Kocha Rollers aifananisha Yanga mlo wa jioni

Muktasari:

Timu hiyo ya Botswana imepania kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza

Dar es Salaam. Kocha wa Township Rollers, Nikola Kavazovic amesema baada ya kuua sungura sasa anaandaa chakula cha jioni.

Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya kuulizwa amejianda vipi kwa mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Yanga utakaofanyika kati ya Machi 6 hadi 7 na mshindi wa mechi hizo mbili atafuzu kwa hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa ya klabu barani Afrika.

Akizungumza na tovuti ya klabu hiyo baada ya kuwasili nchini humo wakitokea Sudan alipofanikiwa kuiondoa Al-Merrikh kwa jumla ya mabao 4-2, Kavazovic alisema sasa anajianda vizuri zaidi kwa mchezo dhidi ya Yanga ili kutimiza lengo lake.

Mechi ijayo ya vijana wa Kavazovic ni dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Yanga ambao wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhid ya St Louis ya Shelisheli.

“Sikutaka kuifikiria Yanga kabla ya kumaliza mechi ya Al-Merrikh, kwa sababu uwezi kuandaa chakula cha jioni wakati Sungura bado yupo porini, na sasa tumeshamua sungura, tunaweza kuandaa chakula chetu.

“Tumeandaa video na taarifa mbalimbali kuhusu Yanga na tutafanya kila kitu kuhakikisha tunajiandaa vizuri kwa mchezo huo. Ligi ya Mabingwa ndiyo lengo letu la kwanza msimu huu tutafanya kila kitu kujiandaa vizuri zaidi ya ilivyokuwa kwa Al-Merrikh na kama tukifanikiwa kucheza hatua ya makundi itakuwa vizuri zaidi,” alisema Kavazovic.

Kocha huyo alijisifu kwa mbinu yake ya kujilinda ilivyofanikiwa kuwamaliza Al-Merrikh katika mchezo wa marudiano pamoja na Wasudan hao kutawala mchezo huo.

“Kupaki basi mbele ya goli ndiyo sifa ya Jose Mourinho, lakini kuna namna nyingi za kufanya hivyo.

“Falsafa yangu ya kupaki basi ni pamoja na kucheza soka la kushambulia, na kutegeneza nafasi za kufunga kupitia viungo wetu Boy na Tshireletso wenye uwezo wa kupiga pasi za kumaliza mchezo kwa (Motsholetsi) Sikele, Moluba (Edwin Moalosi), na Juluka (Mogorosi),” alisema Kavazovic.