Kagera, Azam nguvu sawa

Monday February 12 2018

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Kagera Sugar imeshidwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbanibaada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Mecky Maxime licha ya kucheza katika kiwango bora muda wote wa mchezo ilishindwa kabisa kutumia nafasi nyingi za kufunga ilizopata na kujikuta ikiendeleza rekodi yao mbaya ya kutokapata ushindi katika michezo nane mfululizo msimu huu.

Kagera Sugar ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 49 kupitia kwa Juma Shemvuni akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Japhary Kibaya.

Dakika ya 53, Iddi Kipagwile aliisawazishia Azam baada ya kumpiga chenga  beki wa Kagera Sugar, Mwaita Gereza na kutumbukiza mpira nyavuni.

Kutokana na matokeo hayo Azam imeendelea kubaki nafasi ya tatu ikiwa na poiti 34 sawa na Yanga lakini mabingwa hao watetezi wako nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Kagera Sugar imepanda nafasi moja kwenye msimamo wa ligi hadi nafasi ya 15 baada ya kufikisha pointi 14.