Kabwili awagawa Mwameja, Manyika

Dar es Salaam. Kipigo mabao 2-1 ilichopata Yanga dhidi ya Township Rollers ya Botswana kimewaibua makipa nguli wa zamani waliowahi kutamba nchini.

Mohammed Mwameja, Peter Manyika na Mbwana Makata wamewachambua makipa wawili wa timu hiyo akiwemo kinda Ramadhani Kabwili na Youthe Rostand.

Kabwili na Rostand wameigawa Yanga kuhusu uwezo wa kulinda lango baada ya timu hiyo kujiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati kocha wa makipa Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’ akiweka ngumu kuzungumzia makipa hao, lakini Manyika alisema benchi la ufundi lilifanya kosa kumpanga Kabwili dhidi ya Rollers.

"Kabwili alitwishwa mzigo mzito katika mchezo na Township, mechi ilikuwa kubwa kupewa nafasi ya kudaka, pamoja na kwamba Yanga wanamlalamikia Rostand lakini haikupaswa kumuanzisha katika benchi,” alisema Manyika.

Manyika aliyewahi kuwika Yanga, Simba na Taifa Stars, alisema Rostand alistahili kucheza licha ya kufanya baadhi ya makosa.

Alisema makosa aliyofanya Rostand ni machache kuliko hatari alizookoa na Kabwili alipaswa kuanzia benchi kwa kuwa mchezo huo ulikuwa wa presha.

Naye Mwameja alisema Kabwili hakuwa na uzoefu wa michezo ya kimataifa ingawa ameonyesha kiwango bora, lakini anatakiwa kuongezewa mbinu za kiufundi.

"Kabwili kajitahidi kwa uwezo wake, kucheza mechi ya kimataifa ni kitu kingine na ligi yetu ni kitu kingine, anahitaji kuongezewa baadhi ya vitu ili afanye vizuri zaidi. Mechi ya marudiano anaweza kucheza kama ataandaliwa ingawa ni uamuzi wa benchi la ufundi, binafsi namuona kwa umri wake, uzoefu na mechi aliyocheza amejitahidi," alisema Mwameja.

Kwa upande wake Mbwana Makata alidokeza hashangai Yanga kumuanzisha kinda huyo katika mchezo huo kwa kuwa benchi la ufundi lilimuamini ingawa bado anahitaji kupewa uzoefu.