Ishu ni Okwi, Chirwa

Staa wa Simba, Emmanuel Okwi 

NANI kasema Mwarabu hafungiki? Siyo kwa pacha ya ushambuliaji ya Simba inayoundwa na Emmanuel Okwi na John Bocco ambao, kwa pamoja hadi sasa msimu huu wameshapachika mabao 30 katika mashindano yote.

Wawili hao ndio habari ya mjini Msimbazi kwani kwenye mechi ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Gendarmerie, walifunga mabao manne kati ya matano ya timu yao na kuipeleka raundi ya kwanza ambako watakutana na Al Masry ya Misri.

Hofu kubwa kwa watu wa Simba ni mzimu wa Waarabu unaozisumbua timu za Tanzania, lakini rekodi za Bocco na Okwi zimemtia ndimu kocha Mfaransa, Pierre Lechantre aliyeahidi kuendelea kuwapanga wawili hao pamoja.

Licha ya Bocco kuwa benchi dhidi ya Gendarmerie Jumanne kutokana na majeraha ya goti, Okwi aliendelea kupachika bao pekee la ushindi.

“Bocco na Okwi wanaelewana vizuri wakicheza pamoja, tunawategemea kwenye mechi zijazo na nitaendelea kuwapanga pamoja dhidi ya Al Masry, ila mechi itakuwa ngumu na tunapaswa kujipanga,” alisema Mfaransa huyo.

Okwi ndiye mtamu zaidi msimu huu kwani, ameifungia Simba mabao 16 katika mashindano yote wakati Bocco aliyekosa mechi kadhaa amefunga 14.

ISHU YA CHIRWA

Kwa upande wa Yanga iliyopangwa na Township Rollers ya Botswana katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mastaa wake Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa wanakabiliwa na jukumu zito la kuibeba timu hiyo itinge hatua ya makundi.

Chirwa na Ajibu ndio wamekuwa wakombozi wa Yanga msimu huu, wakifunga mabao 19 katika mashindano yote, hivyo kukabidhiwa mikoba ya mchezo huo.

Pamoja na Chirwa kukosekana kwenye mechi iliyopita, Ajibu aliifungia Yanga bao pekee ilipotoka sare ya 1-1 na St. Louis matokeo yaliyowabeba na kuwapeleka raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla wa 2-1.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina, anaumiza kichwa juu ya kuendelea kukosekana kwa Amissi Tambwe na Donald Ngoma walioifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016, lakini sasa makali yao yamepungua kwa majeraha.

Chirwa amekuwa mtamu zaidi akifunga mabao 12 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu huku Ajibu akifunga saba.

MABAO MAKALI

Kitu kingine ambacho kimezipa Simba na Yanga kiburi ni uwezo mkubwa wa mastaa hao kufunga mabao makali yanayohitajika zaidi katika mechi ngumu za kimataifa.

Kati ya mabao makali ya Okwi msimu huu ni lile la mpira wa adhabu wa dakika za mwishoni dhidi ya Mtibwa. Mengine ni dhidi ya Mwadui, mawili dhidi ya Singida United na alilowapachika Azam hivi karibuni, yote ya Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa Chirwa aliyekwishafunga Hat Trick mbili msimu huu, bao lake maridadi ni alilofunga dhidi ya Mbeya City akichopu mpira uliompita mbali kipa Fikirini Bakari na kwenda kwenye kona ya goli.

Mabao mengine makali ya Chirwa ni dhidi ya Azam alilomhadaa kipa Razack Abalora akapishana na mpira, dhidi ya Njombe Mji na alilofunga dhidi ya Majimaji wiki iliyopita.

WADAU WAFUNGUKA

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe, alisema muunganiko wa Bocco na Okwi ni tija kwa Simba na unavutia kutazama.

“Ni wachezaji wanaofunga kila wapatapo nafasi. Mungu awasaidie wasiumie,” alisema Mwakingwe aliyeichezea Simba kwa miaka tisa.

Naye kiraka wa zamani wa Yanga, Kenny Mkapa, alisema uwepo wa Chirwa unaifanya Yanga kuendelea kutabasamu.

“Ajibu si mfungaji sana, mara nyingi hupenda kucheza na jukwaa tangu akiwa Simba, lakini si Chirwa,” alisema.