Kaitaba lazima pachimbike tu

Muktasari:

Timu hizo zinakutana zikiwa zimetoka kuchezea vichapo jijini Dar, Mwadui ikilala dhidi ya Azam kwa bao 1-0, huku Kagera ikinyooshwa na Yanga kwa 3-0.

MWADUI FC imechimba mkwara kwa wenyeji wao Kagera Sugar kuwa, isitarajie mteremko kwake kwani wanahitaji pointi tatu katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara leo Jumanne, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Timu hizo zinakutana zikiwa zimetoka kuchezea vichapo jijini Dar, Mwadui ikilala dhidi ya Azam kwa bao 1-0, huku Kagera ikinyooshwa na Yanga kwa 3-0.

Mpaka sasa Kagera imekusanya pointi 18 ikiwa nafasi ya 14, huku Mwadui ikiwa na alama 20 katika nafasi ya 12 kila moja ikicheza mechi 21 na Mwadui walisisitiza wanazitaka pointi tatu ili kujiondoa katika eneo la hatari ya kushuka daraja.

Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema amekiandaa vyema kikosi chake ili kupata ushindi, lakini hata kwa mechi nyingine anataka kushinda zote.

Alisema kikosi chake hakipo sehemu nzuri, hivyo ushindi wa leo ni muhimu katika vita ya kupambana kujinasua kutoka chini na kusema kuwa, wataingia uwanjani kwa tahadhari na umakini wa hali ya juu.

“Mchezo utakuwa mgumu kutokana na wenzetu kuhitaji pointi tatu, ila tumejipanga vizuri na hatutaki kupoteza tena mechi,” alisema Bizimungu.

Katika mchezo huo, Mwadui itawakosa viungo wake Abdallah Seseme na Awesu Awesu ambao ni majeruhi, ambapo Bizimungu atalazimika kufanya mabadiliko.