Klopp: Salah sawa ila kuna Messi

Muktasari:

Nyota huyo wa Misri mara kadhaa amekuwa akifananishwa na Messi kutokana na kiwango chake msimu huu

Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ameshindwa kusema kuwa Mohamed Salah ndiye mchezaji bora dunia kwa wanaotumia mguu wa kushoto akisema Lionel Messi hapaswi kusahauliwa katika kipengere hicho.

Salah amekuwa na msimu mzuri katika kikosi cha Liverpool, akiwa amefunga mabao 30, katika mashindano yote tangu alipowasili akitokea Roma.

Katika Ligi Kuu England amefunga mabao 22, kati ya hayo Salah amefunga 19 kwa mguu wa kushoto, mawili kwa mguu wa kulia na moja kwa kichwa.

Alipoulizwa kama nyota huyo wa Misri ndiye mchezaji bora wa mguu wa kushoto duniani, Klopp hakupendezwa sana, lakini alisema kuna Messi wa Barcelona unatakiwa kumtazama pia.

"Katika biashara? Dunia nzima? Lionel Messi, anatumia mguu wa kushoto, Lionel? Labda kama tutamuondoa katika orodha hiyo," alisema Mjerumani huyo.

"Lakini ndiyo, ni mchezaji bora duniani – lakini sivutiwi sana kuhusu suala hilo, lakini yeye ni mchezaji mzuri. Nafurahi jambo hilo.”