Kikwete, Dalali wamzika Chama

Tuesday January 9 2018

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba waliwaongoza mamia ya waombelezaji katika maziko ya beki wa zamani wa Yanga, Athuman Juma Chama yaliyofanyika leo kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Chama aliyeichezea Yanga miaka ya 80, alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya kulazwa kwa takribani wiki mbili kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili akizusumbuliwa na maradhi ya kiharusi. Marehemu ameacha mke na watoto wawili.

Wakizungumza baada ya mazishi hayo nyota wa zamani wa soka waliowahi kucheza na Chama wamemsifia kuwa alikuwa ni mchezaji mwenye nidhamu ya juu na ameacha pengo kubwa kwao.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Makumbi Juma ’Homa ya Jiji’ alisema  amesikitishwa  na kifo cha Chama kwani alimzoea baada ya kucheza naye kwa miaka 10.

Makumbi alisema "hakika tumepata pigo kumpoteza Chama, nimecheza naye kwa muda mrefu moja ya mambo ambayo nitayakumbuka kutoka kwake ni nidhamu aliyokuwa nayo."

Winga wa zamani wa Yanga, Charles Kilinda’Matata’ alisema  amepokea kwa masikitiko msiba huo  kwani Chama alikuwa ni  mmoja  wa  wachezaji  mahiri walioifanya kazi zao vema uwanjani

Zamoyoni Mogela alisema waasisi wa Simba na Yanga wameacha majengo na hawakusoma, vipi vijana wa sasa wameenda shule, lakini ni ngumu kupata mafanikio kwa sababu mpira umevamiwa."

Wadau wengine wa soka waliohudhulia mazishi hayo ni mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina na mwenyekiti wa kamati ya usajili Yanga, Hussein Nyika, Charles Mkwasa, Abed Mziba, Makumbi Juma’Homa ya Jiji’, Zamoyoni Mogela na Charles Kilinda.

 Athuman Chama Jogoo ni nani?

Ni mtoto wa kwanza kati ya watano kwenye familia yao, Chama alichezea timu mbalimbali kabla ya kujiunga na Pamba United ya Mwanza.

Chama alicheza Yanga kwa miaka zaidi ya 10, lakini wakati huo walicheza kwa mapenzi zaidi na walicheza kwa moyo ikilinganisha na wachezaji wa sasa.

Kikosi cha kwanza cha Yanga waliocheza na Chama miaka ya 1983 na 1985 ni; Joseph Fungo, Yusuf Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Athumani Juma Chama ‘Jogoo’, Isihaka Hassan Chuku, Juma Mukambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba ‘JJ Masiga’, Elisha John na Ali Mchumila.

Pia walikuwepo; Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omari Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengine wengi.

Apachikwa jina la Jogoo

Wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 1981, kulikuwa na mchezaji mmoja wa Harambee Stars ya Kenya, Sammy Onyango ‘Jogoo’. Alikuwa makini sana katika ngome.

Alikuwa na uwezo wa kukabiliana na washambuliaji mbalimbali hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Baada ya mashindano yale ya 1981 ambayo pia kulikuwa na mtu aliyekuwa akiitwa Ambroce Ayoi ‘Golden Boy’ wengi waliufananisha uwezo wa Sammy Onyango na Athumani Juma Chama na taratibu jina likafika kwa mwenyewe.

Chama na Mogella

Chama na Mogella…..Chama na Mogella. hii ni kumbukumbu ambayo Chama ameiacha kwenye soka la Tanzania ikiwazungumzia, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Zamoyoni Mogella na beki huyo wa Yanga (Chama).

Itakumbukwa Yanga walitishika na soka ya Mogella katika moja ya mechi za watani, ndipo waliamua kumwekea ulinzi mkali, wa Athumani Juma Chama ambaye aliambiwa popote anapokwenda Mogella awe naye.

Chama alifanya kazi yake, basi ikawa kazi moja, Chama na Mogella kiasi cha Mogella kuumia na kufanyiwa huduma ya kwanza, Mogella alifunga bandeji mfano wa ‘lumundi’ kichwani na kurudi uwanjani, hata hivyo Mogella hakutikisa nyavu siku hiyo.