Kesi ya Masogange yakwama

Muktasari:

  • Upande wa mashtaka umefikia hatua hiyo baada ya Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko, kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa wakili mwenzake, Reuben Simwanza, ndiye aliyeandaa mashahidi na kwamba ameshindwa kutokea kwa sababu ni mgonjwa.

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili, Agness Gerald ‘Masogange’, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuuonya upande wa utetezi kwa kushindwa kutoa ushahidi wao kwa mara ya tatu mfululizo.

Upande wa mashtaka umefikia hatua hiyo baada ya Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko, kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa wakili mwenzake, Reuben Simwanza, ndiye aliyeandaa mashahidi na kwamba ameshindwa kutokea kwa sababu ni mgonjwa.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Nkoko, alisema kutokana na hali hiyo, atahakikisha anaandaa mashahidi ili itakapotokea wakili mmoja hayupo, mwingine aendelee na shauri.

“Hatuna pingamizi na sababu zilizotolewa na upande wa utetezi, lakini tunaomba mahakama itambue kuwa ni mara ya tatu kwa upande wa utetezi unaahirisha kesi hii,” alidai Wakili wa Serikali Constantine Kakula.

“Mawakili wapo wengi lakini wanashindwa kuendelea kutoa ushahidi wao, basi kama hawawezi, waache mshitakiwa aendelee na kesi mwenyewe.”

Kutokana na hali hiyo, upande wa mashtaka umeomba ahirisho la mwisho kwa sababu kesi ni ya muda mrefu.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Masogange, ambaye ni maarufu kwenye kupamba video za nyimbo za wasanii, kesi yake ilianza katikati ya mwaka jana.