Kocha Al Masry tutasonga mbele

Muktasari:

  •  Mshindi wa mechi hizo mbili ataingia hatua atasonga katika hatua ya mtoano

Kocha wa Al Masry,Hossam Hassan amesema anamatumaini timu yake itashinda mechi yake dhidi ya Simba na kusonga mbele kwa raundi ijayo.

Hassan atakiongoza kikosi chake keshokutwa Jumatano kucheza mechi ya kwanza ya hatua ya 32 bira ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Green Buffaloes kwa jumla ya mabao 5-2 katika raundi ya awali.

 

“Tulistahili kushinda dhidi ya Green Buffaloes,” alisema kabla ya timu yake kuondoka Cairo kwa safari ya Tanzania.

“Wachezaji wangu walicheza katika kiwango cha juu, hiyo itatusaidia katika kutimiza lengo letu la kusonga mbele katika mashindano haya. Hatua hii itakuwa ngumu zaidi na tupo tayari kwa ajili ya hilo.”

Kocha huyo atamkosa Islam Serry aliyeumia hivi karibuni, lakini atakuwa na nyota wake wengine Abdallah El-Shamy, Aristide Bance, Saeed Mourad na Ahmed Gomaa.

Simba imefuzu kwa hatua hiyo baada ya kuitoa Gendarmerie Nationale ya Djibout kwa mabao 5-0. Miamba hiyo ya Tanzania katika mchezo wa kwanza ilifunga Gendarmerie Nationale 4-0 na marudiano ilishinda bao 1-0 nchini Djibouti.

“Tunawaheshimu Simba na tutacheza kwa ubora wetu dhidi yao. Naamini tutashinda na kusonga kwa hatua ijayo,” alisisitiza kocha huyo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba anatarajiwa kuongoza maelfu ya Wanasimba na Watanzania kuishangilia Simba kwenye mchezo huo utakaoanza saa kumi na mbili jioni.

Tizeba atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao utachezeshwa na Waamuzi toka nchini Afrika Kusini.

Mapema kesho saa tano asubuhi makocha Pierre Lechantre wa Simba na Hossam Hassan wa Al-Masry watazungumza na Wanahabari kwenye Hoteli ya Serena.