Kinda wa Yanga aanza kuonekana kwenye runinga

Muktasari:

Mobby asema winga huyo ana kasi uwanjani na anapaswakuendelea kujituma kuanzia kwenye mazoezi na mechi ili aweze kupata muda mzuri wa kucheza.

Mwanza. Beki wa Kati wa Mwadui FC, Idd Mobby “Kiraka” amesema winga wa Yanga, Said Mussa akipewa nafasi Jangwani atakuwa mchezaji hatari nchini.

Mobby alisema alimuona kinda huyo katika mchezo wao na Yanga uliopigwa Jumatano iliyopita ambao Mussa aliingia dakika ya 50 akichukua nafasi ya Amissi Tambwe.

Alisema dakika 40 alizocheza winga huyo aliwapa taabu mabeki wa Mwadui endapo ataendelea kujituma na kucheza soka la kiwango hicho atakuwa mchezaji tishio katika siku zijazo.

“Hata ukiwauliza wachezaji wenzangu hasa mabeki watakwambia huyu Mussa alitusumbua japo tulimdhibiti alicheza muda mfupi, lakini kazi tuliipata kwasababu ana kipaji kikubwa,”alisema Mobby.

Mobby alisema winga huyo ana kasi uwanjani jambo ambalo alisema kinachotakiwa kwake ni  kuendelea kujituma kuanzia kwenye mazoezi hadi mechi ili aweze kupata muda mzuri wa kucheza.

“Mmoja wa wachezaji ambao kama akipewa nafasi na muda  atakuja kuwa bora, kikubwa kwake anatakiwa kujituma zaidi kuanzia kwenye mechi hadi mazoezini,” alisema beki huyo.