INAWEZEKANA : Iceland watapokelewa kishujaa nyumbani

Muktasari:

  • Iceland ni nchi yenye raia wasiozidi 300,000. Ni nchi ambayo haijawahi kushiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa kabla ya Euro 2016. Ni timu iliyoshangaza mashabiki wengi wa soka katika kila kona ulimwenguni.

MSOMAJI, Iceland imetolewa katika michuano ya Euro 2016. Imetolewa na wenyeji Ufaransa kwa kufungwa mabao 5-2. Hawakufa kizembe. Ingawa hatutaiona Iceland ikicheza nusu fainali wiki hii, lakini timu hiyo itakuwa imeridhika na mafanikio makubwa waliyoyapata katika ushiriki wa michuano ya Euro 2016.

Iceland ni nchi yenye raia wasiozidi 300,000. Ni nchi ambayo haijawahi kushiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa kabla ya Euro 2016. Ni timu iliyoshangaza mashabiki wengi wa soka katika kila kona ulimwenguni.

Wengi bado wanaiota na ni dhahiri kwenye michuano hii imejinyakulia mashabiki wengi, ambao awali hawakujua kwenye ramani ya soka.

Nikiwa nimeifuatilia timu hiyo ya Iceland ikifanya makubwa pale Ufaransa, ni kama vile nimesoma hadithi ya kusadikika.

Kuna Waingereza ambao mpaka leo hii hawawezi kuamini kwamba timu yao, yenye nyota kama kina Wayne Rooney, Harry Kane na Chris Smalling imetolewa na Iceland. Mpaka sasa Waingereza wanaumia baada ya kipigo kutoka kwa kikosi hicho kwani, wangetamani kuona wanafungwa na Ufaransa ama timu nyingine isingewauma sana. Wanaona wamedharaulika na sasa wanataka kikosi chao kunolewa na kocha mgeni.

Timu ambayo inawategemea wachezaji kama Saevarsson, Arnason na Kristinsson ambao wote wanacheza katika Ligi Kuu ya Sweden.

Lakini hadithi hii ya kusadikika haikuisha vizuri. Iceland ilipambana kiume mbele ya wenyeji Ufaransa, lakini wakaishia kulala kwa mabao 5-2.

Kikawaida kufungwa mabao matano ni aibu kubwa kwa timu yoyote, lakini kwa Iceland sio timu ya kawaida. Baada ya kutolewa na Ufaransa, mashabiki wa Iceland waliendelea kuishangilia timu yao kwa shangwe na nguvu nyingi kana kwamba, imebeba ubingwa.

Ndoto ya mashabiki wa Iceland kabla michuano hii ya Euro ilikuwa kuiona timu yao ikivuka hatua ya kwanza, ikitokea kwenye kundi ngumu lenye timu za Austria, Hungary na Ureno.

Wachezaji wa Iceland walifanya zaidi ya kutimiza ndoto ya mashabiki wao. Walifuzu makundi hadi 16 Bora na kuvuka pia kutinga robo fainali, huku ikishiriki katika michuano hiyo ya Euro kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Kwa mtazamo wangu, siri kubwa ya timu ya Iceland ni kocha wao, Lars Lagerback. Kocha huyo mwenye uraia wa Sweden ni mwanaharakati na kwa kutumia soka la kujihami sana na aliweza kuipeleka timu yake mpaka robo fainali.

Kocha Lagerback anapendwa sana na wananchi wa Iceland. Wiki tatu zilizopita uchaguzi mkuu ulifanyika nchini Iceland wenye lengo la kusaka rais mpya. Na baadhi ya wananchi wa Iceland waliamua kumpigia kura Lagerback, ingawa kocha huyu ana uraia wa Kiswidi!

Bila shaka wananchi wa Iceland wangependa kumuona Lagerback akiendelea kuifundisha timu yao. Lakini kocha huyu alitangaza kabla michuano hii ya Euro kwamba, hataendelea kuifundisha Iceland baada ya mashindano haya kufikia mwisho.

Lagerback na Iceland wameonyesha kwamba timu na nchi ndogo pia zina uwezo wa kupata mafanikio makubwa kimpira. Na bila shaka Lagerback na timu yake watapokelewa kama mashujaa wakirudi Reykjavik, mji mkuu wa Iceland.

Kwa sababu wamefanya kile ambacho hakikutarajiwa hata na raia hao achana na mashabiki wengine wa soka duniani.