wa Galatasaray walitajwa katika kitabu cha “Guiness world record” kuwa mashabiki wa mpira wanaotoa sauti nyingi zaidi katika mechi za nyumbani.

Lakini, msimu huu kumekuwa na mashabiki wachache sana katika majukwaa ya Turk Telecom Arena ambao ni uwanja wa nyumbani wa Galatasaray. Mwezi mmoja uliopita Galatasaray walicheza mechi ya nyumbani dhidi ya Fenerbache. Galatasaray na Fenerbache ni maadui wakubwa kimpira kihistoria.

Huwa tiketi ya mechi hiyo zikitoka tu zinamalizika katika kipindi kisichozidi saa mbili!

Uwanja wa nyumbani wa Galatasaray una uwezo wa kuchukua mashabiki elfu hamsini. Lakini, katika mechi ya Galatasaray dhidi ya Fenerbache kulikuwa na mashabiki 37000 tu!

Nikiwa hapa Istanbul nimepata nafasi ya kuzungumza na shabiki mmoja wa Fenerbache. Amenielezea kwamba mashabiki wengi wa mpira nchini Uturuki wameacha kwenda uwanjani kutazama timu zao kutokana na mfumo mpya wa kununua tiketi wenye jina la “Passolig”.

“Passolig” ilianzishwa mwezi Aprili mwaka huu. Katika mfumo huu, kila shabiki ambaye anataka kununua tiketi ya mpira anahitaji kuwa na kadi ya Passolig. Kupata kadi za Passolig mashabiki wanahitaji kujisajili katika mtandao wa kampuni hiyo. Na pia wanahitaji kulipa Turkish Lira thelathini ambayo ni sawa na Shilingi za Kitanzania elfu ishirini na tatu.

Wakati nikizungumza na shabiki wa Fenerbache aliyeniambia anaitwa Thabit ananielezea kwamba Kampuni ya Passolig inamilikiwa na benki yenye jina la “Aktif Bank”.

Benki hii inamilikiwa na mume wa binti wa Rais Erdogan wa Uturuki. “Mashabiki wengi wa mpira hawampendi rais Erdogan na tunaamini kwamba mfumo huu wa kununua tiketi ni ufisadi ambao unaisaidia familia yake. Na kwa hiyo wengi wetu hatutanunua tiketi za mpira mpaka chama cha soka kirudishe mfumo wa zamani,” anasema Thabit.

Chama cha soka pamoja na Serikali ya Uturuki wameeleza kwamba wameweka mfumo mpya wa kununua tiketi kwa ajili ya usalama. Kwa miaka mingi kumetokea ugomvi katika majukwaa ya viwanja vya mpira nchini Uturuki.

Mashabiki wakijisajili na Passolig wanahitaji kutoa taarifa nyingi. Kwa mfano, wanahitaji kutoa namba zao ya hati za kusafiria na kuonyesha mahali wanapoishi.

Chama cha soka Uturuki kinaamini kwamba taarifa hizo zitawasaidia kutambua mashabiki wanaoanzisha ugomvi.

Lakini Thabit ananielezea kwamba chama cha soka nchini Uturuki hakina nia nzuri.

Makala hii itaendelea wiki iyayo...