MTU WA PWANI: Hivi Olunga na Aishi Manula wanaishi dunia moja?

NI nadra sana kwa mwanadamu kufanikiwa kutokana na juhudi za mtu mwingine. Kufanikiwa au kufeli kwa mwanadamu kwa asilimia kubwa huchangiwa na mipangilio na juhudi zake binafsi.

Nidhamu ya maisha na kujituma mara zote ndio imekuwa siri kubwa ya mafanikio kwa mwanadamu na siku zote huwa hakuna njia ya mkato katika kuyafikia mafanikio katika jambo lolote lile maishani.

Katika dunia ya sasa ya kibepari, njia ya kuyafikia mafanikio huwa rahisi kwa yule aliyejiwekea misingi na malengo na kuyafuata na kinyume chake, ni kuwa hakuna mafanikio kwa yule anayeishi bila kujiwekea malengo ya kufika mbali.

Hivi karibuni, mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Michael Olunga aliungana na mastaa mbalimbali wa soka duniani wanaomiminika katika Ligi Kuu ya China baada ya kujiunga na Klabu ya Guizhou Zhicheng.

Olunga amejiunga na timu hiyo akitokea IF Djurgardens inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden kwa ada ya Pauni 3.4 milioni ambazo ni sawa na Sh9.7 bilioni za Kitanzania na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyenunuliwa kwa pesa nyingi nchini Sweden.

Mshambuliaji huyo kabla ya kujiunga na IF Djurgardens, aliichezea kwa mafanikio makubwa Klabu ya Gor Mahia ya Kenya na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa nchi hiyo mwaka 2015 ambao pia yeye alikuwa mchezaji bora na mfungaji bora.

Ikumbukwe, mwaka huo pia, Olunga ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Kagame ambayo ilifanyika Tanzania baada ya kupachika mabao matano, ingawa Gor Mahia ilishindwa kutwaa taji mbele ya Azam FC.

Uhamisho wa Olunga kwenda China umenifanya nimkumbuke kipa wa Azam FC, Aishi Manula ambaye alikuwa ni miongoni mwa nyota waliotamba katika mashindano ya Kagame mwaka 2015.

Licha ya kutopata tuzo ya Kipa Bora wa michuano hiyo ya Kagame, Manula hakuruhusu bao lolote kwenye nyavu zake kwenye muda wa kawaida wa mchezo kwenye mashindano hayo, akiiwezesha Azam kutwaa ubingwa wa kwanza wa kombe hilo katika historia yake.

Ni mwaka mmoja na nusu tu umepita tangu Olunga na Manula watambe kwenye Kagame lakini maisha ya kisoka kwa wawili hao tayari yameshapishana kwa kiwango kikubwa na hakuonekani tena dalili ya kuwa katika daraja moja.

Manula bado anaendelea kuwepo pale Chamazi kwa matajiri wa soka la Bongo, Azam wakati Olunga tayari ameshakula dau la usajili kwa timu mbili tofauti za Djurgadens na hiyo Guizhou Zhicheng.

Wengi wanaweza kujiuliza, iweje Manula hajaweza kupiga hatua hata moja kutoka pale alipokuwa wakati Olunga amefanikiwa kupiga hatua mbili zaidi mbele?

Kuna majibu mengi ambayo yanaweza kupatikana kwa swali hilo lakini jibu sahihi la kwa nini Manula bado anaendelea kuwepo pale kwenye hosteli za kifahali pale Chamazi, analo yeye mwenyewe na Mungu wake.

Pengine nafasi za kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi zimekuja, lakini klabu yake inamzuia kwa kutambua kuwa itapata wakati mgumu kuziba pengo lake kama ambavyo klabu nyingi za Tanzania zimezoea kufanya.

Kama ni hivyo, itashangaza kidogo kwa sababu ni haohao Azam ambao hivi juzi tu wamemruhusu Farid Mussa kwenda Hispania kuichezea CD Tennerife inayoshiliki Ligi Daraja la Pili.

Labda hakuna ofa yoyote iliyokuja mezani kwa ajili ya kumtaka Aishi, lakini je amejaribu hata kwenda nje ya nchi mara moja kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa?

Pia inawezekana yeye mwenyewe Manula hayuko tayari na wala hana mpango wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na anaamini kuichezea Azam kunamtosha katika maisha yake yake ya soka.

Kama hilo la mwisho litakuwa na ukweli, Manula atakuwa hakitendei haki kipaji chake maridhawa cha kulinda lango ambalo mwenyezi Mungu amemjalia.

Yeye ni miongoni mwa makipa bora katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa sasa, hivyo pasipo shaka yoyote, iwapo anaamua kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, hawezi kukosa nafasi timu ya kuichezea.

Aishi ni mfano tu wa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wamebahatika kupata vipaji vikubwa vya kucheza soka kuliko wengi wanaocheza kwenye ligi kubwa duniani, lakini mwisho wa siku vipawa hivyo vinaishia ndani ya ardhi ya Tanzania.

Wakati Olunga alipokuja kucheza Kagame, wengi hawakutegemea kama straika huyo angeweza kuwa staa mkubwa duniani ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, aliweka malengo na akaitumia vizuri miguu yake ambayo leo hii imemfanya aukaribie utajiri kutokana na noti za Wachina.

Muda umefika sasa kwa wachezaji wetu kutojidharau na kujituma kwa jasho na damu ili malengo wanayojiwekea, yasiishie kuwa ndoto, bali uhalisia kama ilivyotokea kwa Olunga.

Olunga sio malaika kwamba anaishi katika mbingu ambayo Manula na nyota wenzake wa soka la Kitanzania hawawezi kuifikia.

Wote wanaishi katika dunia moja, lakini utofauti huletwa na aina ya maisha ambayo kila mmoja anaishi kulingana na malengo aliyojiwekea na juhudi zake binafsi.