Kile Kiberenge cha URA sasa chanukia Jangwani

YANGA bado inahaha kusaka winga wa kuziba pengo la Simon Msuva aliyepo Morocco na sasa jicho la benchi la ufundi klabuni hapo limenasa kwa Mganda Nicholas Kagaba.

Winga teleza huyo wa URA aliyekuwa na timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mjini Unguja, hivi karibuni, anapigiwa hesabu na Yanga kutua Jangwani ili kukinukisha.

Mabingwa watetezi hao tayari walishamnasa kiungo fundi wa JKU  ya Zanzibar, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na sasa wameelekeza akili zao kwa nyota huyo wa Uganda anayeichezea pia timu ya taifa hilo ‘The Cranes’.

Kagaba amekiri kumvutia Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina na Msaidizi wake, Shadrack Nsajigwa, kwani walimdokeza wakati wa michuano ya Mapinduzi ambayo URA ilifika fainali na kupoteza mbele ya Azam kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Akizungumzia uwezekano wa kutua Yanga, Kagaba alisema: “Natamani siku moja nicheze pamoja na  Ibrahim Ajibu, mkataba wangu na URA, unaelekea ukingoni hivyo inawezekana kujiunga nao, kama watakuja,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussen Nyika, alisema kila kitu ambacho kinahusiana na usajili kinakwenda sawa na muda utakapofikia wataweka wazi.

“Nimeshamaliza usajili wa dirisha dogo na kuhusu dirisha kubwa bado muda upo mwingi, wakati ukifikia tutaeleza kila kitu kwani kamati inafanya kazi,” alisema Nyika.