Mtibwa Sugar yasherekea sare Mbao

Monday February 12 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema anashukuru kupata pointi moja Kanda Ziwa.

Mtibwa Sugar imelazimisha suluhu na Mbao FC katika mchezo wake wa mwisho Kanda ya Ziwa yakiwa na matokeo mazuri kwa baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza mkoani Shinyanga, dhidi ya Stand United mabao 2-1, kabla ya kucharazwa tena na Mwadui FC mabao 3-1.

Kocha Katwila alisema  licha ya kuja kwa malengo ya kuchukua pointi tisa Kanda ya Ziwa na kugonga mwamba, wanashukuru kwa pointi moja kwani kwa sasa Ligi imekuwa ngumu.

Alisema vijana wake walionyesha ushindani, lakini kutokana na maandalizi ya timu pinzani kuhitaji pointi tatu, iliwasababishia kupoteza mechi mbili.

“Kila timu inapigana yenyewe kusaka ushindi, si nyumbani wala ugenini, kumbuka tupo mzunguko wa mwisho kwahiyo kila mmoja anakufa kishujaa kusaka pointi tatu”alisema Katwila.

Kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije alisema licha ya matokeo waliyoyapata, lakini hawakati tamaa na kwamba hawajiandai na mechi moja isipokuwa wanapambana na Ligi kwa ujumla.

“Ndio tumefika mechi ya 18, kwa maana bado ligi haijaisha, leo (juzi) tumepata pointi moja kwahiyo tunaelekeza nguvu mechi inayofuatia kuhakikisha tunashinda,”alisema Mrundi huyo.