Ihefu FC kuizawadia Yanga viroba vya mchele

Mbeya. Mashabiki wa Yanga Mkoa wa Mbeya wameanza mkakati wa kuhakikisha timu yao inapata ushindi kwenye mechi yake ya Kombe la Shirikisho ‘FA’ dhidi ya Ihefu FC ya wilayani Mbarali ikatakayochezwa mwishoni mwa mwezi huu.

Viongozi waandamizi wa matawi yote ya Yanga-Mbeya wakiongozwa na mwenyekiti wa mashabiki hao Mkoa wa Mbeya, Lusajo Kifamba walikutana juzi kwa ajili ya kuweka mikakati yao.

Akizungumza na gazeti hili, Kifamba alisema kwa mfumo wa soka la sasa nchini hawawezi kuidharau Ihefu kwa kigezo cha kutokuwa na jina wala uzoefu katika mashindano hayo kwani lolote linaweza kutokea hivyo hawataki timu yao iaibike.

“Kweli tulikuwa na kikao chetu kupanga mikakati mbalimbali yanayohusu klabu yetu kwa sisi kama mashabiki wa Mbeya. Lakini kubwa zaidi ni maandalizi ya kuipokea timu yetu na kuhakikisha tunapata ushindi dhidi ya Ihefu na hatuawezi kuidharau mechi kwani mashindani haya yana umuhimu sana kwetu Yanga, ukizingatia tulishapigwa kule Zanzibar Kombe la Mapinduzi,”alisema Kifamba.

Wakati  mashabiki hao wakiweka bayana mikakati yao kuiangamiza Ihefu FC,  Katibu Mkuu wa Ihefu FC, Athuman Mndolwa alisema  timu yake ipo vizuri na hawana wasiwasi kwa Yanga na watahikisha wanaizawadia timu hiyo zawadi ya mabao.

Mndolwa alisema, “Tupo vizuri sana, Yanga tunaiheshimu ni timu kubwa lakini hilo ukongwe na uzoefu wake kwenye michuano mbalimbali hauwezi kutofanya sisi tukahofia chochote. Tutapambana hadi dakika ya mwisho. Tunajua mikakati yao lakini na sisi tumejipanga na wachezaji wapo vizuri kisaikolojia kuelekea mechi hiyo.”