Kocha Katwila atoa utetezi Mtibwa Sugar kuchemka

Muktasari:

  • Katwila aliyewahi kutamba na kikosi hicho kabla ya kuwa kocha, alisema timu yao itaendelea kuwa imara msimu huu licha ya kuibuka kwa changamoto hizo.

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amezidi kujitetea kuwa kufanya vibaya kwa timu yake katika siku za karibuni kumetokana na kuongezeka kwa ushindani miongoni timu za Ligi Kuu Bara na si kwamba timu yake imeshuka kiwango.

Katwila aliyewahi kutamba na kikosi hicho kabla ya kuwa kocha, alisema timu yao itaendelea kuwa imara msimu huu licha ya kuibuka kwa changamoto hizo.

Mtibwa imekuwa na wakati mgumu hivi karibuni ikifungwa mechi mbili na kutoka sare moja kwenye mechi zake tatu za mwisho.

“Wanaotubeza labda wanatawaliwa na ushabiki, soka linachezwa sehemu za wazi na si chumbani, kiufundi bado tupo vizuri,” alisema Katwila.

Katwila alisisitiza hawajakata tamaa ya kuwania moja ya nafasi tatu za juu, hivyo hawawezi kukatishwa tamaa na watu wanaona wao ni nguvu ya soda kwa kuwa na moto mechi za mwanzoni tu.