JICHO LA MWEWE: Tshabalala, ataweza kurudi kuwa yuleyule?

Muktasari:

>> Sasa hivi hayupo vile sana. Aliumia katika pambano la fainali ya FA dhidi ya Mbao pale Dodoma. Hajarudi kuwa vile.

ALININONG’ONEZA mtu mmoja hivi majuzi kuwa anamuona beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ameshuka kiwango.

Na wengi kwa sasa wanaona hivyo. Hawamuoni kama amerudi katika kiwango kilekile ambacho amezoea kuwa nacho.  Nina ushabiki binafsi na Tshabalala. Nina mapenzi binafsi naye. Ndiye beki wa kushoto anayenivutia zaidi nchini. Anacheza soka maridadi. Anacheza tofauti na mabeki wengi nchini, hasa wale wa pembeni. Anatulia.

Sehemu ambayo mabeki wengi wa pembeni wangebutua, Tshabalala huwa habutui. Anatumia akili. Anataka kucheza soka kuanzia nyuma kama timu yake inaanza kutengeneza shambulizi kuanzia upande wake. Hapeleki mpira katikati wala mbele kwa harakaharaka.

Sasa hivi hayupo vile sana. Aliumia katika pambano la fainali ya FA dhidi ya Mbao pale Dodoma. Hajarudi kuwa vile. Anaweza kurudi kuwa vile lakini wakati mwingine historia zinatusuta pindi tunapoangalia matibabu ya wachezaji wa dunia ya tatu.

Hatutibiwi kifahari. Hatutibiwi madhubuti. Kwa mfano, kwa wazungu na wengineo tumeona matibabu yao na jinsi wanavyoweza kumrudisha mchezaji alivyokuwa. Kwetu inakuwa vigumu kiasi kwa sababu mbalimbali. Uwezo wetu wa kiuchumi upo chini na hatuwezi kuwa madhubuti.

Kuna matibabu ya aina mbili. Kuna matibabu ya kimwili na kuna matibabu ya kisaikolojia. Kwa mfano, huenda kwa sasa Tshabalala ameathirika kwa matibabu ya kisaikolojia. Labda hajapatiwa matibabu ya kisaikolojia. Anaamini kilichomtokea kinaweza kumtokea tena.

Mchezaji akifikia hatua hii, hachezi kwa kasi ileile. Anafikiria tukio lake linaweza kujirudia. Anajikuta ni mhanga wa hofu. Kuna watu wapo nyuma yake wakimhakikishia usalama wake kisaikolojia? Hili ndio tatizo kubwa katika matibabu ya kawaida ya Mtanzania.

Si kwa wanasoka tu, hata kwa binadamu wa kawaida wa nchi yetu wanapopata ajali huwa wanaishi na kivuli cha ajali wakiamini tukio linaweza kujirudia muda wowote.

Tshabalala kwa sasa hana kasi sana na hajiamini sana kama ilivyokuwa awali. Amepata matibabu ya kisaikolojia? Sio yeye tu, kuna wanasoka wengi wamepotea baada ya kushindwa kupata matibabu ya kisaikolojia. Wanapona vizuri tu lakini wanashindwa kumudu hisia za tatizo linaweza kujirudia tena. Hili ni tatizo kubwa na ndio maana timu zetu zinahitaji watu wa aina hii.

Pale kwa wazungu baada ya awamu ya kwanza ya matibabu wachezaji hupelekwa kwa wanasaikolojia kwa ajili ya kumaliza mchakato mzima wa matibabu. Wako wapi watu wa aina hii nchini? Hili ni swali la kujiuliza. Mabenchi ya ufundi ya kina Jose Mourinho huzungukwa na watu zaidi ya 20.  Wengine kati ya hawa ndio wanafanya kazi hizi.

Ukiachana na awamu hii, kuna awamu ya kwanza kabisa. Awamu ya matibabu yenyewe. Bila ya kuwakosea heshima madaktari wetu, lakini mashabiki wengi wa soka huwa tunajiuliza kama kuna uwezekano wa mchezaji wa Kitanzania kupona na kurudi uwanjani kama akivunjika mguu kama ilivyokuwa kwa Aaron Ramsey na Eduardo da Silva wa Arsenal.

Ni kweli mchezaji wa Kitanzania anaweza kuumia katika kiwango kilekile akarudi uwanjani?  Jaribu kujiuliza, vifaa ambavyo vinatumika kabla hajaondolewa uwanjani. Ni kweli anaweza asipate huduma zile lakini isiathiri lolote katika matibabu yake?  Inafikirisha sana. Baada ya hapo unakutana na malezi ya mchezaji baada ya ajali yake uwanjani. Jinsi anavyojilea, jinsi ambavyo klabu yake inamlea. Hapa ndipo kuna kichekesho kikubwa ndani yake na inazua hofu kama wachezaji wetu wanaoumia vibaya wanaweza kuwa fiti wakirudi uwanjani.  Kwa mfano, staa wa zamani wa Manchester United, Ryan Giggs aliwahi kumshauri staa wa zamani wa Liverpool enzi hizo, Michael Owen kuwa atalazimika kubadili aina ya gari analotembelea kama anataka kupona goti lake vema.

Leo tuna mchezaji aliyeumia goti lakini ambaye analazimika kutoka Dar es Salaam hadi Songea kwa basi kwa ajili ya kucheza mechi huku goti lake likiwa halijapona sawasawa. Kuna mchezaji anayeshauriwa kula aina fulani ya vyakula kwa ajili ya kupona vema lakini inakuwa shida kwake kufuata ratiba. Haya ni maisha ya soka letu ambayo yamepoteza vipaji vingi kila kukicha kuanzia timu kubwa hadi ndogo.

Haya mengi ya kisaikolojia na kitabibu ndio ambayo yalipita kichwani baada rafiki yangu mmoja kunikumbusha kuwa alikuwa haoni kama Tshabalala yupo vizuri tangu atoke katika majeraha yake. Ni kweli, sio yeye tu, bali hata kwa wanasoka wengine wengi wa ndani na nje.

Ikitokea mwanasoka akarudi vizuri moja kwa moja ni bahati. Naombea miongoni mwa wachezaji watakaoingia katika mkumbo wa kurudi vema moja kwa moja awe Tshabalala.  Unawezaje kupoteza kipaji cha aina yake?  Wapo wachezaji wengi wanaocheza katika nafasi yake lakini sio kwa utulivu wake au kwa kipaji chake maridhawa. Anapopotea mchezaji kama yeye, tena kwa majeruhi na sio kwa tabia mbovu, inakuwa hasara kwa taifa. Labda tuombee tu kuwa kadiri atakavyoendelea kucheza mechi nyingi ndivyo atakavyojiamini. Huwa inatokea. Akiingia katika mkumbo mwingine itakuwa hasara.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alilazimika kuachana na Eduardo kwa sababu alishindwa kurekebisha hisia zake na kuwa mchezaji yuleyule aliyekuwa awali baada ya kuvunjika mguu. Binafsi namuombea Tshabalala awe yuleyule.

Namuombea sio tu kwa sababu ya uwezo wake, lakini pia kwa tabia zake. Utatoa wapi mchezaji maridadi mwenye kipaji halafu mpole ana nidhamu na muungwana, hasa katika soka letu ambalo wanasoka wanajikuza wenyewe?