JKU yauvaa muziki wa Zesco Amaan

Muktasari:

Timu za Zanzibar hazina mafanikio katika mashindano ya klabu barani Afrika

Zanzibar. Mabingwa wa Zanzibar, JKU itakuwa na kibarua kizito mbele ya ZESCO kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mchezo huo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika utaanza saa 10:00 za jioni huku viingilio vya mchezo huo ni Sh 1000 na 500.

Akizungumzia mchezo huo kocha wa timu ya JKU, Ali Suleiman Mtuli alisema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo.

“Sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri kukabiliana na mchezo huu tunategemea kupata ushindi mnono katika mechi hii,” alisema Mtuli.

Kocha wa ZESCO FC, Tenant Chembo alisema JKU ni timu nzuri hatuwezi kuwadharau, lakini wamejipanga kuhakikisha tunashinda.

“Wapinzani wetu ni wazuri na hatuwezi kuwadharau, ila tumejipanga ili kuhakikisha tunaondoka na kurudi nyumbani tukiwa na ushindi, nakusubiri kwa ajili ya mechi ya marudio”, alisema Chembo.