Kambi ya ngumi Taifa, ni chai na chapati mbili tu unaambiwa

Muktasari:

Kambi hiyo inatia huruma kwani, mabondia wanashindia chai na chapati mbili tu licha ya mazoezi makali yanayoendelea.

UNAWEZA kucheka au kusikitika, ila ndio hali halisi ya mazingira katika kambi ya Taifa ya ngumi za ridhaa inayojiandaa na Michezo ya Madola. Kambi hiyo inatia huruma kwani, mabondia wanashindia chai na chapati mbili tu licha ya mazoezi makali yanayoendelea.

Kikosi cha mabondia 20 kinajifua katika mazingira magumu kwenye kambi hiyo inayoendelea Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mazoezi ya jana asubuhi, timu hiyo ililazimika kupokezana glovu pea nne huku makocha wa timu hiyo wakisema hiyo ni hali ya kawaida kwenye kikosi hicho kitakachokwenda kushiriki michezo hiyo itakayofanyika kati ya Aprili 5-14 nchini Australia

“Timu ya taifa ina glovu pea nne na mabegi mawili tena yaliyochakaa! Hii sio haki kwa mabondia ila makocha hatuna namna zaidi ya kuwatia moyo wachezaji,” alisema kocha wa timu hiyo, Jonas Mwakipesile.

Awali, timu hiyo ilikuwa ikiazima vifaa vya mazoezi, lakini waliokuwa wakiwaazimisha nao wamesitisha na sasa wanalazimika kufanya mazoezi kwa kupokezana vifaa vichache vilivyopo.

“Hivi katika hali ya kawaida tu, timu ya taifa inaweza kuwa na gloves pea nne? Tena inajiandaa na mashindano makubwa kama ya Madola, timu haina pad hata moja, wala ulingo na kuna wakati tunajiona kama tumetengwa,” alisema.

Chai kwa chapati

Nahodha wa timu hiyo, Suleiman Kidunda alisema kambi yao ya wazi inakosa huduma muhimu kama matibabu na dawa pale bondia anapoumia mazoezini na hata chakula ambacho ni muhimu kwao, ni shida.

“Mwanzoni kiongozi mmoja wa BFT alijitolea kutununulia chai na chapati mbili asubuhi, lakini tangu wiki iliyopita huduma hiyo haipo tena. Hata hivyo, hatujakata tamaa, tunaendelea kuonyesha uzalendo na tunaamini kuna siku Mungu atasikia kilio chetu,” alisema.

Uhakika wa medali ukoje?

Kidunda anasema uwezekano wa kushinda medali kwenye Madola utatokana na juhudi binafsi za bondia.

“Unajua ngumi ni mchezo binafsi, tunajiandaa japo ni kwenye mazingira magumu, ikitokea tumefika Australia kila kitu kitajulikana huko huko, lakini timu ina morali na hamasa ya kufanya vizuri,” alisema.

Hali halisi ya mazoezi

Mbali na kupokezana gloves pea nne, katika mazoezi hayo pia timu hiyo inajifua kwa kutumia tairi kuu kuu ambalo kocha mwingine wa timu hiyo, Said Omary ‘Gogopoa’ alisema linawasaidia kuwapa wepesi wa miguu.

“Hilo tairi sio kifaa rasmi cha mazoezi, lakini tumelazimika kulitumia kwa kuwa hatuna mbadala, tunahitaji pia mabondia wetu wafanye ‘sparing’ wakiwa ulingoni, lakini imeshindikana na badala yake wanafanyia sparing kwenye sakafu.

BFT WALONGA

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga alipoulizwa kuhusu changamoto hizo alijibu.

“Kwani vifaa vilivyokuwepo vimechakaa? walikuwa hawajaniambia ngoja nifuatilie, lakini awali timu ilikuwa na gloves za kutosha, ila nitalifuatilia suala hilo kwa karibu,” alisema Mashaga.