Jamani Bonny anaumwa, tuache masihara

Bonny alifikishwa hospitalini hapo Jumanne ya wiki hii, huku akishindwa kusimama, kuongea wala kula pekee yake

Muktasari:

  • Awali aligundulika anasumbuliwa na homa ya matumbo (typhoid) na vidonda vya tumbo, hivyo akawa anapata matibabu tu na kuendelea na shughuli zake.

KIUNGO fundi wa zamani  klabu ya Yanga na Taifa Stars, Geofrey Bonny ‘Ndanje’ hali yake kiafya ni mbaya na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Makandana-Rungwe.

Maneno rahisi ambayo unaweza kutumia kuelezea hali ya mchezaji huyo ambaye wakati fulani alikuwa akijitoa mhanga Yanga mpaka kucheza na plasta kichwani, ni kwamba hali ni mbaya na anahitaji msaada na uangalizi wa karibu sana wa wataalam wa afya na ndugu na marafiki.

Bonny alifikishwa hospitalini hapo Jumanne ya wiki hii, huku akishindwa kusimama, kuongea wala kula pekee yake na ndugu zake wakieleza kwamba hali ya kiuchumi kwake si nzuri hivyo anahitaji msaada kwa wasamaria wema kuwezesha matibabu yake.

Akizungumza na gazeti hili, hospitalini hapo pembeni ya kitanda cha mgonjwa huyo ambaye hawezi kufungua mdomo kuzungumza chochote, dada wa nyota huyo wa zamani, Neema Bonny alisema kaka yake alianza kuumwa miezi mitatu iliyopita na kipindi chote hicho alikuwa akipata matatibu madogo madogo na kupata nafuu, hivyo kuendelea na shughuli zake za kawaida.

“Leo (juzi) anaanza mwezi wa nne tangu aanze kuumwa, lakini awali aligundulika anasumbuliwa na homa ya matumbo (typhoid) na vidonda vya tumbo, hivyo akawa anapata matibabu tu na kuendelea na shughuli zake. “Muda mwingine alikuwa anafundisha timu moja hivi hapa Rungwe huku akiwa anasumbuliwa hivyo hivyo. Ila wiki  iliyopita ndiyo alianza kuzidiwa akilalamika miguu haina nguvu na kifua kubana,” alisema Neema.

Alisema kutokana na hali yake kubadilika zaidi, Jumanne ya wiki hii walimpeleka hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi ambapo alichukuliwa vipimo kwa kupigwa X-ray, lakini hadi juzi jioni walikuwa wamepokea picha ya X-ray bado kuambiwa majibu.

Alisema: “Kama unavyomuona anashindwa kuinuka, kuongea kwenyewe ni shida hata chakula ni hadi ashikiliwe ndio tunamnywesha uji na madaktari wamesema watakuja kutupatia majibu yatakayobaini ugonjwa unaomsumbua kaka yangu.”

Mke wa mchezaji huyo wa zamani, Suzan Mwakisale ambaye alidai alitengana na Bonny miaka kadhaa iliyopita, alisema alipigiwa simu na ndugu zake akiarifiwa kuwa mzazi mwenzie anaumwa na hali yake si nzuri hivyo aliomba ruhusu kazini kwake na kwenda kumuuguza.

Alisema kwa sasa wanasubiri majibu ya vipimo kutoka kwa madaktari ili kujua kama atahitajika kwenda hospitali kubwa zaidi ama la.

Alisema kutokana na hali inavyoonekana, mumewe anahitaji msaada zaidi ili kufanikisha matibabu yake.

Mchezaji huyo alitamba na Yanga iliyokuwa na mastaa kama Herry Morris, Shadrack Nsajigwa, Ivo Mapunda na Samson Mwamanda. Alitamba pia Prisons na Tukuyu Stars na hivi karibuni alikuwa Nepal akimalizia soka lake ingawa hapakuwa na mafanikio makubwa.