Jicho la ziada linahitajika mechi za mwisho

Tuesday May 9 2017

 

By MAONI YA MHARIRI

LIGI Kuu Bara inatarajiwa kufikia tamati Mei 20 mwaka huu, kuhitimisha msimu wa 2016-2017 ulioanza rasmi Agosti 20, mwaka jana. Ligi hiyo imesaliwa na mechi za raundi kama mbili tu kuhitimisha na kupatikana kwa bingwa mpya wa msimu, japo mbio za kuwania taji hilo zipo kwa watetezi Yanga na watani zao wa jadi Simba.

Wakati ligi hiyo ikienda ukingoni, tayari kumeibuka malalamiko kwa baadhi ya makocha na hata viongozi wa klabu katika mechi wanazoenda kucheza viwanja vya ugenini.

Inawezekana malalamiko yaliyotolewa huenda yametolewa kutokana na matokeo mabaya iliyopata timu zao, lakini bado haipaswi kupuuzwa.

Hakuna asiyejua jinsi ligi kwa sasa ilivyokuwa ngumu hasa katika vita ya timu zinazopambana kushuka daraja na ile ya ubingwa ambao hata hivyo imebaki kwa timu mbili tu za Simba na Yanga. Mechi inazozikutanisha timu zinazotaka kushuka daraja dhidi ya zile zilizopata nafasi ya kusalia kwa msimu ujao ndizo zenye lawama na hata kuwepo kwa hisia ya kufanyika kwa hila katika upangwaji matokeo.

Hatuwezi kukataa mambo hayo yanafanyika kwa sababu msimu uliopita katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yalitokea na timu kuadhibiwa.

Hivyo ni wajibu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na Kamati ya Mashindano ya TFF kufuatilia kwa ukaribu mechi hizi za lala salama, ili kuepusha malalamiko mengi zaidi wakati ligi yetu ikielekea kumalizika.

Mwishoni mwa wiki, tumemsikia Kocha wa Mwadui, Ali Bushir ‘Benitez’ alivyokuwa akilia na maamuzi mabovu dhidi ya wenyeji wao Majimaji, ambapo timu yake ikafungwa mabao 3-0.

Kocha huyo anakiri bao la tatu walilofungwa na Majimaji hawana tatizo nalo kama mabao mawili yaliyofungwa kabla ya mapumziko.

Inawezekana Bushir amelia hivyo kwa sababu tu ya aibu ya kufungwa kwa timu yake, lakini siyo mara nyingi kwa kocha huyo kulalamikia maamuzi. Sio Bushir tu, bali hata makocha wengine ambao huwa hawazungumzii maamuzi ya waamuzi katika mechi zao wanapoibuka na kulalamikia, ujue wameguswa kweli kweli.

Ndiyo, zipo timu ambazo kila mechi wao ni kulalamikia waamuzi, wapo viongozi hata timu yao ishinde bado huwalaumu waamuzi kwa kuwanyima ushindi mnono kwa sababu ni hulka yao kulalamika, lakini wapo wengine ni vigumu kuwasikia wakifanya hivyo. Wao wanaamini soka ni mchezo wenye matokeo matatu ya kufungwa, kufunga na kutoka sare na matokeo yoyote inayopata uwanjani, huamini ni kutokana na kile walichopanda kabla ya kushuka uwanjani na suala la waamuzi huwa wanalichukulia poa kwa kujua nao ni binadamu kama wao.

Hata hivyo, bado TPLB na TFF haipaswi kupuuza mechi za kufungia msimu, lazima izitupie macho kwa umakini kwa nia ya kutaka kuona timu zinazostahili kushinda zinashinda kihalali na zinazofungwa zipoteze mechi kwa matokeo ya uwanjani tu. Kadhalika ni vyema kukawa na uangalizi wa ziada katika mechi hizi kuepuka hila za upangwaji wa matokeo, kwani soka la Tanzania kwa sasa limekuwa na mambo yenye mashaka kutokana na baadhi ya viongozi kupenda kulazimisha matokeo.

Kama timu za FDL baadhi zikiwa zinamilikiwa na taasisi za kiserikali zimeweza kupanga matokeo, vipi kwa klabu za Ligi Kuu zenye viongozi wanaoishi kijanja mjini? Ni rahisi kufanya hila zao, ilimradi kuona yao yanafanikiwa na kulivuruga soka la Tanzania.